Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Tuesday, October 16, 2012

Muswada wa fao la kujitoa wawasilishwa...!

Mbunge wa Ubungo ( Chadema), John Mnyika

Mbunge wa Ubungo ( Chadema), John Mnyika, amewasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha muswada binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii, ya  mwaka 2012 kwa hati ya dharura.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari jana mbunge huyo, amewasilisha muswada huo kwa hati ya dharura kwa mujibu wa kanuni ya 81 ya kanuni za kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).

Mnyika alisema amechukua uamuzi huo kwa kuwa mpaka sasa zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Mkutano wa Bunge kuanza mjini Dodoma,  hakuna jitihada zozote zilizoonyeshwa na serikali kushughulikia suala hilo.

“Serikali  mpaka sasa haijaitisha mkutano wowote kati yake na wafanyakazi, pamoja na wadau wa mifuko ya jamii ili kupokea mapendekezo hali inayoashiria kuwa upo uwezekano kwamba muswada huo usiwasilishwe kwa wakati,” alisema Mnyika.

Mnyika aliongeza kuwa lengo la muswada huo ni kufanya marekebisho yenye kuboresha mfumo wa utoaji wa mafao nchini ikiwamo kuwezesha kutolewa kwa fao la kujitoa na mafao mengine muhimu ambayo hayatolewi katika utaratibu wa sasa wa mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii.

Hata  hivyo, jitihada za NIPASHE kumtafuta Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ili athibitishe kama amepokea kusudio hilo la Mnyika hazikuzaa matunda, kwa kuwa simu yake ya kiganjani haikuwa na majibu.

Katika mkutano wa Tisa wa Bunge, sakata la fao la kujitoa lilizua malumbano badaa ya serikali Aprili mwaka huu kupitisha sheria kwamba ili mwanachama aweze kupata mafao yake, lazima awe ametimiza umri wa miaka 55 au 60.

Katika mkutano huo wa Bunge la bajeti, Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), aliwasilisha maelezo binafsi akitaka muswada huo urejeshwe bungeni ili ufanyiwe marekebisho.

Jafo alitaka kupitishwa kwa azimio ili sheria hiyo irejeshwe bungeni na kufanyiwa mabadiliko ya kifungu cha muda wa ukomo wa kuchukua mafao ya mteja kutoka cha sasa, ambacho ni kati ya miaka 55 hadi 60 na kisha kimruhusu mwanachama kuchukua fao la kujitoa kabla ya umri rasmi wa kustaafu.

Akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2012/2013 bungeni katika mkutano huo wa Bunge, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alisema sheria hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na umma na kutangazwa kwa hisia tofauti na vyombo mbalimbali vya habari.

Waziri Kabaka alisema baadhi ya vyombo vya habari vilidai kuwa serikali iliweka kifungu cha kufuta fao la kujitoa kutokana na mifuko mingi ya jamii kuwa katika hali mbaya kifedha.

“Wengine walisema NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii) iko hatarini kufilisika baada ya serikali kushindwa kulilipa shirika hilo kutokana na uwekezaji mbaya uliofanywa,” alisema Kabaka.

Alisema wapo waliodai kuwa hatua hiyo ya serikali ina lenga kutunisha mifuko ya hifadhi ya jamii ili baadaye ichukue fedha hizo kwa ajili ya chaguzi mbalimbali.

Alisema sababu zote hizo hazikuwa sahihi na kwamba serikali inachokiona ni kuwa haikutoa elimu ya kutosha kabla ya kuwasilisha muswada huo wa sheria Aprili, mwaka huu.

“Serikali imesikia malalamiko ya wafanyakazi na hoja za wabunge na kuzingatia yote yaliyopo katika azimio la Bunge na imekubali kuleta muswada kwa hati ya dharura,” alisema Kabaka.

Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, iliishauri serikali kuirekebisha sheria hiyo haraka kwa kuwa imeleta mtafaruku mkubwa kwa wafanyakazi.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mbunge wa Nkenge, Assumpter Mshama, alisema kamati imebaini kuwa sheria mpya ilianza kutumia hata kabla ya kutungwa kwa kanuni zake.

Kutokana na upungufu huo, kamati hiyo ilipendekeza kurejeshwa kwa fao la kujitoa na mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kulipia mkopo wa nyumba.

Kamati hiyo ilipendekeza kufanyiwa marekebisho sheria hiyo ili mwanachama aruhusiwe kutumia sehemu ya mafao yake ya uzeeni kwa ajili ya kugharimia shughuli nyingine yoyote kwa lengo la kuandaa mazingira mazuri ya maisha baada ya kustaafu.

Kuwasilishwa kwa maelezo binafsi ya Jafo yaliyosababisha Bunge kupitisha azimio lake katika mkutano huo na maelezo ya Waziri Kabaka kulizima mjadala mkali uliotarajiwa kuibuka bungeni.

Wabunge wengi walikuwa wamepanga kukwamisha bajeti ya wizara hiyo endapo Serikali ingeshikilia msimamo wake wa kukataa kuleta muswada huo bungeni katika mkutano ujao.

Sheria hiyo iliibua chuki na hasira za wafanyakazi nchi nzima, huku baadhi ya vyama vya wafanyakazi vikijiandaa kuendesha maandamano na migomo nchi nzima kupinga sheria hiyo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment