Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 19, 2012

MAMENEJA 29 TANESCO WASIMAMISHWA KAZI KWA HUJUMA..!

Mameneja 29 wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wameshimamishwa kazi baada ya kuhusishwa kuhujumu utendaji wa shirika hilo kwa kuunganisha umeme kinyume cha utaratibu, wizi wa mafuta ya transfoma na nyaya za umeme.

Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alisema hayo jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi na operesheni inayoendelea nchini kote ya kuwasaka watu wanaojiunganishia umeme kinyemela.

“Tanesco ya sasa siyo ile ya zamani. Tunajisafisha na tayari wapo waliochukuliwa hatua na wengine kusimamishwa,” alisema lakini akakataa kutaja majina ya vigogo waliosimamishwa.

Alisema waliosimamishwa kazi ni wenye vyeo vya umeneja na maofisa.

Akizungumzia hali ya umeme nchini, Badra alisema hakutakuwa na mgawo wa umeme kwa sababu sasa hivi Tanesco haitegemei zaidi umeme wa maji, isipokuwa wanatumia umeme wa mafuta na gesi.

“Hakuna mgawo na hatutarajii kuwa na mgawo. Sasa hivi tunatumia umeme wa mafuta na gesi,” alisisitiza.

Kuhusu kukatika kwa umeme katika baadhi ya mikoa, alisema hiyo inatokana na sababu za kupanga wenyewe ili kuruhusu kufanya marekebisho katika njia za umeme au wakati mwingine inatokana na sababu tofauti kama vile mvua za radi, upepo, kukatika kwa miti kunakosababisha kuharibu mfumo wa usambazaji umeme au hata gridi ya taifa kupata matatizo ya kiufundi.

Katika hatua nyingine, Badra alisema Tanzania inafanya mazungumzo na serikali ya Ethiopia ili kuangalia uwezekano wa kununua umeme kutoka nchi hiyo.

“Njia kuu za kusafirisha umeme zitakapounganishwa na kukamilika, nchi yetu itaweza kununua umeme unaozalishwa kwa njia ya maji na unaouzwa kwa bei nafuu moja kwa moja kutoka nchi kama Ethiopia,” alisema na kuongeza:

“Ethiopia wanazalisha nishati ya umeme megawati 10,000 na kubakiwa na ziada ya megawati 8,000.”

Alikuwa akizungumzia mkutano wa mawaziri wa nishati wa nchi za Afrika Mashariki na Kati kuhusu mtandao wa usambazaji wa nishati hiyo unaojulikana kama Eastern Africa Power Pool (EAPP) unaozihusisha nchi 11 za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Djibout, Ethiopia, Libya, Jamhuri ya Sudan na Misri.

No comments:

Post a Comment