Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, October 27, 2012

Muswada wa fao la kujitoa wazidi kupingwa...!

Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Pichani)amemtaka Rais Jakaya Kikwete kutia saini hati ya dharura ya kuwezesha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo ya fao la kujitoa kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii, kuwasilishwa bungeni.

Katika ombi hilo mbunge huyo ametaka mifuko mingine ya Mfuko wa Pensheni wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa umma-Serikali Kuu (PSPF) na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) ifanyiwe marekebisho.

Mnyika amefikia hatua hiyo, kufuatia maelezo yaliyotolewa Oktoba 14, mwaka huu na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, kuwa marekebisho ya kurejesha fao la kujitoa yatafanyika mpaka mkutano wa kumi wa Bunge mwezi Februari mwakani kukinzana na tangazo la serikali lililotolewa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema kuwa, kufuatia hatua yake na zile za wadau wengine serikalini kinyume na msimamo huo wa Mahanga, Serikali imechapa katika Gazeti lake muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali na juzuu 40 namba 93.

Alisema muswada huo katika sehemu ya 6 vifungu vya 13, 14 na 15 imependekeza kurejesha fao la kujitoa kwa upande wa Mfuko wa Mashirika ya Umma (PPF) na haujawasilishwa kwa hati ya dharura kama ilivyoazimiwa na kuahidiwa.

Aidha, alisema sehemu hiyo ya sita ya muswada huo haijakidhi mahitaji na matakwa ya Azimio la Bunge la Agosti 6, mwaka huu lililoungwa mkono na wabunge katika kikao cha 41 cha mkutano wa nane hivyo itasababisha mgogoro baina ya serikali na wafanyakazi na waajiri na wafanyakazi na kuathiri uchumi wa nchi.

“Katiba inamtambua Rais kuwa ni mkuu wa nchi na kiongozi wa serikali, Ibara ya 34 inaeleza mamlaka yote yapo mikononi mwake na kwamba madaraka hayo yanaweza kutekelezwa na watu wengine kwa niaba yake, na ibara ya 35 inaeleza shughuli zote za serikali zitatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba yake, hivyo wakati umefika wafanyakazi kuchukua hatua,” alisema na kuongeza:

“Hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na wafanyakazi na wadau wengine ni kuwezesha Rais kuingilia kati kabla ya mkutano wa bunge kuanza Oktoba 30, mwaka huu” alisema.

Alisema Rais anatakiwa kutumia madaraka na mamlaka aliyonayo kuondoa udhaifu uliojitokeza wa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema na Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka wa kutotekeleza kwa wakati mapendekezo na maamuzi ya Bunge pamoja na ahadi ya serikali kwa wabunge.

“Kanuni ya 80 fasili ya 4 inaelekeza kwamba ‘Muswada wowote wa sheria wa serikali wa dharura hautaingizwa kwenye shughuli za Bunge bila ya kuwa na hati iliyowekwa saini na Rais inayoelekeza kuwa muswada uliotajwa kwenye hati hii ni wa dharura’,” alisema.

Mnyika alisema kuwa, iwapo Rais hataweka saini hati ya dharura au serikali haitawasilisha bungeni hoja kwa mujibu wa kanuni ya 93 fasihi ya 4, bunge litabanwa na fasihi ya 1 ambayo inakataza bunge kushughulikia hatua zaidi ya moja katika mkutano mmoja.

Alibainisha kuwa tafsiri ya hilo ni kwamba sheria hiyo itasubiri kupitishwa Februari mwakani katika mkutano wa kumi wa Bunge hivyo wafanyakazi kuendelea kunyimwa mafao yao ya kujitoa.

Alisema Rais anatakiwa atengue tangazo na agizo la SSRA linaloeleza kuwa, ‘kufuatia kuanza kutumika kwa sheria hiyo (ya 13 Aprili 2012’maombi mapya yamesitishwa kwa kipindi cha miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuiwezesha mamlaka hiyo kutoa elimu kwa wadau.

Aliongeza kuwa marekebisho ya sheria hiyo kwa upande wa kusitisha fao la kujitoa yaliyofanywa Aprili 13, mwaka huu, yalihusu zaidi mashirika ya umma hivyo hayakupashwa kutumika kama sababu ya kusitisha mafao ya mifuko yote.

Alisema wafanyakazi wanaodai mafao yao ya haki na stahili ni pamoja na kupata fao la kujitoa mazingira yakilazimisha hivyo kabla ya pensheni ya uzeeni.

Alifafanua kuwa, kusubiriwa kwa marekebisho ya sheria hiyo hakupaswi kuwa kisingizio cha kuendelea kusitisha mafao yao ya kujitoa.

Mnyika alisema kuwa iwapo Rais na serikali yake haitachukua hatua, Octoba 30, mwaka huu ataeleza nini kitakachofanyika.

HABARI NA ROMANA MALLYA
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment