Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa |
Serikali kupitia Wizara ya Fedha imepewa mkopo wa Sh. bilioni 280, ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Dar es Salaam na maeneo ya Chalinze, mkoani Pwani.
Akisaini mkopo huo jana jijini Dar es Salaam na Meneja Mkuu wa Benki ya Exim ya India, Geeta Poojary, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alisema mkopo huo umekuja kwa wakati ili kusaidia Tanzania kukabiliana na tatizo hilo kwa kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa maeneo husika.
“Badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji, ni vyema wakazi wa maeneo hayo kupitia mkopo huu kujiongezea kipato na kukabiliana na umaskini,” alisema.
Aidha, Dk. Mgimwa alisema mradi huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa maji kutoka mita za ujazo milioni 82 hadi milioni 196 kwa siku.
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa njia ya usafirishaji wa maji na kuongeza mtandao wa usambazaji kwa mteja,” alisema Waziri huyo na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo itakuwa ni sehemu ya kutekeleza mkakati wa kukuza Uchumi na Kupunguza Umasilini (Mkukuta) na kupunguza magomjwa yanayotokana na maji yasiyokuwa salama.
Alisema mkopo huo ni moja ya mikopo nafuu sana kwani Tanzania itatakiwa kulipa riba ya asilimia 1.7.
No comments:
Post a Comment