Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo |
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei kikomo mpya, ambazo zitaanza kutumika leo nchini kote zikiwa zimeshuka kwa Sh. 306 kwa lita ya petroli, Sh. 192 kwa lita moja ya dizeli, huku mafuta ya taa bei zikibaki bila kubadilika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, bei za mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam zitakuwa Sh. 1,994 kwa lita moja ikiwa imeshuka kutoka Sh. 2, 300 ya bei ya Septemba, huku mafuta ya dizeli bei yake ikishuka hadi kufikia Sh. 1,950 kutoka Sh. 2,142, wakati mafuta ya taa yakibaki Sh. 1,993 kutokana na kutoingia meli yoyote ya mafuta hayo.
Taarifa hiyo ilisema bei hizo zitaendelea kuongezeka kutokana na gharama za usafirishaji kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani, ingawa kwa jumla katika kila eneo punguzo litakuwa ni Sh. 306 na Sh. 192 kwa petroli na dizeli kwa lita moja.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, Kaguo alisema bei za bidhaa za mafuta ya petroli, zitaendelea kupangwa na soko na Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
“Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta kulingana na bei anayoiona mteja inamfaa,” ilieleza taarifa hiyo na kuongeza:
“Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo. Na kama mfanyabiashara atakiuka atapewa adhabu ya kulipa Sh. milioni tatu.”
Taarifa hiyo ilivitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana ili kumfanya mteja afanye uchaguzi wa kununua mafuta akiwa anajua bei halisi ya mafuta katika kituo husika.
No comments:
Post a Comment