WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuna haja ya kutafuta mbinu mpya ya kukieneza Kiswahili baada ya kuwa kimepata hadhi ya kimataifa.
“Kadiri Kiswahili kinavyoendelea kupata hadhi ya kimataifa, ni muhimu sasa kuanza kutazama hatua inayofuata ya kukieneza duniani. Mataifa mengi yamefanikiwa kueneza lugha na utamaduni wao kupitia vituo vya utamaduni vilivyoanzishwa katika nchi mbalimbali duniani,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Julai 7, 2026) wakati akizungumza na washiriki waliohudhuria kilele cha Maadhimisho ya Tano ya Siku ya Kiswahili Duniani kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za makao makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa.
“Serikali itaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kupitia elimu, tafiti, uchapishaji, tafsiri, teknolojia za kidijiti na diplomasia ya lugha. Tutaendelea kushirikiana na UNESCO, nchi mbalimbali, vyuo vikuu, taasisi za kimataifa na wadau mbalimbali katika kuendeleza lugha hii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema sasa hivi Kiswahili kimeshatambulika kuwa lugha rasmi ya EAC na SADC. “Kiswahili ndiyo utambulisho wetu wana jumuiya ya Afrika Mashariki. Mtu akiongea Kiswahili anajulikana kuwa anatokea Tanzania, Burundi, Congo au Sudan Kusini. Na pia kimekuwa moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU),” amesema.
“Si hivyo tu, sasa hivi Kiswahili kinatambulika kuwa ni lugha rasmi ya mikutano mikubwa ya UNESCO kutokana na pendekezo lililopitishwa kwa kaulimoja Novemba, 2025 wakati wa Mkutano Mkuu wa 43 wa UNESCO, uliofanyika Samarkand, Uzbekistan.”
Amesema kwa mujibu wa wataalamu wa lugha, Kiswahili kinazungumzwa na watu kati ya milioni 300 hadi milioni 500 na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kutokana na matumizi yake katika elimu, biashara, vyombo vya habari, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii.
“Hali hiyo inaonesha kwamba Kiswahili siyo mali ya Watanzania pekee bali ni urithi wa Afrika na zawadi ya Afrika na dunia. Kiswahili kinaunganisha watu, Kiswahili kinaunganisha biashara, Kiswahili kinaunganisha jamii,” amesisitiza.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Prof. Khaled El-Enany aliwaeleza washiriki wa maadhimisho hayo kwamba shirika lake limesaidia kufadhili uandaaji wa kamusi ya Kifaransa kwenda Kiswahili.
“Mbali na matumizi ya kawaida kwa watalii au watu wanaojifunza lugha, tunatarajia kwamba uwepo wa kamusi hiyo na nyaraka nyingine kutasaidia kuongeza fursa kwa walimu na wanafunzi wanaojifunza Kifaransa na Kiswahili,” amesema.
Amesema uzuri wa Kiswahili ni lugha ambayo imekuwa ikiendelea kukua na kuvuka mipaka bila kupoteza uasili wake na imeunganisha watu bila kulazimika kuvuka mipaka ya nchi zao.
Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda alisema Tanzania ina lugha za makabila zaidi ya 150 katika maeneo mbalimbali lakini wananchi wake wameweza kuunganishwa na lugha moja ya Kiswahili.
Alisema wakati jijini Paris, Ufaransa wakiadhimisha kilele cha maadhimisho hayo na kongamano la pili lililoandaliwa na UNESCO kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, nchi nyingine tatu za Uingereza, Algeria na Burundi nazo pia leo zimeadhimisha makongamano kama hayo.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Bw. Saidi Othman Yakub alisema maadhimisho hayo ya tano ambayo yanafanyika sambamba na Kongamano la Pili la Siku ya Kiswahili Duniani, yamevutia washiriki zaidi ya 300 kutoka nchi 16 duniani.
Amezitaja nchi hizo kuwa ni Comoro, Tanzania, Ujerumani, Marekani, Canada, Uingereza, Italia, Luxembourg, Sweden, Ubelgiji, Austria, Uturuki, Misri, Kenya, Uganda na wengi kutoka Tanzania.
“Tangu tarehe 4 Julai hadi leo tarehe 7 Julai, 2026 tumeshuhudia shughuli mbalimbali zilizolenga kuendeleza na kukitangaza Kiswahili duniani. Shughuli hizo zilijumuisha matembezi ya hamasa katika mitaa maarufu ya Jiji la Paris, hafla za vyakula vya Kiswahili kwa Diaspora, kongamano kuhusu nafasi ya Kiswahili katika biashara na uchumi, semina na warsha mbalimbali hapa UNESCO.
Amesema waliandaa pia tamasha la Usiku wa Mswahili lililofanyika chini ya Mnara wa Eiffel kandokando ya Mto Seine, maonesho ya filamu na chakula pamoja na kazi za Kiswahili.






No comments:
Post a Comment