Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, September 18, 2012

MAGEREZA YA TANGA YATAFUTA SULUHU NA WAFUNGWA...!

Jeshi la Magereza mkoani Tanga limethibitisha kuwapo mgomo wa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa katika Gereza la Maweni na kusema linaendelea kutafuta mwafaka kuhusiana na madai yao mbalimbali yaliyosababisha wagome.
 

Madai hayo ni pamoja na kunyimwa matibabu, kitendo ambacho wamedai kimesababisha wenzao wawili kufariki dunia kutokana na kukosa huduma hiyo gerezani.

“Wapo kweli (wafungwa), ambao wamegoma tangu jana (juzi) waliohukumiwa kunyongwa,” alisema Mkuu wa Jeshi hilo mkoani humo, Rita Mallya, alipotakiwa na NIPASHE kuthibitisha kuhusu kuwapo kwa mgomo wa wafungwa hao au la.

Kutokana na hali hiyo, alitaka apewe muda wa kuchunguza ili kupata ukweli kuhusu madai ya wafungwa hao kunyimwa matibabu na kwamba, anaendelea kuzungumza nao ili kufikia mwafaka kuhusu madai yao ya kunyang’anywa redio, na hivyo kunyimwa haki ya kupata habari wawapo gerezani.

Alisema awali, waliona sio vizuri kila mfungwa kuwa na redio katika bweni moja licha ya kutokuwapo redio ya pamoja gerezani, hivyo ikaamuliwa wapunguziwe redio.

Hata hivyo, alisema hakuna mfungwa aliyenyang’anywa vyombo vya chakula, badala yake kilichofanywa na mkuu wa gereza ni kupunguza mfungwa mmoja kumiliki vyombo vingi na kuwapa ambao hawana kabisa.

Kuhusu madai ya wafungwa kukosa chakula, alisema hayana ukweli, kwani wanaendelea kupata vyakula vyote ambavyo viko ndani ya uwezo wa Magereza.

Alisema madai ya wafungwa walioathirika na ugonjwa wa ukimwi kupata chakula mara moja badala ya mara mbili kwa siku, alisema hayana ukweli, badala yake wamekuwa wakipata chakula kama kawaida ikiwamo mboga za majani na maziwa.

Pia alisema wamezuia kila mfungwa kumiliki ndoo, kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha ndoo kujaa bwenini na hivyo, kukosekana hewa.

Kuhusu madai ya ukosefu wa vyandarua vilivyotolewa na serikali, ambavyo wafungwa wamekuwa wakiuziwa kwa Sh. 7,000 kila kimoja, alisema hayana ukweli.

Alisema serikali ilipeleka vyandarua hivyo, lakini wakaelekezwa na Magereza Makao Makuu visitumiwe, badala yake vipelekwe kwenye zahanati, kwani katika mabweni ya gereza magodoro hutandikwa chini, hivyo si rahisi vyandarua kufungwa.

Mallya alisema baadhi ya wafungwa walijaribu kufunga vyandarua hivyo dirishani, lakini wakazuiwa, kutokana na nyavu za madirisha kukatika.

“Kwa hiyo, vyandarua vyote viko stoo, vimefungiwa hakuna chandarua kilichouzwa,” alisema Mallya.

Alisema kwa sasa mabweni ya gereza yamepuliziwa dawa ya kuua mbu, hatua ambayo imemaliza tatizo la mbu, hivyo hakuna sababu tena ya kufunga vyandarua.
 
Chanzo: NIPASHE

No comments:

Post a Comment