Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, September 9, 2012

Nagu `amchezea rafu` Sumaye

Uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) si lelemama, sasa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Mary Nagu, anatajwa `kucheza rafu’ kumdhibiti bosi wake wa zamani, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Jina la Nagu, linadaiwa kupenyezwa baada ya Katibu wa chama hicho wilaya ya Hanang’ kubadilisha muhtasari wa kikao cha kamati ya siasa ya wilaya.
Kufanikiwa kwa njama hizo kunatajwa kuwepo ‘mkono’ wa Nagu aliyekuwa mshirika wa karibu wa Sumaye kwenye kura za maoni, kuwania urais kupitia CCM mwaka 2005.
Taarifa kutoka ndani ya ofisi ya Katibu wa CCM wilaya ya Hanang’, zinadai kuwa Kiongozi huyo, Allan Kingazi, alibadilisha muhtasari wa kikao kilichomuengua Nagu kuwania nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM.
Kwa mujibu wa marekebisho ya Katiba ya CCM, wajumbe wa Nec wanachaguliwa katika ngazi za wilaya, tofauti na mkoa ilivyokuwa awali.
Nagu alienguliwa kuwania nafasi hiyo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutokidhi kanuni za chama hicho.
Uamuzi huo ulihusisha kanuni zinazokataa wajumbe wa nafasi hiyo, wasiwe wenye majukumu mengi ya kikazi kama ilivyo kwa Nagu ambaye ni Mbunge na Waziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Wakati jina la Nagu likielezwa kurejeshwa kinyemela ili likajadiliwe kwenye ngazi ya mkoa, taarifa zinazidi kuainisha kuhusu matumizi makubwa ya rushwa, yaliyofanikisha mpango huo.
“Kiongozi wetu amepewa hongo ya Shilingi milioni mbili, kati ya hizo milioni moja na nusu azipeleke kwa (XXXXXX) anamtaja kiongozi wa ngazi ya mkoa) na Shilingi 500,000 abaki nazo,” kilieleza chanzo chetu kutoka ndani ya CCM.
Lengo la fedha hizo zinazopingwa kwa matumizi ya kufanikisha kuchaguliwa ndani ya CCM, linatajwa kushawishi yafanyike mabadiliko ya muhtasari na kukubaliwa katika ngazi ya mkoa, ili kufikia tarajio kusudiwa.
CCM wilaya ya Hanang’ ilipokea na kujadili majina ya wagombea watano waliojitokeza kuwania ujumbe wa Nec, ambapo majina ya Sumaye na Leonsi Marmo yalipitishwa baada ya kukidhi vigezo.
Nagu alienguliwa licha ya wajumbe watano kati ya 12 waliohudhuria kikao hicho, kujipambanua kuwa watetezi wake, wakitaka jina la Waziri huyo liwasilishwe mkoani.
Taarifa zaidi zilidai kuwa Kijazi, alionekana kumtetea Nagu ili apitishwe kwa madai kuwa, amepata agizo (barua) kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama.
Agizo hilo linaelezwa kutaka wilaya ya Hanang’ ilipitishe jina la Nagu kwa madai kuwa anaandaliwa kwa ajili ya kugombea urais mwaka 2015.
Hata hivyo, ilidaiwa wajumbe saba kati ya 12 walibaki na msimamo wa kutaka kanuni za CCM zifuatwe na Nagu aenguliwe katika kuwania nafasi hiyo.
Kura zilipigwa kufikia uamuzi huo, ndipo Nagu akapata tano wakati 12 zilitaka aenguliwe.
Mwandishi wa habari hizi alipowasiliana naye kwa njia ya simu, Kingazi alikanusha na kusema taarifa za kamati ya siasa ni siri na kwamba mtu anayezitoa hatambuliwi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za CCM.
Aidha, alisema taarifa za waliopitishwa kugombea nafasi ya Nec zitatolewa baada ya kamati ya siasa ya mkoa kupitia majina yaliyopendekezwa.
“Kwa hali hiyo taarifa zinazotolewa sasa sio sahihi,” alisema Katibu huyo wa CCM wa wilaya ya Hanang’.
Naye Katibu wa CCM mkoani Manyara, Nden’gaso Ndekubali, alipowasiliana na Mwandishi wa habari hizi, hakukataa wala kukubali kuhusika na hatua yoyote ya kufanikisha njama hizo.
Hata alipoulizwa ikiwa anahusika kwa namna yoyote na tuhuma za rushwa inayodaiwa kuwasilishwa CCM mkoa wa Manyara, kushawishi kulikubali na kulijadili jina la Nagu, alimgeuzia kibao (Mwandishi) na kumhoji “wewe umehongwa ili uandike habari hiyo?”
Naye Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Wilson Mukama, alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kujibu madai ya wajumbe kuwa, alitaka wajumbe hao kupitisha jina la Nagu kwa kuwa anaandaliwa kugombea Urais, alijibu kwa kifupi “ sihusiki na lolote linalotokea au kuendelea kutokea Hanang’.
Sumaye alipowasiliana na NIPASHE Jumapili jana, alisema hana taarifa zozote kuhusu majina hayo, kwa madai kuwa taarifa za kikao zinakuwa siri.
“Hata mimi ninazisoma sana taarifa hizo kwenye magazeti, lakini sina uhakika kwa maana ninasubiri uamuzi wa vikao husika,” alisema.
Nagu alipotafutwa kujibu madai hayo simu yake ilionyesha kuwa inatumika kwa muda mrefu.
Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu hadi tulipokuwa tunakwenda mitamboni

No comments:

Post a Comment