Spika wa Bunge, Anne Makinda
Bunge liimeazimia serikali ilete Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kurudishwa bungeni chini ya hati ya dharura katika mkutano wa tisa ili ifanyiwe marekebisho mbalimbali ikiwemo la kifungu cha fao la kujitoa kabla ya umri wa kustaafu.
Lilifikia uamuzi huo baada ya Mbunge wa Kisarawe, Seleimani Jafo (CCM), kuwasilisha hoja yake ya kutaka sheria hiyo ili watu watakaostaafu chini ya umri wa miaka 55.
Alitaka Bunge liazimie kuwa katika mkutano wa tisa iwasilishe mabadiliko ya sheria hiyo kwa ajili ya kuweka fungu la kujitoa katika mifuko hiyo anayeacha ama kuachishwa kazi kabla ya kufikisha umri wa miaka 55 ama 60.
Pia alitaka kifungu kingine kinachohusu kuruhusu watumishi kutumia sehemu ya mafao yao ya uzeeni kwa ajili ya kulipia shughuli nyingine yoyote kwa ajili ya ujiwekea mazingira mazuri uzeeni.
“Katika Muswaada iondoe vifungu vya sheria vinavyoweka mamlaka ya kumtaka mtumishi kuwasilisha maombi kwa mheshimiwa Rais utaratibu uliojaa urasimu wa kupata msamaha kwa fao la kujitoa,” alisema na kuongeza:
“Serikali iagize migodi hasa mgodi wa Bulyakuru kutosimamisha mfanyakazi yoyote aliyehoji kwa kina juu ya mafao yao baada ya kupata mshutuko wa kutoruhusiwa mafao yao baada ya kuacha kazi ama kuachishwa.”
Jafo ambaye alikuwa wa kwanza kuomba mwongozo wa Spika kuhusiana na utata huo, alisema wakati Watanzania wakisubiri kuletwa kwa muswaada wa marekebisho katika mkutano wa tisa, Serikali ilete waraka wa kuelekeza mifuko ya jamii kuendelea kuwalipa watumishi wanaostaafu kabla ya muda wa umri huo uliowekwa kisheria kwa kupewa fao la kujitoa.
Alitaka pia serikali iangalie upya kanuni ya kukokotoa mafao ya watumishi wanaostaafu ili kuepusha kuzua balaa jingine katika siku za usoni na ingalie utaratibu wa kutoa namba ya Tin ili watambulike kama walipa kodi halali.
“Serikali isipowasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama nilivyoomba, nitawasilisha Muswada binafsi wa mbunge ili kuwezesha marekebisho hayo muhimu niliyopendekeza,” alisema Jafo.
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo ambayo iliungwa mkono kwa kushangiliwa na Bunge zima, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwahoji wabunge kama wanaoafiki hoja hiyo kuwa inafaa katika uendeshaji wa serikali wasema ndio jambo ambalo liliwafanya kuikubali.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment