Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Sunday, September 9, 2012

Nchi imeingia katika laana-Maaskofu

Askofu Dk. Valentino Mokiwa
Maaskofu wawili wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa na Dk. Basil Sambano katika nyakati tofauti, wamelaani mauaji ya raia yanayofanywa na Jeshi la Polisi huku wakisisitiza kuwa utafikia wakati raia hawatakubali na kuanza kutumia silaha kujihami na polisi.
Katika mahojiano maalum na gazeti la NIPASHE JUMAPILI, Maaskofu hao wameelezwa kwamba hatua hiyo ikishafikia, Tanzania hapatakuwa mahali pazuri tena pa kuishi kama ilivyozoeleka kuwa ni kisiwa cha amani.
Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk. Valentino Mokiwa, alisema katika mauaji hayo, polisi hawakuwa na sababu ya kutumia nguvu kubwa kwani alisema risasi za moto ni hatua ya mwisho kabisa kutumiwa na majeshi yanayolinda usalama wa raia na mali zao.
Kwa mujibu wa Askofu Dk. Mokiwa, risasi hizo zimetumika mahali ambapo hapakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
"Unajua itafikia wakati raia watafanya maandamano au kwenda kwenye mikutano yao ya hadhara wakijihami na silaha zao, maana wanazo na polisi wanapojaribu kuwaonyesha mtutu nao watajibu, sasa hebu tuangalia katika mazingira hayo hali itakuwaje?" Alihoji.
Dk. Mokiwa alisema polisi wanajenga usugu kwa raia, hivyo wasijekushangaa silaha wanazowamilikisha raia hao zikawageukiwa wao.
Alimpongeza Mkuu wa Jehsi la Polisi kwa kubuni zana ya ulinzi shirikishi aliosema kuwa ni utaratibu mzuri ambao ulionyesha mafanikio mazuri kutokana na baadhi ya matukio makubwa yanayohatarisha usalama wa raia kupungua.
"Hii zana ilikuwa ni nzuri sana, lakini utaratibu huo unahujumiwa na baadhi ya polisi hasa wadogo..." alisema.
Hivi karibuni, polisi wameendeleza kampeni zao za kuua raia waliokuwa kwenye shughuli za kisiasa.
Miongoni mwa mauaji hayo ni yale yaliyotokea eneo la Msamvu mkoani Morogoro Agosti 27, ambako msoma magazeti aliyetambulika kwa jina la Ally Zona aliuawa kwa kupigwa risasi kichwani.
Tukio jingine ni lile lililotokea Septemba 2, mwaka huu mkoani Iringa ambako mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kupigwa bomu la machozi lililosababisha mwili wake kusambaratika, na matukio mengine yaliyotokea mkoani Singida na Arusha.
Matukio hayo yalilaaniwa na mtu mmoja mmoja, vikundi, vyama vya siasa, vyama vya kijamii na vituo vya kisheria nchini huku wakisisitiza viongozi wa jeshi hilo na Waziri wa Mambo ya Ndani wajiuzulu.
NCHI IMEKOSA MAADILI, ISHARA YA LAANA
Naye Askofu mstaafu wa kanisa la Kianglikana Jimbo la Dar es Salaam na Pwani , Dk. Basil Sambano, amesema matukio ya vurugu yanayosababisha watu wasio na hatia kupoteza maisha ni ishara kuwa nchi imeingia kwenye laana kutokana na kupungua maadili na kutaka wananchi kumuomba Mungu aweze kurudisha baraka zake.
Akizungumza na NIPASHE JUMAPILI jana, Askofu Sambano alisema laana hiyo katika nchi imesababishwa na ukiukwaji wa maadili kwa wananchi wake hususani vijana pamoja na kutopewa kipaumbele somo la uraia.
“Tunatakiwa tutubu ili kuepukana na laana hii, kwani nchi imeingia mahali pabaya na tuombe Mungu aweze kuturudishia baraka zake…polisi wanaua watu ovyo, watu wanaandamana, wafanyakazi wanagoma, tutubu kwanza,” alisema Askofu Sambano.
