Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, October 3, 2012

JANGA JINGINE TENA LA AJALI KWA TAIFA ...!

Watu 13 wamefariki dunia na wengine 50 wamejuhiwa vibaya, akiwamo Mbunge wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mbeya, Dk. Mary Mwanjelwa, baada ya jana kutokea ajali tatu tofauti mikoa ya Mbeya, Shinyanga na Tanga.

Katika ajali iliyotokea mkoani Mbeya, watu 10 walipoteza maisha na wengine 25 kujuruhiwa kati yao vibaya baada ya lori la mafuta kuyagonga magari matatu kwenye mteremko.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, akizungumza na NIPASHE kwa simu alisema maiti za watu waliokufa bado hazijatambuliwa na kwamba zimehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na Hospitali Teule ya Ifisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Alisema ajali hiyo ilitokea jana saa 7:00 mchana katika mteremko wa mlima Iwambi kuelekea mji mdogo wa Mbalizi katika Halmashauri ya Mbeya Vijijini.

Athumani alisema Dk. Mwanjelwa na majeruhi wengine wamelazwa katika Hospitali Teule ya Ifisi iliyopo nje kidogo na Jiji la Mbeya.

Taarifa zaidi ambazo gazeti hili ilizipata kutoka Mbeya zinaeleza kuwa lori hilo la mafuta lenye namba za usajili IT 9518 lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kufeli breki na kuyagonga magari hayo, lililipuka moto.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Steven Jonas, Mkazi wa Mbalizi, alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori hilo liliokuwa limebeba mafuta likielekea barabara ya Tunduma kufeli breki na kuanza kuteremka  kwa kasi kwenye mteremko huo.

Alisema wakati lori hilo linashuka kwa kasi, magari mengine yalikuwa yakipandisha mlima huo likiwamo gari dogo la abiria aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T587 AHT  pamoja na T671 ABM Toyota Hilax alilokuwa akitumia Dk. Mwanjelwa kukutana uso kwa uso na lori hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa mbunge huyo katika gari hilo alikuwa na katibu wake aliyetambuliwa kwa jina moja la Amina ambaye amefariki papo hapo pamoja na dereva wake gari lake, ambaye hajulikana aliko.

Katika ajali hiyo, gari la abiria mara baada ya kugongwa ilitumbukia kwenye korongo huku gari dogo ambalo lilikuwa likitumiwa na mbunge huyo nalo likiteketea kwa moto.

Mashukuda wanasema kuwa baada ya ajali hiyo, lori hilo lilianza kuwaka moto na kutumbukia mtoni ambako nako kulikwa na idadi kubwa ya watoto waliokuwa wakiogelea.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali Teule ya Ifisi, Rhoda Kasongwa, alisema majeruhi waliopokelewa katika ajali hiyo ni 10, akiwemo Dk. Mwanjelwa.

Alisema kati ya majeruhi hao, watatu walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu kutokana na kuunguzwa na mafuta. Kati ya hao, wawili ni  watembea kwa miguu na mwingine alikuwa akiendesha pikipiki kando ya barabara hiyo.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Dickson Nswila, ambaye alikuwa akienda kwenye mazoezi ya vitendo Tazara, jijini Mbeya na mfanyabiashara wa mitumba katika mji mdogo wa Mbalizi, Charles Mwakanyuma.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo, mtu wa tatu aliyefariki katika ajali hiyo ni Mariamu Said (31), mkazi wa mji mdogo wa Mbalizi.

Kasongwa alisema dereva huyo ambaye bado hajatambulika jina lake wala makazi, amepoteza fahamu na anaendelea kupatiwa matibabu akiwa chumba cha wagonjwa wa uangalizi maalum (ICU) hospitalini hapo ameumia vibaya maeneo ya kichwani na miguuni, hivyo jitihada zaidi zinafanyika ili kuokoa maisha yake.

Dk. Mwanjelwa akizungumza na NIPASHE kwa simu akiwa katika hospitali hiyo alikolazwa, alisema amepata maumivu makubwa mgongoni na kiunoni.

“Nimeumia mgongoni na kichwani, siwezi kuongea sana najisikia maumivu makali,” alisema.

Hata hivyo, alithibitisha kuwa ndani ya gari lake kulikuwa na watu wawili ambao ni dereva, na katibu wa ofisi yake.

Habari zaidi kutoka kwa mashuhuda wa ajali hiyo zinasema kuwa mbali na magari hayo, pia lori la mafuta lilogonga lori lingine lililokuwa limepakia shehena ya chokaa, lilikuwa katika mwendo kasi na kabla ya kuwagonga na kupinduka, pia liligonga gari namba T.438 BRT aina ya Land Rover, mali ya mchungaji Nduka wa Kanisa la Uinjilist Mbalizi.

Walisema dereva wa Land Rover alikimbizwa katika Hospitali ya Ifisi na aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kutibiwa na kuonekana hali yake ni nzuri, kwani alipata michubuko kidogo.

