Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, October 17, 2012

AUWAWA KATIKA UGOMVI WA WAMASAI NA WAARUSHA...!

MTU mmoja ameuawa kwa kukatwa na mapanga na ng'ombe 11 kuibwa katika mfululizo wa matukio ya mapigano ya kuviziana baina ya wafugaji wa kabila la Wamasai na Waarusha.

Tukio hilo lililothibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Millya lilitokea juzi, baada ya wafugaji wa jamii wa Kimasai kumvamia kijana wa jamii ya Kiarusha,  Seuri Meibuko (16), akiwa machungani na kumkatakata kwa mapanga hadi kufa na kuchukuwa mifugo.

Kaka wa marehemu, Joshua Kivuyo akizungumza na Mwananchi jana, alisema mdogo wake aliuawa akiwa machungani eneo la Engikareti baada ya kuvamiwa na wamasai.

"Tukio hili ni mfululizo wa matukio ya vita   vinavyoendelea baina ya wamasai na Waarusha, kwani kama ni  wizi tu, ilikuwa haina sababu ya kumuua huyu kijana mdogo ambaye alikuwa peke yake machungani," alisema Kivuyo.

Kivuyo aliiomba Serikali kuendeleza vikao vya usuluhishi kwani bado si shwari baina ya makabila hayo, ambayo awali yalikuwa na undugu.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Longido, James Millya licha ya kukiri kupata taarifa za tukio hilo, alisema inawezekana lilikawa ni tukio la ujambazi wa mifugo.

"Ingawa ni kweli bado mahusiano baina ya wamasai na Waarusha hayajawa mazuri lakini tukio hili inaweza ikawa ni wizi wa mifugo tu," alisema Millya.

Hata hivyo, alisema anaamini bado uchunguzi wa kina wa tukio hilo unafanywa ili kubaini wahusika  na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

Akizungumzia  hatua ambazo zimefikiwa na ofisi yake katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa makabila hayo, alisema vikao vya viongozi wa mila Laigwanani kwa upande wa Longido na Monduli vimefanyika ili kuwaomba wazee kuwazuia vijana kupambana tena.

"kwa takriban wiki mbili tulikuwa na vikao katika maeneo haya ya wamasai na kwa kiasi kikubwa wametuelewa kuwa tunataka amani na migogoro yao ya mipaka inafanyiwa kazi," alisema Millya.

Wasusia kushirikiana katika minada

Katika hatua nyingine, wafugaji wa jamii ya Kimasai wamesusia kushiriki katika midana katika maeneo ya Waarusha na Waarusha wamesusia kushiriki katika minada ya wamasai, ili kukwepa mapigano zaidi.

Baadhi ya wafugaji, Julias Ole Mollel  na Elias Nanyaro, walisema sasa wamasai wamesusia kwenda katika mnada wa Odonyosambu na Ngaramtoni huku pia Waarusha wakisusia minada  ya Namanga na Longido.

"Juzi mnada wa Oldonyosambu hakuwa na masai kabisa kwani wameanzisha mnada wao Engikareti sasa hii ni hatari tunaomba serikali kuingilia kati kurejesha amani," alisema Nanyaro.

Wakati huo huo, Serikali imeombwa  kupeleka msuluhishi wa migogoro ya ardhi haraka wilayani Ngorongoro, ili kutuliza ugomvi wa mipaka baina ya wamasai wa jamii ya Loita na Wasonjo (batemi) ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu 15 na mifugo zaidi ya 2500 kuporwa.

Wakitoa tamko kwa waandishi wa habari jana mjini hapa, Madiwani wa kata zenye migogoro, wilayani humo,wakiwa na wenyeviti wa vijiji,walisema kama serikali isipochukuwa hatua mapema maafa makubwa yanaweza kutokea.

Madiwani na wenyeviti hao, katika tamko lao walilosaini wote, walisema kati ya mwaka 2007 na 2012 watu 15 wameua na wakataja majina yao na ng'ombe 2647 na mbuzi 685 wameporwa.

No comments:

Post a Comment