Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 5, 2012

NUNDU,MAJI MAREFU CHALI


Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani 'Professa Maji Marefu'
 
Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani maarufu kama Professa Maji Marefu, wamebwagwa katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Meya wa zamani wa Jiji la Tanga, Kassim Kisauji ameibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho kupitia Wilaya ya Tanga kwa kupata kura 514, huku Nundu ambaye pia ni Mbunge wa Tanga Mjini akipata kura 127 kati ya kura halali 1,175 zilizopigwa.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulilazimika kurudiwa katika raundi ya pili baada ya Kisauji  kushindwa kupata nusu ya kura.

Alipata kura 556 akifuatiwa na Saumu Bendera 458, Nundu 127 na Salehe Bakari Masudi 37.

Baada ya uchaguzi huo kurudiwa ndipo Kisauji alishinda kwa kupata kura 514 akifuatiwa na Bendera aliyepata kura 446.

Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga ilikwenda kwa  Kassim Mbughuni aliyepata kura 540 na kuwashinda Mwanshamba Pashua kwa kura 372 huku Mkuu wa Wilaya wa zamani Samweli Juma Kamote akipata kura 200 na Salim Rashid Al-Mazurui kura 98.

Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutanio Mkuu wa CCM Taifa ni Danny Mgaza aliyepata kura 485, Muzzamili Shemdoe (485), Mozza Mohamed (427), Mwanshamba Shekue (412) na Rukia Mapinda (413).

Nafasi ya Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Tanga ilikwenda kwa Lipakisio Kapande huku Bernard Goliama akishinda kuwa Katibu wa Mipango, Uchumi na Fedha.

Wakati huo huo, Dk. Edmund Mndolwa aliibuka kidedea katika nafasi ya ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Korogwe Vijijini dhidi ya Profesa Maji Marefu.

Mndolwa ambaye kitaaluma ni mchumi, alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura  962 dhidi ya kura 310 alizopata mpinzani wake.

Katika uchaguzi huo uliosimamiwa na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Pangani, Mohamed Rished, nafasi hiyo ya Nec Jimbo la Korogwe Vijijini iligombewa na wagombea wanne.

Wagombea wengine walikuwa ni Aweso Mandondo aliyepata kura 112 na George Kinyasi kura 21.

Kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya Korogwe Vijijini, Nassor Malingumu alifanikiwa kutetea nafasi yake kwa kupata kura 1,230 dhidi ya kura 164 alizopata mpinzani wake, Majaliwa Tekero.

Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Sadick Kallaghe, Halima Mussa, Christine Kabelwa, Mohamed Dodoadoa na Seif Bilal.

LAIZER AKATAA UCHAGUZI KURUDIWA


Katika uchaguzi wa ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, Mbunge wa Longido, Lekule Laizer, ambaye alikuwa mmoja wa wagombea, amekataa kurudiwa kwa uchaguzi huo baada ya kuongoza, lakini kura zake zikashindwa kufikia zaidi ya asilimia 50.

Katika uchaguzi huo uliofanyika juzi, Laizer aliongoza kwa kupata kura  416, Peter Mushau kura 381 na Syokino kura 355. Kura mbili ziliharibika.

Mushau alitaka uchaguzi huo urudiwe kwa hoja kuwa kanuni za uchaguzi wa CCM zinaelekeza kuwa mshindi lazima apatikane kwa kupata kura kuanzia asilimia 50.

Hata hivyo, Laizer alikataa kurudiwa kwa uchaguzi huo, hivyo aliyekuwa msimamizi, Halid Kijazi, aliamua kuahirisha shughuli hiyo na kuahidi kuwa uamuzi utatangazwa baada ya wiki moja.

 NIPASHE jana ilimtafuta Laizer ili aeleze sababu za kukataa kurudiwa kwa uchaguzi huo, lakini simu yake ilikuwa imefungwa.

 UVCCM DODOMA WACHAGUANA


Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dodoma imepata  Mwenyekiti wake mpya, Henry Msunga.

Msunga alishinda nafasi hiyo baada ya kupata kura 268 dhidi ya washindani wenzake, Wenslaus Mazanda, aliyepata kura 110 na Said Sambala aliyepata kura 28.

 Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa UVCCM Mkoa, Josephat Ndulango, alisema kuwa katika nafasi ya kuwakilisha Baraza Kuu Taifa walikuwa wagombea wawili na aliyeshinda ni Egla Mamoto aliyepata kura 232 dhidi ya mgombea mwenzake, Juma Mtoro, aliyepata kura 141.

 Kwa upande wa uwakilishi wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, aliyeshinda ni Josephat Chitinka kwa kura 215 baada ya kumshinda mpinzani wake, Fatuma Issa kwa kura 71.

 Nafasi nyingine iliyoshindaniwa ni ya uwakilishi wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) mkoa ambayo ilikwenda kwa Fatuma Sanda aliyepata kura 177 huku washindani wake Neema Mkobalo kura 126, na Egla Mamoto kura 44.

 Katika nafasi ya uwakilishi wa Jumuiya ya Wazazi mkoa aliyeshinda ni Philipo Funga, ambaye alipata kura 208 huku wagombea wenzake Amani Mfaume aakipata kura 87, Silvester Cosmas kura 27 na Pascal Rwechungura kura 14.

Awali akifungua uchaguzi huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoa wa Dodoma Anton Mavunde aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwachagua viongozi bora watakaowasaidika kuwafikisha wanapopataka na siyo kujali fedha za wagombea.

Mavunde alisema kuwa kiongozi anayetumia fedha ili kuchaguliwa hafai kuwaongoza kwa kuwa fedha siku zote haziwezi kumuandaa kiongozi bora.

 Aidha, alitoa wito kwa viongozi watakao chaguliwa kizitumia nafasi zao katika kuwaletea mabadiliko wana-CCM, kwa kuwa wabunifu katika kubuni miradi na kuiendeleza iliyopo.

WALIOCHAGULIWA UVCCM MTWARA

UVCCM Mkoa wa Mtwara imepata uongozi mpya kufuatia uchaguzi uliofanyika juzi.

Nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na Nestory Chilumba ambaye alipata kura 254 na kuwashinda Nasibu Haji (171) na Slaji Mohamedi (26). 

Nafasi ya ujumbe Baraza Kuu la Taifa ilikwenda kwa Mwidini Nanilah aliyepata kura 367.

 Katika kinyanganyilo cha nafasi ya wajumbe Mkutano Mkuu CCM Taifa ilikwenda kwa Amani Abdul akiibuka kidedea kwa kupata kura 277.

Nafasi ya uwakilishi katika UWT ilichukiliwa na Diya Mwanya ambaye  aliibuka kidedea kwa kupata kura 250.

Kwa upande wa uwakilishi katika Jumuiya ya Wazazi, ilichukuliwa na Palongo Abdul baada ya kupata kura 336.

WILAYA YA KISHAPU

Katika uchaguzi wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti ni Shija Ntelezu wakati aliyechukua nafasi ya ujumbe wa Nec ni Boniface Butondo.

No comments:

Post a Comment