Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 11, 2012

Dawa za ARVs zamng’oa bosi MSD

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi

Serikali imewasimamisha kazi vigogo watatu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Joseph Mgaya, kwa tuhuma za uzembe uliosababisha kununua Dawa bandia za Kupunguza Makali ya ugonjwa wa Ukimwi (ARV’s) zilizotengenezwa na Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPI).

Wengine waliosimamishwa kazi kwa tuhuma hizo, ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora na Ofisa Udhibiti Ubora wa Bohari hiyo.

Taarifa za kusimamishwa kazi kwa vigogo hao wa MSD, zilitangazwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu, wizara kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilibaini kuwapo kwa ARV’s aina ya TT-VIR 30, toleo namba OC.01.85 katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.

Dk. Mwinyi alisema baada ya kubaini hilo, TFDA ilifanya ukaguzi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika mkoa huo.

Alisema baadaye ilifanya ukaguzi katika mikoa mingine nchini kote kwa kushirikiana na vyombo vya usalama.

Waziri huyo alisema ukaguzi huo ulihusisha MSD makao makuu, kanda na TPI na kuchukuliwa sampuli za dawa husika kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara na iligundulika kuwa ni bandia.

Alisema matokeo ya ukaguzi huo, yalibaini kuwa toleo namba 0C.01.85 lilikuwa na dawa zenye rangi mbili; njano na nyeupe.

Dk. Mwinyi alisema vidonge hivyo vilikutwa kwenye vifungashio vya dawa husika, vilikuwa tofauti na vifungashio vya dawa vilivyosajiliwa na TFDA.

“Tumeona tuchukue hatua kutokana na uzembe wa watendaji wa MSD. Lakini pia kusitisha uzalishaji wa TPI  pamoja na usambazaji wa dawa zote zilizokwisha kutengenezwa na kiwanda hicho hadi uchunguzi utakapokamilika,” alisema Dk. Mwinyi.

Alisema tayari makopo 9,570 ya dawa hiyo, yamekamatwa na kuondolewa kutoka katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya na kurudishwa MSD.

Aidha, alisema wizara inaendelea kuimarisha mfumo na taratibu za kuhakiki ubora, utunzaji usambaji na matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea dawa nchini kote.

Dk. Mwinyi aliitaka jamii kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwapo kwa ubora wa dawa zenye shaka au uvunjifu wa sheria.

Sakata la kuwako kwa dawa bandia zilianza kuripotiwa nchini hivi karibuni baada ya watumiaji wa dawa hizi kulalamika na taarifa kurushwa na vyombo vya habari.

No comments:

Post a Comment