Aliyekuwa mbunge wajimbo la Arusha Mjini Godbless Lema akiwasalimu wanachama mara baada ya kutoka mahakamani |
Wakili wa Lema, Method Kimomogoro aliiambia mahakama kuwa iwapo madai ya wakili ya wajibu rufani, Alute Mughwai kwamba hati ya kukazia hukumu iliyomvua ubunge Lema, ni batili, basi mteja wake ni mbunge halali.
Kimomogoro alitoa madai hayo jana wakati akijibu pingamizi la awali lililotolewa na wakili Mughwai, aliyedai kwamba hati hiyo ina kasoro kubwa za kisheria ambazo inafanya rufani hiyo kuwa batili tangu mwanzo hadi mwisho wake.
Kutokana na hoja hiyo, Kimomogoro aliiomba Mahakama ya Rufani ifute mapingamizi yaliyotolewa na Mughwai.
Wakili Kimomogoro alitoa ombi hilo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Mkuu, Mohammed Othman Chande, ambaye anasaidiana na majaji Natalia Kimaro na Salum Massati.
Pia, aliomba wajibu rufani walipe gharama za kuendesha kesi. “Tunaomba mapingamizi hayo yatupiliwe mbali na walioleta wawajibike kulipa gharama na kama mtaona inafaa basi kila upande ubebe mzigo wake iwapo hoja yao itazingatiwa,” alidai Kimomogoro.
Rufani ya kesi hiyo iliyosikilizwa jana katika Mahakama Kuu Arusha, ilikuwa ikisikilizwa pingamizi la awali, lililowasilishwa na wakili wa wajibu rufani, kwa niaba ya wateja wake, Musa Mkanga, Agnes Mollel na Hapines Kivuyo, ilivuta umati mkubwa wa watu kutoka karibu kila kona za jiji la Arusha.
Mapema wakili Mughwai alitaka rufani hiyo ifutwe kwa kuwa hati ya kukazia hukumu ilikuwa ina kasoro mbalimbali. Pia alitaka waomba rufani walipe gharama ya kesi hiyo pamoja na gharama za mawakili kwani wameihangaikia sana kesi hiyo.
“Rufaa ambayo ipo mbele yenu ni batili kwa sababu imesimikwa kwa hati ya amri ya Mahakama Kuu ambayo ni batili, hiyo hati ni batili toka mwanzo hadi mwisho wake,” alidai.
Aliendelea kuiambia mahakama kuwa kukosekana kwa muhuri wa mahakama katika hati hiyo ni hitilafu kubwa hata kama hati yenyewe ina saini ya jaji aliyeiandika.
Alidai kuwa uwepo wa muhuri wa mahakama unaonyesha mamlaka na uhalali na nyaraka yenyewe na kwamba bila muhuri nyaraka hiyo ni karatasi ya bure.
Mughwai hakukubaliana na hoja ya waleta rufaa kwamba hawahusiki na kasoro hizo isipokuwa wanaohusika ni mahakama kwani wao walitakiwa kujiridhisha kwamba hati hiyo imekamilika.
Katika hoja nyingine ya pingamizi, Mughwai alidai kuwa hati hiyo haionyeshi tarehe iliyotolewa ingawa ipo tarehe iliyoandikwa.
Aliieleza kuwa utaratibu huo unakwenda kinyume cha Kanuni ya 9 ya Masjala ya Mahakama Kuu na kuongeza kuwa hati hiyo haikuandikwa kwa muundo unaotakiwa kwa mujibu wa kanuni na sheria.
Akijibu mapingamizi hayo, Kimomogoro alidai kuwa mazingira ya shauri hilo yalikuwa ya kipekee baada ya kutolewa hukumu Mahakama Kuu na kwamba jalada la kesi lilipelekwa Dar es Salaam, kwa hiyo hawakuwa na nafasi ya kuangalia hati hiyo.
Aliongeza kuwa wakili Mughwai katika pingamizi amekwepa au kuchenga kwa makusudi kuelezea kanuni mpya na uamuzi wa kesi zilizotolewa siku za hivi karibuni kwa kuzingatia kanuni hizo kuelezea haki za msingi.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Timon Vitalis, ambaye katika kesi hiyo anamwakilisha Mwanasheria Mkuu, lakini kama sehemu muhimu (necessary party) alimuunga mkono wakili Kimomogoro, kwa hoja kwamba hati ya kukazia hukumu inatolewa chini ya Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Madai (CPC) na siyo chini ya Kanuni ya Masjala ya Mahakama Kuu, hivyo alitaka kama kuna mgongano basi CPC ndiyo itumike.
“Hata ukisema hati ya kukazia hukumu ina kasoro, basi anayepaswa kulaumiwa ni mamlaka iliyotoa hati hiyo na siyo wakili wa waomba rufani, hivyo mahakama ina jukumu la kutoa hati iliyo sahihi,” alidai.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Jaji Mkuu Chande, aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe nyingine ambayo watapanga.
“Uamuzi utatolewa kwa tarehe ambayo mtaarifiwa,” alisema Jaji Chande.
Aprili 5, mwaka huu, Mahakama Kuu Tanzania Kanda Arusha, ilitengua matokeo ya ubunge yaliyompa ushindi Lema baada ya kuridhika kuwa alitumia lugha ya kashfa na udhalilishaji dhidi ya aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Dk. Batilda Burian.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila, baada ya kumtia hatiani Lema kwa makosa mawili kati ya manne aliyokuwa akikabiliwa nayo, huku akitupa mawili kwa kukosa ushahidi.
Jaji Rwakibarila alimvua ubunge Lema baada ya kuridhika na ushahidi kuwa alitumia maneno ya kashfa na ubaguzi wa jinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Burian.
Pia Jaji Rwakibarila katika hukumu yake hiyo, alimwamuru Lema kulipa gharama za kesi hiyo.
Hata hivyo, alimweleza kuwa ana haki ya kukata rufaa ikiwa ataona hakuridhika na hukumu hiyo.
No comments:
Post a Comment