Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe |
Jinamizi la anguko kwa ‘vigogo’ ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), limemkumba Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, baada ya kushindwa katika ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho.
Chikawe anaingia kwenye orodha ya ‘vigogo’ kadhaa waliobwagwa, wakiwania nafasi hiyo, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Fredreck Sumaye.
Taarifa kutoka wilaya ya Nachingwea alipokuwa anawania ujumbe wa Nec, zilieleza kuwa Chikawe, `aliangukia pua’ baada ya kupata kura 503 dhidi ya 749 za Fadhili Liwaka aliyeibuka mshindi.
Hata hivyo, wakati Chikawe `akiangukia pua’, taarifa zinaeleza kuwa mshindi wa nafasi hiyo, Liwaka, alianguka chini na kupoteza fahamu baada ya matokeo kutangazwa.
Ilisadikiwa kuwa, pamoja na mambo mengine, kuanguka kwa Liwaka, kulisababishwa na kutoamini ushindi wake dhidi ya ‘kigogo’ huyo mwenye nguvu kubwa ndani ya CCM wilayani Nachingwea.
Hali hiyo iliwafanya wanachama wa CCM na waliokuwa karibu na eneo hilo, kumpeleka hospitali ya wilaya kwa uchunguzi na tiba.
Wakati Chikawe akishindwa, mtu anayetajwa kwa jina moja la Kamlo, akiaminika kuwa swahiba wake (Chikawe) kisiasa, alishindwa katika kuwania Uenyekiti wa CCM wilayani humo.
Nafasi hiyo ilichukuliwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Albert Mnali.
Vyanzo vilivyoshiriki uchaguzi huo vilieleza kuwa Mnali alipata kura 948 dhidi ya 74 za Kamlo.
ALIWAHI KUMCHAPA VIBOKO MWALIMU
Februari 2009, iliripotiwa kuwa, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Mnali aliwaamuru polisi kuwachapa voboko walimu 32 wa shule tatu tofauti za msingi wilayani huo.
Mnali alifikia hatua hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba.
Kwa tukio hilo, Mnali ambaye baadaye alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete, alikuwa gumzo kwenye maeneo tofauti ya nchi, huku akipachikwa jina la ‘Mzee wa viboko’.
NGAWAIYA AZUSHIWA KUFA KILIMANJARO
Katika hatua nyingine, mizengwe imezidi kuibuka ndani ya CCM ambapo sasa, mgombea Uenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Thomas Ngawaiya, amezushiwa kufa.
Taarifa ambazo NIPASHE Jumamosi imezipata kutoka mkoani humo na kuthibitishwa na Ngawaiya, zilieleza kuwepo uvumi unaoenezwa kuwa mwanasiasa huyo hayupo duniani.
“Huo uvumi upo, ninadhani ni sehemu ya mchezo mchafu unaofanywa na watu wachache ndani ya CCM, lakini mwisho wa siku hali itatulia,” alisema.
Hata hivyo, Ngawaiya alisema mbali na kuzushiwa kifo, zipo taarifa nyingine zinazoenezwa kwamba jina lake lilikatwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) asiwanie nafasi hiyo.
Ngawaiya ni mmoja wa wanachama wanaoelezwa kupata ushindani mkubwa katika kuwania nafasi hiyo inayowajumuisha pia Mildred Julius KISAMO (52), James Amos KOMBE (62) na Iddi Juma MOHAMED (58).
Wakati taarifa zikieleza hivyo, wiki iliyopita, Ngawaiya alionekana kwenye mitaa kadhaa ya mjini Moshi, akitembea na kugawa vipeperushi vya CCM na beji zenye picha ya Rais Jakaya Kikwete.
Aliiambia NIPASHE Jumamosi kuwa kitendo hicho kilikuwa sehemu ya kufurahia kuteuliwa kwake kulikofanywa na Nec, ikiongozwa na Rais Kikwete.
MFANYABIASHARA ACHAGULIWA GEITA
Kutoka wilaya ya Nyang'wale mkoani Geita, mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Adam Mtore (38), amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM katika wilaya hiyo.
Mtore alipata kura 325 kati ya kura 585 zilizopigwa hivyo kuwashinda Mwalimu Sostheness Ngusa (25) na Mayunga Magiri (235).
ALIYEKUWA MBUNGE AIBUKA KIDEDEA NEC NYANG’WALE
Aliyewahi kuwa Mbunge wa Nyang'wale, James Msalika, ameibuka kidedea kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Nec.
Msalika alipata kura 503 dhidi ya washindani wake, Dk Peter Mwininga aliyepata kura 57 na Jacob Nyanda aliyeambulia kura tisa.
NANSIO, MUHEZA WATANGAZA MATOKEO USIKU WA MANANE
Matokeo ya uchaguzi katika wilaya ya Nansio yaliyotangazwa usiku wa manane kuamkia jana.
Walioshinda ni Ally Mambile (Mwenyekiti wa wilaya) aliyepata kura 614 dhidi ya Focas Katembo (150) na Jungu Tungalaza (157).
Nafasi ya ujumbe wa Nec imechukuliwa na James Kazoba alipata kura 392 na kumshinda Dk. Deusdedit Makalius aliyepata kura 368.
Wilayani Muheza katika mkoa wa Tanga, Laicky Gugu, alichaguliwa kuwa mjumbe wa Nec.
Uchaguzi huo uliofanyika wilayani Muheza ulimalizika saa tisa za usiku.
Gugu alipata kura 514 dhidi ya Faustine Chombo (472), Husseni Katua (17) na Shariffa Kivugo, ambaye hakuambulia kura hata moja.
Ujumbe wa Nec (wazazi) ilichukuliwa na Sofiani Mwedi na Ally Mkufya.
NYALANDU HAKAMATIKI SINGIDA
Naibu Waziri Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Nec kupitia wilaya ya Singida.
Nyalandu alipata kura 897 dhidi ya Deogratius Daffi (131) na Manase Sabasaba (104).
Waliochaguliwa Nec kupitia vijana ni Jumanne Salamu, Deogratius Sabasaba, Daud Elias na Hilda Lazaro, wakati kundi la UWT ni Amina Mweli, Faida Lazaro, Neema Matiti na Zuwena Mohamed.
Pia wajumbe wawili wa Nec (wazazi) ni Justine Monko na Edward Yared.
Habari hii imeandikwa na Mashaka Mgeta, Steven William, Muheza, Renatus Masuguliko, Nyang'wale, Jovither Kaijage, Ukerewe na Elisante John, Singida.
No comments:
Post a Comment