Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 18, 2012

Dk. Ulimboka aibuka, atoa ya moyoni

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, ameibuka na kusema yupo tayari kueleza yaliyompata ikiwa serikali itaunda chombo huru kwa ajili ya kuchunguza sakata hilo.

Kwa mara ya kwanza jana, Dk. Ulimboka alitoa tamko lilisosainiwa na wakili wake, Rugemeleza Albert Nshala na kusomwa na wakili Nyaronyo Kicheere, jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.

Dk. Ulimboka mwishoni mwa Juni, mwaka huu, alitekwa na watu wasiofahamika katika barabara ya Tunisia, wilayani Kinondoni na kupigwa, kung’olewa meno na kutupwa katika msitu wa Mabwepande, nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, jana waandishi wa habari walishikwa na butwaa baada ya kuona tamko hilo zito likisomwa na Wakili Kicheere badala ya Dk. Ulimboka mwenyewe kama watu wengi walivyotarajia.

Wakili Kicheere aliwaambia waandishi wa habari kwamba Dk. Ulimboka, alishindwa kufika mbele yao na kusoma tamko hilo kwa kuwa yupo nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Hata hivyo, Kicheere hakutaja nchi ambayo Dk. Ulimboka amekwenda kuchunguzwa afya wala siku aliyoondoka.

Katika tamko hilo, Dk. Ulimboka alisema yupo tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo huru na makini vitakavyoundwa na serikali ili aeleze ukweli wa kilichompata.

Katika tamko lake hilo, Dk. Ulimboka alisema ametafakari sana na kuona kwamba kama hatatoa tamko hilo, atakuwa hajawatendea haki Watanzania wenzake kwa kuwa walihusika katika kumuombea kwa Mwenyezi Mungu alipokuwa anaumwa.

Alisema kuwa mambo mengi yaliyoelezwa na vyombo vingi vya habari hasa magazeti, yalikuwa yana ukweli ndani yake likiwamo lile la MwanaHalisi lililofungiwa na Serikali Julai 30, mwaka huu.

Aliongeza kuwa kabla ya kutoa tamko hilo, alijiuliza maswali mengi ambayo yalikosa majibu na kati ya mambo aliyojiuliza, ni jukumu la nani atakayehakikisha haki inatendeka katika nchi ya Tanzania.

“Ni jukumu la asasi za kiraia ama mhusika mwenyewe, kuelezea kinagaubaga kilichompata na baada ya kukosa majibu nikaona ni vyema niwaeleze Watanzania hali halisi,” alisema.

Alieleza kuwa kabla ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika msitu wa Mabwepande, alikuwa na kikao na ofisa aliyetambulishwa kwake kwamba anatokea Ikulu.

Alimtaja mtu huyo kuwa ni Ramadhan Abeid Ighondu, ambaye  alitambulishwa kwake kama ofisa anayetoka Ikulu kwa kuwa alikuwa anakutana naye mara kwa mara kabla ya tukio hilo la kutekwa na kupigwa.

Sehemu ya tamko hilo lilisema Ighondu alitambulishwa kwake na kigogo mmoja ambaye hakumtaja jina akiwa na wenzake ambao ni madaktari.

Dk. Ulimboka alisema walijulishwa kwamba hoja na madai mbalimbali ya madaktari, yatakuwa yanachukuliwa na Ighondu na kuyapeleka serikalini kwa ajili ya kutafuta mwafaka wa kupandishiwa nyongeza za mishahara na madai mengine.

Alisema siku hiyo aliyotekwa, alipigiwa simu na Ighondu kupitia simu ya mkononi namba 0713 760473 na kwamba anamtambua Ighondu kwa sura.

Aliongeza kuwa katika mawasiliano hayo, yeye (Dk. Ulimboka), alikuwa akitumia simu namba 0713 731610 na kwamba anaamini ofisa huyo wa Ikulu yupo hai na yupo tayari na wenzake kutoa ushahidi.

Aidha, Dk. Ulimboka alisema kwa nyakati tofauti, ofisa huyo alitumwa kwake na kumtaka ampatie nyaraka mbalimbali vikiwamo vyeti vya elimu kwa ajili ya uthibitisho wa taaluma yake.

“Mimi Dk. Ulimboka nina haki ya kuishi kwa mujibu wa ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wenzangu wana haki ya kuulinda uhai wangu,” alisema. 

“Je; uhai na maisha yangu vina thamani ndogo kama ya mnyama anayekwenda machinjioni? Je, serikali itakubali lini kuunda tume huru kuchunguza tukio hili?,” Alihoji.

 Aliwataka madaktari kutovunjika moyo katika kudai haki zao za msingi na kwamba yupo pamoja nao katika harakati hizo.

Juni 26, mwaka huu, Dk. Ulimboka alitekwa, akapigwa, akang'olewa kucha kabla ya kuokotwa msitu wa Mabwepande na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) kwa matibabu.

Hata hivyo, baadaye alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Dk. Ulimboka alirejea nchini Agosti 12, mwaka huu. 

Tangu hapo, hajawahi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusiana na sakata zima la kutekwa kwake hadi alipotoa tamko hilo jana.

No comments:

Post a Comment