Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, October 25, 2012

MADIWANI WA CHADEMA WATWANGANA MOSHI...!

MADIWANI wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Manispaa ya Moshi, Kilimanjaro juzi walitwangana makonde huku kiini kikitajwa kuwa ni gari la Mstahiki Meya.

Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi katika moja ya kumbi za mikutano ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wakati madiwani hao wakiwa katika kikao cha ndani cha maandalizi ya mkutano wa baraza la madiwani. Hata hivyo, licha ya taarifa za tukio hilo kuzagaa haraka, wahusika wameifanya siri ili kulinda heshima ya chama hicho.

Inadaiwa kuwa kisa cha kupigana ni ubishi juu ya nani anastahili kupanda gari hilo la Meya na baada ya kurushiana maneno, madiwani hao walivaana na kuanza kupigana kabla ya kuamuliwa na wenzao. Habari zinadai kuwa madiwani watatu wamekuwa wakilitumia gari la Meya kila wanapolihitaji bila kikwazo jambo ambalo limekuwa likiwakera baadhi yao.

Mwenyekiti wa Madiwani wa CCM katika Baraza hilo, Michael Mwita amekiri kuarifiwa juu ya tukio hilo lakini hakulishuhudia akisema alikuwa katika ukumbi mwingine. Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwani tangu juzi, simu yake imekuwa ikiita bila kupokewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Bernadette Kinabo alisema amesikia kutokea kwa tukio hilo.

Alisema tukio hilo limemsikitisha na kuwataka madiwani kuhimili jambo hata kama ni kutukanwa... “Nimearifiwa juu ya jambo hilo japo si kwa undani sana. Ila kwa kweli madiwani wanapaswa kujiheshimu ili na wengine wajifunze kutoka kwao. Haipendezi madiwani kutumia lugha ya kuudhi zaidi yao na anayetolewa lugha hiyo naye lazima azuie jazba.”

Habari ya Daniel Mjema via Mwananchi, MOSHI


No comments:

Post a Comment