Waliongeza kuwa kabla ya kuligonga Land Rover, lori hilo lilikwepa basi lililokuwa limewabeba wafanyakazi wa hospitali ya Ifisi, ndipo liligonga gema lililopo pembeni ya barabara, kupaa hewani kisha kuingia kwenye karakana ya mafundi seremala, iliyopo eneo la Tarafani.

Wananchi hao walisema polisi walifika eneo la tukio mapema na kuwazuia wananchi wasiendelee kupakua shehena ya chokaa, ambayo walikuwa wakibeba mifuko na kutokomea nayo katika makazi yao.

Aidha, kabla ya polisi hawajafika eneo la tukio, baadhi ya watu wasiofahamika walifanikiwa kufungua tangi la mafuta la lori lililokuwa limebeba chokaa hilo kisha kutokomea nalo.

Miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika hospitali Teule za Ifisi iliyopo Wilaya ya Mbeya Vijijini na Rufaa Mbeya.

BASI LA RAS LAUA WATATU

Katika ajali ya pili iliyotokea wilayani Kahama mkoani Shinyanga, watu watatu wamefariki dunia papo hapo na wengine 24 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba, mkoani Kagera kugongana na lori la mizigo.

Ajali hiyo iliyotokea jana, ililihusisha basi la Kampuni ya RS Bus Express ambalo liligongana na lori la mizingo la Kampuni ya Dhaudho aina ya Faw lenye namba za usajili T 513 BNP katika Kata ya Ngongwa wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

Lori hilo lilikuwa likitokea Ushirombo Wilaya ya Bukombe mkoani Geita kwenda jijini Dar es Salaam majira ya saa 12:20 asubuhi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Emmanueli Andrew, alisema baadhi ya majeruhi wamevunjika miguu huku wanne wakiwa mahututi na kulazimika kuwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Edwin Stephano, Hamidu Yusuph ambaye alikuwa dereva wa lori la mizigo na Zuraia Tuli (50).

Dk. Andrew aliwataja majeruhi waliopelekwa katika Hospitali ya Bugando kuwa ni  Chabukana, raia wa Uganda; Makame Suleiman, Mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Fred Peter na Shafii Abdallah.

 Kwa mujibu wa mashuhuda, chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa lori la mizigo kujaribu kumkwepa mwendesha baiskeli na kusababisha lori kwenda upande ambao basi ilikuwapo kisha kugongana uso kwa uso.

Naye mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Johannes Ndyamukama, alisema kuwa kabla ya ajali hiyo kutokea, basi hilo likuwa lifukuzana na basi la kampuni ya Sumry.

Ndyamukama aliongeza kuwa baada ya kulipita Sumry walikutana na lori lingine ambalo lilikuwa limemkwepa mwendesha baiskeli huyo na kuingia katika upande wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo chake ni mwendo kasi wa basi hilo.

Kamanda Mangala alisema kuwa polisi wanaendelea kumhoji dereva wa basi hilo.
 DAR EXPRESS LATEKETEA KWA MOTO

Basi la abiria lijulikanalo kama Dar Express likiwa linawaka moto
 

Mkoani Tanga, abiria 48 waliokuwa wakisafiri kutoka Rombo mkoani Kilimanjaro kwenda jijini Dar es Salaam wamenusurika kufa, baada ya basi walilokuwa wakisafiria, mali ya Kampuni ya Dar Express kuteketea kwa moto.

Chanzo cha basi hilo kuwaka moto kinaelezwa kuwa ni hitilafu ya umeme iliyoanzia eneo la karibu na siti ya dereva kisha mizigo yote ya abiria ikateketea kwa moto.

Gari hilo yenye namba za usajili T369 ARH aina ya Scania liliteketea moto majira ya saa 5:30 asubuhi katika eneo la Segera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, alitihibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na John Mwakihaba (41), mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Kamanda Massawe alisema kuwa abiria mmoja aliyejulikana kwa jina la Jacqueline Kisanga (21) alijeruhiwa maeneo ya kichwani baada ya kuruka nje kutoka kwenye basi. Kisanga alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ya Magunga kwa matibabu.

“Huyu binti baada ya kuona moshi unachanganya kwenye basi aliamua kuruka ili kunusuru maisha yake, lakini inaonekana aliangukia kichwa na tulimfikisha katika Hospitali ya Magunga kwa ajili ya matibabu zaidi,” alisema Kamanda Massawe.

Hata hivyo, alisema kuwa mizigo yote ya abiria wa basi hilo iliteketea kwa moto na kwamba uchunguzi wa Polisi kuhusiana na ajali hiyo bado unaendelea na kuongeza kuwa thamani halisi ya mali zilizoteketea haijafahamika.

Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Dar; Mohab Dominick, Kahama na Lulu George, Handeni.

No comments:

Post a Comment