Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, October 9, 2012

Mahakama ya Rufaa yatupilia mbali rufaa ya Aeshi

Mahakama  ya Rufani Tanzania imetupilia mbali rufaa aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Aeshi Hilaly, aliyevuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, baada ya maombi yake ya rufaa kuwa na upungufu wa kisheria.

Uamuzi huo ulisomwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Msajili, Zahra Mruma, baada ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Januari Msoffe, Jaji Edward Rutakangwa na Jaji Engela Kileo, kupitia maombi hayo na kubaini kwamba, maombi hayo ya rufaa yalikuwa na upungufu wa kisheria.


Aidha, wakati wote uamuzi huo ulipokuwa unasomwa na mahakama hiyo, Hilaly hakuwapo mahakamani hapo. Aliyekuwapo ni mgombea wa kiti hicho kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Nobert Yamsebo.


Yamsebo alisema anamshukuru Mungu mahakama inaendelea kuona ni jinsi gani ubunge wa Hilaly haukuwa halali na kwamba, imefanya kazi yake kama sheria inavyotaka.


Septemba 19, mwaka huu jopo hilo la majaji watatu liliketi na kubaini upungufu wa kisheria kabla ya kuanza kusikiliza rufaa hiyo iliyofunguliwa na Hilaly dhidi ya Yamsebo.


Miongoni mwa upungufu huo, mahakama ilibaini kuwa katika mwenendo wa kesi uliowasilishwa mahakamani hapo, haukuwapo mwenendo wa uamuzi, maombi ya kupunguziwa gharama za kufungua kesi hiyo zinazowekwa mahakamani kama amana, yaliyowasilishwa na aliyekuwa mlalamikaji katika kesi ya msingi, kuomba apunguziwe gharama hizo.


Katika kesi hiyo namba 01 ya mwaka 2010, Yamsebo alikuwa akipinga ushindi wa Hilaly, akidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi na hivyo kusababisha uchaguzi huo kutofanyika kwa haki na huru.


Aprili 30, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga ilimvua ubunge Hillary, baada ya kuona ushahidi uliotolewa na upande wa mlalamikaji Yamsebo kuthibitisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka 2010 haukuwa wa haki na kulikuwa ukiukwaji wa sheria.

No comments:

Post a Comment