KAMATI
iliyokuwa ikichunguza vurugu zilizotokea mkoani Iringa na kusababisha
kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa Kituo Cha Televisheni cha Channel Ten,
David Mwangosi imekabidhi ripoti yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Dk
Emaanuel Nchimbi.
Katika vurugu hizo ambazo zilizotokea Kijiji cha Nyololo wilayani
Mufindi Septemba 2 mwaka huu, kati ya Polisi na wafuasi wa Chadema
waliokuwa wakifungua tawi la Chama hicho baadhi ya watu walijeruhiwa
akiwemo askari wa jeshi hilo.
Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara hiyo Isaac Nantanga
ilisema kamati hiyo imekamilisha kazi iliyopewa na hivyo kusubibili
kikao cha kamati hiyo na waziri wiki ijayo.
“Waziri ameishukuru kamati hiyo kwa kazi walioifanya na Jumanne (kesho
kutwa) atafanya kikao na waandishi wa habari” alisema Nantanga.
Wakati akiitangaza kamati hiyo Dk Nchimbi aliitaka kujibu maswali sita ambayo yalikuwa hanaya majibu kutokana na tukio hilo.
“Tuna maswali sita ambayo mimi sina majibu yake. Swali la kwanza
tunataka kujua nini chanzo cha kifo cha Daudi? Pili tujue ni kweli
kwamba kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa?” alisema Dk
Nchimbi
Aliongeza: “Tatu tujue kama ni kweli kuna orodha ya waandishi watatu wa
kushughulikiwa Iringa? Nne kama nguvu zilizotumika zilistahili? Tano
kama kuna utaratibu wa vyama vya siasa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa
polisi? Mwisho kujua uhusiano wa Jeshi la Polisi na vyama vya siasa
ukoje?”
Dk Nchimbi alisema, sheria lazima zifuatwe kwani nchi ikiingia kwenye
matatizo, Serikali haitaweza kuwaeleza wananchi kwamba ndicho kitu
kinachotakiwa... “Hatutaki tuwe na vita vya wenyewe kwa wenyewe.”
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Theophil Makunga
alisema kamati yake ilifanya ziara katika mikoa ya Iringa na Dar es
Salaam na kufanya mahojiano na wadau mbalimbali.
Alisema wakati wa zoezi hilo walizingatia yale waliyoelezwa na Dk
Nchimbi ikiwa ni kufanya kazi kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.
“Alitutaka
kufanya kazi bila kuegemea upande mmoja wa Serikali ama chama na
tumejibu maswali yote yaliyokuwa katika habibu za rejea alizotupa bila
kuacha hata moja,” alisema Makunga.
Aliongeza licha ya kujibu habibu hizo za rejea pia tumetoa mapendekezo ambayo kama yatatekelezwa hakutatokea tukio kama hilo.
Alipotakiwa
kueleza kilichomo ndani ya ripoti hiyo alisema hawezi na kutaka
kusubiri Jumanne ambapo Waziri na Kamati nzima itazungumza na waandishi
wa habari.
Kamati hiyo ilikuwa watu watano ambayo ilikukuwa chini ya Mwenyekiti ,
Jaji mstaafu Steven Ihema, mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF), Theophil Makunga,
Wajumbe wengine walikuwa ni mwakilishi wa Baraza la Habari Tanzania
(MCT), Pili Mtambalike, mtaalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishina wa Polisi (DCP),
Isaya Mngulu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment