Arusha, Oktoba 13,2012 (EANA) – Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wa Burundi, Leontine Nzeyimana amezipongeza juhudi zinavyofanywa za kuanzisha kumbukumbu za picha zinazoonyesha jinsi jumuiya hiyo inavyojiimarisha zaidi katika nyanja za kiuchumi na kisiasa katika nchi zake tano wanachama.
‘’Kumbukumbu za picha ni muhimu katika kuonyesha mshikamano mkubwa uliopo miongoni mwa nchi za EAC,’’ alisema waziri huyo.
Waziri huyo alisema hayo wakati wa mapokezi ya ujumbe wa pamoja wa wapiga picha wa EAC na Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la Ujerumani (GIZ) mjini Bujumbura, Burundi, Juzi. Timu hiyo imeshatembelea nchi za Kenya, Tanzania Bara na Visiwani pamoja na Rwanda. Nchi ya mwisho kutembelewa katika ziara hiyo ni Uganda.
Amezipongeza juhudi za EAC-GIZ akisisitiza kwamba hatua hiyo ni muhimu na imekuja kwa wakati mwafaka. Alisema, hivi sasa, kanda hiyo inakosa picha zenye ubora wa hali ya juu zinazohusiana na juhudi za kuimarisha mtangamano katika kanda, hususan ni zile zinazoonyesha hali halisi ya ushitrikiano huo katika nyanja za watu wa kanda hii kutembeleana na usafirishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa raia wake.
‘’Picha huzungumza maneno elfu moja. Wale wanaokuwa na wasiwasi na mtangamano huo wanaweza kuamini kwa vitendo kwamba mtangamano upo unafanayakazi na unaendelea kuimarika,’’ alisema na kuongeza kuwa upigaji wa picha chanya juu ya mtangamani utawezesha pia kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza Afrika Mashariki.
Timu hiyo ya watu wanne pia inajumuisha Mkuu wa mafunzo wa EAC-GIZ na Mtaalamu wa Picha Hermut Fiebebig.
Ziara hiyo inafuatia mafunzo ya kwanza ya wapiga picha kutoka nchi wananchama wa EAC yaliyofanyika mjini Arusha, Tanzania, katikati ya mwaka huu. Lengo la ziara hiyo ni kupiga picha za kumbukumbu muhimu katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi wananchama kwa ajili ya kuzihifadhi kwa matumizi mbalimbali ndani na nje ya EAC.
DB/NI
Na Dennis Bizimana, EANA
No comments:
Post a Comment