Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, July 31, 2012

SAKATA LA DR. ULIMBOKA LAIBUKA TENA BUNGENI KWA KASI...!


Kizitto Noya, Dodoma
SAKATA la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven Ulimboka, limeibuka upya bungeni baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kuitaka Serikali itoe majibu ya kina kuhusu watendaji wake kutajwa kuhusikana na tukio hilo.

Kambi hiyo pia imeitaka Serikali ieleze sababu za watendaji hao kutokamatwa hadi sasa na kuhojiwa na vyombo vya dola, wakati kuna taarifa kuwa wanafahamika.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu  hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katia mwaka wa fedha wa 2012/13,  Conchesta Rwamlaza alisema, haiwezekani Serikali kuendelea kukaa kimya wakati watendaji wake wanatajwa kuhusika katika tukio hilo.

Rwamlaza alikuwa akizungumza kwa niaba ya msemaji wa kambi hiyo, Dk Antony Mbassa, ambaye alitaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu kubaini ukweli.

"Aidha kwa kuwa Serikali imetuhumiwa kuhusika, kambi rasmi ya upinzani, inasisitiza haja ya kuundwa kwa tume huru ili kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo. Taarifa iliyotolewa na polisi kuhusu kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa raia wa Kenya, haipaswi kutumika kama kisingizio cha kuzuia mjadala na haiwezi kuwa kizuizi cha uchunguzi huru kuendelea kufanyika," alisema Rwamlaza.

Katika hatua nyingine, Rwamlaza alilaani kitendo cha Bunge kuzuia mjadala wa kibunge kuhusu tukio la kutekwa kwa D Ulimboka, akisema hata kama limefanya hivyo kwa kutumia kanuni, siyo sahihi.
Kambi hiyo ilisema tukio la Ulimboka linapaswa kufikishwa  bungeni ili lijadiliwe na kwamba Bunge halipaswi kuwekewa vikwazo vya kikanuni katika kujadili matatizo ya wananchi.

Kambi hiyo ilienda mbali zaidi na kukituhumu kiti cha Spika kwamba kinachangia mgogoro wa madaktari unaoendelea nchini, kwa kuzuia mijadala iliyoombwa na wabunge kuhusu suala hilo ambalo hatima yake ni kuwasitishie leseni madaktari 319.

"Kama Kiti kingetoa fursa kwa Bunge kujadili na mwisho kutoa ushauri au maazimio yake kwa Serikali, jambo ambalo ndio wajibu wetu kwa mujibu wa katiba ibara ya 63, mgogoro huo usingeendelea kudumu kwa muda mrefu na kuleta athari zaidi katika sekta ya afya," alisema.

Rwamlaza alisema "kanuni zinazolizuia Bunge kujadili masuala ya wananchi kwa kisingizio kuwa masuala hayo yako mahakamani, zinadumaza demokrasia ya nchi yetu, zinalipora Bunge haki yake ya kikatiba ya kuisimamia Serikali na zinawakandamiza wananchi wanyonge ambao hawana pa kusemea isipokuwa kupitia Bunge lao."

Alielezea kushangawa kwake na Bunge kuzuiwa kujadili suala hilo kwa maelezo kuwa liko mahakamani, wakati Rais Jakaya Kikwete alilizungumzia katika hotuba yake kwa taifa, ya Julai mosi mwaka huu. na kulitolea maagizo mbalimbali.

"Kambi ya upinzani inataka kujua kama kitendo cha Baraza la Madaktari Tanganyika kusitisha usajili kwa madaktari 319 kuanzia Julai 11 mwaka huu ni sahihi wakati madaktari hao walikuwa wameshtakiwa mahakamani kwa shauri hilo," alisema.

Alisema kutokana na upungufu huo, kambi ya upinzani inapendekeza Bunge liazimie kuwa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma kwa Jamii, iliyoshughulikia mgogoro kati ya Serikali na Madaktari, iwasilishwe bungeni taarifa ya jambo hilo  na kujadiliwa kabla ya kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo.

"Hatua hiyo italiwezesha pia Bunge kupitisha maazimio ya kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu namna ya kushughulikia vyanzo vya migogoro katika sekta ya afya," alisema na kuongeza;

'Kitendo cha kuwadharau, kuwadanganya madaktari na hatimaye kuwafutia leseni madaktari 319 wa mafunzo kwa vitendo, ni kujikanganya kwa Serikal. Ni uamuzi unaoonekanaa umechukuliwa kwa kukomoa na kwa ubabe bila kujali maslahi ya taifa na afya za wananchi.
Mgogoro mzima unaashiria uwezo finyu wa Serikali katika kutatua migogoro kwa njia ya majadiliano na ukosefu wa dhima ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM," alisema.

Alisema kambi ya upinzania, inasikitishwa na kitendo cha Serikali kushindwa kutumia busara katika kutafuta ufumbuzi wa madai ya vitendea kazi na stahili za madaktari, jambo ambalo lilisababisha migomo ya madaktari nchini.

Hata hivyo akiwasilisha hotuba yake ya wizara bungeni jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi, alisema Serikali imesikitishwa na tukio la kutekwa, kuteswa na kutelekezwa msituni kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk  Steven Ulimboka.

"Serikali inatoa pole kwa ndugu Ulimboka na inamtakia kupona haraka ili aunganike na familia yake," alisema Dk Mwinyi.

Mapema waziri huyo alieleza historia ya mgogoro wa madaktari na Serikali akifafanua kuwa kwa upande wake, Serikali ilijitahidi kadri ilivyoweza  kuhakikisha kuwa unamalizika. Mwisho

 

No comments:

Post a Comment