Sambano alisema matatizo hayo ya ukiukwaji wa maadili na kusababisha nchi kuingia ‘upotevuni’ kunatokana na kutotiliwa mkazo masomo ya uraia ambayo watu wanatakiwa kutafsiriwa maana ya uraia ni kitu gani.
Akizungumzia matatizo yanayotokea nchini hivi sasa, Akosfu Sambano alisema miaka ya hivi karibuni kumeibuka na migomo ya mara kwa mara hususani kwa walimu na madaktari, huku wakisahau kazi hizo ni wito.
“Kweli kazi hizi mbili pamoja na ile ya polisi na jeshi, ni kazi za wito kwani lengo kubwa ni kuweza kuitumikia jamii…sasa wanapogoma wanawafundisha nini watoto wetu,” alihoji Sambano.
Aidha, alisema ili kuepukana na laana inayoikabili nchi hivi sasa, inatakiwa watanzania wote kuliombea taifa hili ili liweze kurejea katika mstari mzuri wa kuweza kuitii serikali ambayo ndio mzazi wa kila mtu nchini mwake.
Kiongozi huyo wa kidini alisisitiza, ili nchi iweze kusimamia rasilimali zake vizuri, ni lazima kumuomba Mungu na kutubu mbele zake ili wakubwa waheshimiwe na wadogo na vile vile wapate kuheshimiwa.
“Naamini ili kuweza kuepukana na laana hii inayoonekana kuitafuna nchi hivi sasa, lazima tukazanie ufundishaji wa somo la raia kwa watoto wetu mashuleni, kwani somo bora linalojenga maadili mazuri kuliko hata hesabu na jiografia,” alisema.
Askofu Sambano aliongeza kuwa vijana wengi wanakosa maadili kama vile hakuna serikali, hivyo kusababisha kukosekana kwa upendo, heshima na huruma ambavyo ndivyo vitu asili vya mwafrika.
“Waafrika wanafahamika kwa mambo hayo matatu, lakini huruma ndilo jambo kuu ambalo tunatakiwa kujivunia…kwa kweli huruma hiyo kwa sasa hatuna kabisa kwani watu wanauliwa kama mzaha huku migomo isiyo na tija ikiendelea kila sehemu,” alisema.
Naye Askofu wa Kanisa katoliki wa Jimbo la Ifakara, Salutaris Lubena amesema Taifa linakabiliwa na changamoto ya baadhi ya vijana kukosa maadili mema kutokana na kushindwa kupata malezi bora toka kwa wazazi wao.
Alisema kama wazazi hawatachukua hatua za haraka kusimama imara kutoa malezi yanayosimamia maadili mema, ukweli na upendo, kuna hatari nchi ikaendelea kuwa na watu wenye tabia ya ubinafsi na ukiukaji wa maadili.
Askofu Lubena alisema hayo Mjini Kibaha jana wakati akiwatunukia vyeti vya kumaliza elimu ya darasa la saba wanafunzi wa Shule ya Msingi St. John Bosco.
"Baadhi ya wazazi wamejisahau katika utoaji wa malezi bora, matokeo yake tunashuhudia jinsi Taifa linavyokabiliwa na changamoto ya vijana wengi kuingia katika vetendo viovu ambavyo vipo kinyume na maadili yetu," alisema Askofu Lubena.
Alisema kuanzia sasa wazazi waanze kuwajengea msingi mzuri watoto wao kwa kuwapa elimu bora pamoja na kuwasimamia kwa kila jambo ili kuwafanya waweze kumudu changamoto za maisha mara watakapoanza maisha yao.
Alipongeza uongozi wa Shule ya St. John Bosco kwa hatua yao ya kutoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu kupitia shule hiyo, ambapo watoto wanaotoka hapo wanafanya vizuri katika ngazi ya kimkoa na Taifa.
Aidha, Mkurugenzi wa Shule hiyo Father Benno Kikudo alisema mwaka huu jumla ya wanafunzi 31 watafanya mtihani wa darasa la saba ambapo wamewandaa kikamilifu kukabiliana na mitihani ya Taifa.

No comments:

Post a Comment