Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisisitiza jambo wakati akiongea na Waziri wa
Ujenzi Dkt.John Pombe Magufuli wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ujenzi wa
Daraja la Kigamboni uliofanyika huko Kurasini jijini Dar es Salaam leo
mchana.Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadik.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo,
Alhamisi, Septemba 20, 2012, ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Daraja
la Kigamboni, Dar es Salaam kwa kuwaonya watu ambao amewaeleza kuwa
wanavyo viwanda vya kutunga uongo kuacha tabia hiyo na kuelekeza nguvu
kwenye maendeleo.
Aidha, Rais
Kikwete amewahakikishia wakazi wote wa Kigamboni ambao wanaondolewa
katika maeneo yao kwa ajili ya kupisha ujenzi wa daraja hilo na ujenzi
wa Mji Mpya wa Kigamboni kuwa watalipwa stahili na haki zao zote.
Daraja hilo
la Kigamboni ambalo wazo la kujengwa kwake lilibuniwa kwa mara ya
kwanza zaidi ya miaka 30, tokea mwaka 1978, wakati wa uongozi wa Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, linajengwa kwa gharama ya Sh. bilioni
214.6 na litakuwa tayari katika muda wa miezi 36 ijayo, ingawa muda huo
unaweza kupungua na kubakia miezi 30.
Daraja hilo
ambalo litakuwa na urefu wa mita 680 linagharimiwa kwa pamoja na
Serikali na Shirika la Hifadhi ya Jamii la NSSF ambalo litachangia kiasi
cha asilimia 60 na Serikali asilimia 40.
Daraja hilo
ambalo litakuwa na jumla ya barabara za kupitisha magari sita kwa
wakati mmoja linajengwa na makampuni mawili ya China ambayo ni China
Railway Construction Engineering Group na China Railway Major Bridge
Engineering Company na mhandisi msimamizi wa ujenzi huo ni Kampuni ya
Misri.
Daraja hilo
litapunguza adha ya usafiri kati ya Kigamboni na Dar es Salaam ambao
kwa sasa unategemea vivuko, ama boti ndogo, mitumbwi ama wenye magari
kulazimika kufanya mzungumo wa kilomita 52. Kwa uamuzi wa sasa, wavuka
kwa miguu ambao watakuwa na njia maalum kwenye daraja hilo pamoja na
waendesha baiskeli watavuka bure bila malipo yoyote.
Akizungumza
kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali haiwezi
kudhulumu wananchi wake na hivyo watu wote ambao wanastahili fidia
kutokana na ujenzi wa daraja hilo na mji mpya wa Kigamboni watalipwa
haki na stahiki zao.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa Serikali yake haitaruhusu mtu yoyote kuzuia ama
kuchelewesha miradi ya maendeleo ambayo inalenga kunufaisha watu wengi.
Rais Kikwete pia amewaonya watu ambao wamelifanya suala la kutunga na kusema uongo kama sehemu ya utamaduni wao. “Watu
wana viwanda vya kuzalisha uongo. Wanashinda wanasambaza uongo kwenye
mitandao, kila mahali. Wamepata hata kusema kuwa mimi nimemuuzia George
Bush eneo la Kigamboni. Bush aje kufanya nini Kigamboni?”
Rais pia amesema kuwa wapo watu ambao hawapendi maendeleo ya nchi. “Wanatamani
kila siku tushindwe kuwaletea wananchi maendeleo. Lakini watakufa kwa
kihoro kwa sababu hatutashindwa. Kila tulilosema tutalifanya,
litafanyika”.
Amesema kuwa thamani kubwa ya vyama vya siasa ni maendeleo ya wananchi. “Lakini
wapo wenzetu ambao wanaudhika wakiona maendeleo. Wanapenda hata daraja
hili lisijengwe. Leo hawatalala usingizi. Kazi ya vyama vya siasa ni
kuweka maslahi yetu sote mbele.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
20 Septemba, 2012
|
No comments:
Post a Comment