Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, September 10, 2012

Askofu Hotay akabidhiwa Dayosisi

Mchungaji Stanley Hotay.

Kanisa la Anglikana Tanzania limewapongeza waumini wa Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), kwa kuvumilia aibu iliyofanywa na waumini wake watatu kwa lengo la kuzuia kazi ya Mungu isifanyike baada ya kufungua kesi Mahakama Kuu ya Arusha, kupinga kupewa uaskofu na dayosisi Mchungaji Stanley Hotay.

Hata hivyo, Hotay alipewa uaskofu Juni mwaka jana, licha ya pingamizi hilo lakini hakuweza kupewa dayosisi hadi jana kwa kuwa kesi ya msingi ilikuwa bado ikiendelea mahakamani.

Jaji Fatma Massengi aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alitoa hukumu yake Septemba 5, mwaka huu ambapo alitupilia mbali pingamizi hilo hatua ambayo imeliwezesha kanisa hilo kufanya ibada maalum ya kumkabidhi kiti na dayosisi.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Lothi Oilevo, Godfrey Mhone na Frank Jacob ambao ni waumini wa dayosisi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine  walidai kwamba Hotay alikuwa ameghushi umri ili aweze kuchaguliwa.

Akihubiri katika ibada maalum ya kumkabidhi kiti na dayosisi katika Parish ya Christ Church jijini hapa, Dk. Mokiwa alinukuu Injili ya Luka Mtakatifu 23:34 inayosema, “Yesu akasema; Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.”

Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na maaskofu wengine wa kanisa hilo kutoka Newala, Morogoro, Zanzibar, Tanga na Kajdyo nchini Kenya pamoja na maskofu na wawakilishi wa madhehebu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati,  Menonite na TAG, mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.

Alisema “waumini hawa wamesamehewa kabisa na kanisa na hata wale waliotoa fedha kwa ajili ya kuwezesha pingamizi hizo nao pia tunawasamehe.” 

“Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki kabisa katika shughuli zao za kila siku na waweze kumjua Kristo, napenda wampe ushirikiano na wawe pamoja na askofu…tunaishi katika kipindi cha msamaha,” alisema.

Aliipongeza mahakama kwa hukumu iliyotoa kwa maelezo kuwa imempa Kristo ushindi aliokuwa akistahili.

“Siku zile (wakati wa pingamizi) mioyo yetu ilifadhaika sana, unajua nina magonjwa matatu, kisukari, shinikizo la damu na hypetention, ulikuwa ni wakati mgumu sana kwangu na vyombo vya habari vikazidisha maumizi zaidi kwa kusema nimeitunishia misuli mahakama.

“Kama kuna wakati nilipandwa na kisukari hata macho yangu yakawa hayaoni vizuri ni pale ambapo nilipotakiwa na mahakama kufika mahakamani,” alisema na kufanya waumini mara kwa mara kucheka kwa furaha.

Akimkabiti kiti, Dk. Mokiwa alisema, “Kanisa la Anglikana linao utaratibu wake wa kuwapata na kuwatuma kazini viongozi iliowapata na leo (jana) inamalizia kutekeleza kanuni ya kumweka kitini ambayo ilikuwa imezuiwa kwa kuwekewa pingamizi mahakamani.”

Baada ya kukabidhiwa kiti, Mchungaji mwandamizi wa parishi hiyo, David Mnankali, alimkabidhi Askofu Hotay fimbo ya kichungaji ya kiaskofu na kisha akamkabidhi kwa wachungaji na mashemasi wote wa dayosisi wampokee na baadaye walikula kiapo cha utii mbele yake.

Akizungumza, Askofu Hotay naye alisema, “mimi nimewasamehe wale wote kwa yale yote waliyoyafanya…nashukuru sana sasa yamekwisha, lakini wao ndio walikuwa na kazi kubwa zaidi kuliko mimi.”

No comments:

Post a Comment