Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 5, 2012

RIPOTI MAUAJI YA MWANGOSI IKO TAYARI

Aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi

Kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, imekamilisha kazi yake na sasa inatarajia kukabidhi ripoti ya uchunguzi huo wiki ijayo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Septemba 5, mwaka huu, ilihusisha wajumbe kutoka tasnia za sheria, habari, Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakiongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji Ihema aliliambia NIPASHE jana kuwa watakabidhi ripoti hiyo Jumanne ijayo baada ya Waziri Nchimbi kurejea nchini.

“Tutakabidhi (ripoti) Jumanne (ijayo). Tunamngoja Waziri arudi tumkabidhi,” alisema Jaji Ihema alipokuwa akijibu swali la NIPASHE lililotaka kujua kama kamati imekamilisha kazi yake na lini itakabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Nchimbi.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Nantanga, Waziri Nchimbi yuko safarini jijini Geneva, Uswisi, kwa shughuli zinazohusu masuala ya wakimbizi.

Nantanga aliliambia NIPASHE kuwa hadi jana wizara ilikuwa bado haijakabidhiwa ripoti hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Septemba 5, mwaka huu, Waziri Nchimbi alisema nia ya kuunda kamati hiyo ni kupata matokeo yasiyoegemea upande wowote kwa kuwa kamati iliyoundwa ni huru.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambaye pia ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications; Ofisa Mipango wa Baraza la Habari Nchini (MCT), Pili Mtambalike; mtaalamu wa milipuko kutoka JWTZ, Kanali Wema Wapo na Naibu Kamishna wa Polisi, Isaya Mngulu.

Kamati hiyo ilipewa hadidu za rejea sita na ilipewa siku 30, kuanzia Septemba 5, mwaka huu, kufanya kazi hiyo.

Hadidu rejea hizo ni kuchunguza chanzo cha kifo cha Mwangosi, kama kuna uhasama kati ya waandishi wa Iringa na Polisi, kama kuna orodha ya waandishi watatu waliopangwa kushughulikiwa na polisi mkoani humo.

Hadidu rejea nyingine ni kama kuna taratibu za kukata rufaa ya vyama vya siasa dhidi ya polisi pindi mikutano yao inapozuiwa, je, kuna tatizo la mahusiano kati ya polisi na vyama vya siasa kwa ujumla wake na kama ukubwa wa nguvu zilizotumika katika tukio la Iringa ni sahihi.

Waziri Nchimbi alisema kuna maneno mengi yanayozungumzwa kuhusu kuuawa kwa mwandishi huyo, hivyo matokeo ya uchunguzi wa tume yataweka wazi uhalisia wa mauaji hayo.

Kufuatia kuundwa kwa kamati hiyo, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, aliitisha mkutano na waandishi habari siku zilizofuatia na kutangaza msimamo wa chama chake wa kutoiunga mkono kamati hiyo kwa madai kwamba, imeundwa kinyume cha Sheria ya Tume za Uchunguzi ya Mwaka 1962 Sura ya 29.

Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, tume zote za uchunguzi huundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye huzipa pia hadidu za rejea na baadaye kutoa ripoti kwake au hadharani endapo ataelekeza hivyo katika hadidu za rejea atakazoipa na haziundwi na waziri.

Hivyo, akasema tume hiyo haina lengo la kuchunguza mauaji, bali kurekebisha uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari.

Alisema kwa kuwa tume hiyo siyo ya kuchunguza mauaji, Chadema haitaiunga mkono na pia itawashauri Watanzania, wawe wanachama wa chama hicho au la kutoiunga mkono.

Lissu alisema hawaungi mkono tume hiyo kwa sababu masuala ya kuunda tume za uchunguzi wa mambo yanayotokea kitaifa ni jukumu kisheria la Rais na siyo la waziri, ambaye anaowasimamia ndiyo watuhumiwa wa kile kinachotakiwa kuchunguzwa.

Siku moja baadaye, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia msemaji wake, Nantanga ilitoa ufafanuzi na kusema kilichoundwa na Waziri Nchimbi ni Kamati ili kumsaidia kupata majibu ya maswali mbalimbali, likiwamo nini kilikuwa chanzo cha kifo cha mwandishi huyo, ambayo hakuwa na majibu yake, na kwamba, hakuwa ameunda tume.

“Kupitia taarifa hii, tunapenda kuuarifu umma kuwa Waziri Nchimbi hakuunda Tume ila aliunda Kamati hiyo kwa mamlaka aliyonayo kama waziri na uundaji wa Kamati hii hauhusiani kwa vyovyote na matakwa ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, Marejeo ya Mwaka 2002,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Nantanga.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa utaratibu wa kutumia Kamati kutafiti jambo kwa kina kwa ajili ya kumshauri waziri au kiongozi mwingine yoyote ni wa kawaida katika utendaji na utekelezaji wa majukumu ya umma.

Mwangosi, ambaye alikuwa pia Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), aliuawa kwa kupigwa na bomu na kusambaratisha mwili wake wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwazuia kufungua tawi la chama hicho, katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo, Septemba 2, mwaka huu.

Tayari askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mwenye namba G2573 Pasificus Cleophace Simon (23), anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya Mwangosi, amefikishwa mahakamani kwa mashitaka ya mauaji.

No comments:

Post a Comment