Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, October 6, 2012

MHANDO WA TANESCO AFIKISHWA KORTINI DAR

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) aliyesimamishwa kazi, William Mhando

Mkurugenzi  Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) aliyesimamishwa kazi, William Mhando, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kuondolewa bila kusomewa shtaka.

Mhando alifikishwa mahakamani hapo jana kati ya saa 7:00 mchana na saa 9:00 alasiri, akiwa ndani ya gari aina ya Noah, chini ya ulinzi wa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya mahakama hiyo,  Mhando alifikishwa mahakamani hapo lakini hakushushwa kutoka ndani ya gari kutokana na muda wa mahakama kufanya kazi ukiwa umekwisha.

“Amefika hapa akiwa ndani ya gari aina ya Noah, lakini hakushushwa, zaidi mtu mmoja alishuka ndani ya gari hilo na kuingia kwenye mahakamani na kutoka, kisha akarejea kwenye gari na kuondoka, wamekuja muda wa mahakama ukiwa umeisha,” kimebainisha chanzo hicho.

Julai mwaka huu, Mkurugenzi huyo alisimamishwa kazi na bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka katika shirika hilo.

Taarifa za kusimamishwa mkurugenzi huyo zilitolewa na bodi hiyo na kusainiwa na mwenyekiti wake, Jenerali Mstaafu Robert Mboma.

Aidha, katika sakata hilo watendaji wakuu ambao ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi Harun Mattambo nao walisimamishwa kufuatia tuhuma hizo za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. 

NIPASHE Jumamosi jana ilifika katika ofisi za Takukuru ili kupata undani ya suala hilo, na kujibiwa na mtu wa mapokezi kuwa, mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, amesafiri na watendaji wengine akiwemo msemaji wa taasisi hiyo, wapo kwenye kikao.

No comments:

Post a Comment