Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, August 28, 2012

Wachimbaji watano wajeruhiwa kwa risasi na Wawekezaji wa Tanzanite One, Mirerani...!
WACHIMBAJI wadogo watano wa madini ya Tanzanite, wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na majabali, kulikofanywa na walinzi wa Kampuni ya Wawekezaji wa Tanzanite One, kufuatia vurugu kubwa za kurushiana risasi wakiwa chini ya migodi ya madini, huko Mererani, mkoani Manyara.

Vurugu hizo, zilitokea juzi baada ya walinzi hao wa Tanzanite One, kuwavamia wachimbaji wa kampuni ya Manga Gems (T) Ltd wakiwa chini  ya mgodi wakichimba madini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Mkuu wa Mgodi huo ,Abdallah Mbaruku, aliwataja wachimbaji waliojeruhiwa kuwa ni, Fidelis Kefas, Peterson Richard, Remmy Manga, Kiberenge Laizer na Mahadhi Salum.
Mbaruku alisema wachimbaji hao, walikuwa chini ya ardhi, umbali wa meta 465 na kwamba , walishangaa kuvamiwa na walinzi wa Tanzanite One na kuanza kurushiwa risasi kwa madai ya kuwa walikuwa wamevamia mgodi wao.

"Sisi tulikuwa kwenye eneo letu na tuna leseni  ya uchimbaji wa mgodi wetu, PML No.0004678 sasa tumeshangazwa na hawa wanaojiita wawekezaji kuvamia eneo letu na kupiga risasi, majabali na kurusha mabomu dhidi ya vijana wangu,"alisema Mbaruku.

Alisema licha ya kuwapiga vijana hao, walinzi hao pia walifungulia maji ambayo yaliingia ndani ya  mgodi, jambo linalokiuka maagizo ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele ambaye amepiga marufuku wawekezaji hao, kuwamwagia maji wachimbaji wadogo wakiwa chini ya ardhi.

Meneja msaidizi  wa mgodi huo, Athuman Miraji alisema kitendo cha wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One,kuingia na silaha chini ya mgodi ni cha kuvunja sheria ya madini.
Wachimbaji wengine wadogo,Kelvin Lymo,Remmy Manga, waliomba Serikali kutotoa tena kibali kwa kampuni ya Tanzanite One, kwa maelezo kuwa imeshindwa kuimarisha mahusiano kati yake na wachimbaji wadogo wa Mererani.
"Kwanza leseni yao imekwisha,tunaomba wasipewe tena leseni  kwani hata uchimbaji wao, hauna tofauti na sisi,"alisema Lyimo.

Wachimbaji, pia waliomba Wizara ya Nishati na Madini na wizara ya mambo ya ndani, kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na vitendo vya ukiukwaji sheria unaofanywa na kampuni hiyo.
 Meneja mkuu wa kampuni ya Tanzanite One, Wessel Marais hakupatikana jana, kuelezea chanzo cha mgogoro huo, baada ya kuelezwa yupo nje ya nchi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa, alithibitisha kupokea taarifa za mgogoro kati ya Kampuni ya Tanzanite One na Manga Gems(T) Ltd na kwamba uchunguzi unaendelea.
 

No comments:

Post a Comment