TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
PINDA: NENDENI KUKAGUA BARABARA WAKATI ZINAJENGWA
*Azindua Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Katavi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Katavi kuweka ratiba ya kukagua ujenzi wa barabara na madaraja badala ya kusubiri kuletewa taarifa na watendaji.
Amesema hayo leo mchana (Alhamisi, Agosti 30, 2012) wakati akizungumza na wajumbe wa Bodi hiyo kwenye mkutano wa kwanza wa Bodi hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Idara ya Maji mjini Mpanda. Waziri Mkuu aliizindua rasmi Bodi hiyo leo.
“Si vibaya mkiamua kuipa Bodi hii ratiba na mkaamua kwenda kuona hali halisi ya ujenzi wa barabara na madaraja au makalavati badala ya kusubiri kuletewa taarifa na watendaji wa idara,” alisema.
Alisema kuna umuhimu wa kujiwekea mazoea ya kwenda kuangalia barabara au madaraja wakati zinajengwa ili kujiridhisha na kiwango cha kazi kinachofanyika pale. “Unaweza usiwe mtaalam wa ujenzi lakini kama kazi ni mbovu si utaiona, si utapata nafasi ya kuhoji kulikoni au kuarifu mamlaka husika?” aliongeza.
Alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012 (wakati huo mkoa huu ukiwa ni Wilaya ya Mpanda) zilitolewa sh. bilioni 5.5/- ambazo zimetumika kujenga barabara kwa viwango tofauti vyenye jumla ya kilometa 1,186.62 na madaraja ama makalvati makubwa 52.
Katika kwa mwaka huu wa fedha zimetengwa sh. bilioni 10.65/- ambazo zimepangwa kujenga barabara kwa viwango tofauti zenye urefu wa kilometa 1,310.06 na madaraja pamoja na makalvati makubwa 58.
Alionya kwamba changamoto kubwa waliyonayo wajumbe wa bodi hiyo kwenye suala la kuhakikisha fedha inatumika kama ilivyopangwa, ni uadilifu wa watendaji kwenye vyombo vya usimamizi la sivyo wataibiwa fedha na kuishia kubakia na barabara ambazo ziko chini ya kiwango.
“Changamoto kubwa mliyonayo ni kuona fedha iliyopangwa inatumika ipasavyo. Ni vema wajumbe wa Bodi mkawa ‘akina Tomaso’, mwende mkakague japo madaraja na makalvati mawili au matatu. Mkifika mtabaini kama limejengwa kwa kiwango kinachostahili, la sivyo mtaishia kukabidhiwa daraja lakini baada ya siku mbili mnasikia limesombwa na maji,” alionya.
Alimtaka Meneja wa TANROADS wa mkoa huo, Mhandisi Isaack Kamwele ahakikishe anafuatilia suala la mizani ya barabarani hata kama ni ya kuhamishika ili kudhibiti ubebaji wa mizigo mizito (overloading) unaofanywa na wasafirishaji wa mazao kutoka eneo la Bonde la Ziwa Rukwa.
“Changamka tupate mizani ya kupima uzito kwa sababu huwezi kumkamata dereva kwa kuzidisha uzito bila kupima kwanza japokuwa kwa macho unauona kabisa kwamba mzigo huu ni mkubwa… tupate japo miwili kwa kuanzia. Mmoja uende barabara ya Mpanda – Inyonga na mwingine kwenye barabara ya kwenda Bonde la Ziwa Rukwa ambako wanasomba mazao kwa wingi,” alisema.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzindua Bodi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Rajab Rutengwe alisema mkoa huo una kilometa 2,430 za barabara na madaraja 117. Kati ya hizo kilometa 1,101.44 zinahudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS), kilometa 1,074.10 zinahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda wakati kilometa 251.5 zinahudumiwa na Halmashauri ya Mji Mpanda. “Asilimia 42 ya mtandao wa barabara ni nzuri, asilimia 20 ni za wastani na asilimia 38 ni mbaya,” alisema.
Akizungumzia changamoto zinazoukabili mkoa huo, Dk. Rutengwe alisema ofisi ya TANROADS ya mkoa huo inahitaji walau magari matatu ili iweze kufanya kazi kuliko ilivyo hivi sasa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Pinda mara baada ya kuwasili Mpanda mjini akitokea kijijini kwake Kibaoni, alikwenda kwenye nyumba ya Askofu iliyoko Kanisa la Mt. Maria Imakulata la mjini hapa kusaini kitabu cha maombolezo ya kifo cha Mhashamu Askofu Pascal William Kikoti ambaye alifariki dunia Agosti 28, mwaka huu katika Hospitali ya Bugando, jijini Mwanza.
Mwili wa Mhashamu Askofu Kikoti ambaye alikuwa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, unatarajiwa kuwasili Mpanda kesho (Ijumaa, Agosti 31, 2012) na mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho kutwa (Jumamosi, Septemba mosi, 2012.)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 30, 2012.
No comments:
Post a Comment