Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, September 4, 2012

APIGWA NA KUMWAGIWA MAJI YA MOTO KWA KUTUHUMIWA KUBAKA...!

Mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam, Salehe Abdallah (35), amefanyiwa unyama wa kutisha baada ya kukatwakatwa mapanga na kumwagiwa maji ya moto na kutembezwa hadharani bila nguo.
Tukio hilo la kusikitisha linalodaiwa kufanywa na jirani yake, lilifanyika kwa muda wa masaa sita kuanzia saa 3:00 usiku hadi saa 8:00 usiku huko eneo la Mbezi Makondeni Wilaya ya Kinondoni.
Ilielezwa kabla ya kufanyiwa unyama huo, Abdallah alitekwa nyara na jirani yake huyo kisha kumfunga kamba mikononi.
Akizungumza kwa shida akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) wodi namba 23 jengo la Sewahaji juzi akipatiwa matibabu, Abdallah alisema jirani yake huyo (jina limehifadhiwa) alimfanyia unyama huo kwa kumwagia maji ya moto yaliyosababisha kuungua sehemu zake za siri baada ya kumtuhumu kubaka binti yake.
Alisema siku ya tukio alifuatwa na watu watatu nyumbani kwake na kumueleza anatakiwa na jirani yake huyo ambaye ni mfanyabiashara ili akampatie kazi ya kufyatua matofali.
Alieleza baada ya kuelezwa jambo hilo, aliondoka na watu hao kuelekea nyumbani kwa mfanyabiashara huyo bila ya wasiwasi wowote, akiamini hakuna kitu chochote kibaya kitakachomkuta mbele yake.
Wakiwa njiani watu hao walianza kumdadisi mambo mbalimbali, kitu ambacho kilimfanya aanze kupata wasiwasi kuwa huko anakokwenda sio kwa ajili ya kazi kama walivyomuambia awali.
Baada ya kufika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo, watu hao walimlazimisha kuingia ndani kwa maelezo kuwa huko ndiko alikokuwa akihitajika, hata hivyo alipinga kuingia ndani na kuomba kama kweli kulikuwa na mtu anataka kumpatia kazi hiyo wazungumzie nje.
"Niligoma kuingia ndani kwa sababu tayari nilikuwa na wasiwasi, niliomba kama mazungumzo ya kazi tufanyie pale pale nje, kitu ambacho watu wale walikataa wakang'ang'ania niingie ndani kwa nguvu," alisema Abdallah.
Abdallah alisema kuwa aliwasisitiza watu wale kuwa hataweza kuingia ndani kama walivyotaka, lakini watu hao walimkamata kwa nguvu na kumfunga kwa waya wa umeme mikononi na kuanza kumpatia kipigo.
Katika kipigo hicho, watu hao walitumia mapanga kwa kumkatakata sehemu mbalimbali ya mwili na kumjeruhi vibaya.
Wakati anafanyiwa ukatili huo, mara alitokea mfanyabiashara huyo akiwa pamoja na mtoto wake anayedai alibakwa wakitokea hospitali. Watu hao baada ya kumuona walimuuliza kama amepata majibu ya vipimo kutoka kwa daktari, mfanyabiashara huyo aliwajibu huko alipokwenda hawakuona alama yoyote inayoonyesha mtoto huyo alikuwa amebakwa.
Pamoja na jibu hilo watu hao waliendelea kumpiga akishirikiana na mfanyabiashara huyo, kisha walichukua sufuria la maji iliyokuwa na maji ya moto na kumwagia mwilini.
Alisema licha ya kujaribu kukwepa maji hayo, yalimwagikia sehemu ya tumboni hadi sehemu zake za siri na kumuunguza vibaya.
"Nilihisi maumivu makali sana, niliona jinsi ya ngozi ya mwili inavyochunika na kuniacha nikiwa na jeraha kubwa" alisema.
Kama vile haitoshi, watu hao walimvua nguo zote na kuendelea kumchapa viboko na baada ya kuhakikisha amekuwa taabani, walimuamuru kuinuka na kumtembeza mitaani akiwa mtupu hadi kwenye kituo cha polisi kilichopo eneo hilo.
Alisema mara alipofikishwa kituoni hapo aliishiwa nguvu na kuzirai.
Mmoja wa wauguzi aliyekuwa zamu wakati chanzo chetu kilipokwenda kumuona mgonjwa huyo (hakutaka jina lake liandikwe gazetini) alisema Abdallah alifika hapo akiwa chini ya ulinzi wa polisi huku akiwa na hali mbaya, lakini walishangaa baada ya siku chache polisi hao walitoweka na kumtelekeza wodini.
Alisema mwanzoni waliamini kweli ametenda kosa hilo kutokana na kulindwa na polisi, lakini hatua ya polisi hao kumuacha huru inaonyesha wameshapata ukweli wa tukio hilo.
"Hali yake sio mbaya sana, anaweza kunyanyuka na kula akiwa peke yake, tuna imani akiendelea na hatua hii ataweza kuondoka wodini," alisema muuguzi huyo.
Afisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alipotafutwa kwa kutumia simu yake ya mkononi hakuweza kupatikana baada ya simu yake kuzimwa.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema ofisi yake bado hajapelekewa suala hilo na aliahidi kulifuatilia ili kujua ukweli wa tukio hilo.

Chanzo: Mwandishi wetu

No comments:

Post a Comment