Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, October 9, 2012

Chadema yaibana Polisi kutoroka kwa watuhumiwa wa mauaji

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelitaka Jeshi la Polisi kutoa maelezo ya kutosha yatakayoendana na uwajibikaji na hatua za kisheria, kufuatia watuhumiwa wawili wa mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, kutoroka mbele ya askari wenye silaha.

Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, alisema chama hicho kimepokea kwa mshtuko kitendo cha watuhumiwa hao kutoroka mbele ya askari wenye silaha, baada ya kumnyang’anya bunduki mmoja wa askari waliokuwa lindo eneo la mahakama ya wilaya.

Alisema Chadema inasikitika kwa kitendo cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, kugoma kutaja jina la askari aliyenyang’anywa bunduki na hata majina ya wenzake waliokuwa lindo mahakamani.

Alisema kutokana na tukio hilo lenye utata, kuna umuhimu wa kuundwa kwa chombo huru cha uchunguzi wa mauaji yenye utata, yanayohusishwa na siasa, mojawapo likiwa ni tukio la mauaji ya Mbwambo.

Lwakatare alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katika barua aliyomwandikia Rais, alimtaka kuunda Tume ya Kijaji/ Kimahakama ya uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa yaliyohusisha Chadema.

“Ni bahati mbaya kuwa wakati Watanzania wapenda haki wakisubiri kujua majibu ya Rais kwa barua hiyo, masuala kadhaa yametokea, ambayo yote yameonesha kuwa serikali ya CCM inazidi kukomaza mfumo wa kulindana na kutaka kuficha masuala fulani fulani, hasa katika matendo ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi,”alisema Lwakatare.

No comments:

Post a Comment