Ofisa Uhamiaji mkoani Mwanza, Albert
Buchafwe, amenusurika kuuawa baada ya askari polisi kumiminia risasi
tano kwa kile kilichodaiwa kuwa walimfananisha na jambazi sugu.
Akisimulia mkasa huo wa aina yake, Buchafwe alisema mkasa huo ulitokea
usiku wa kuamkia jana saa 4:00 usiku alipokuwa akirejea nyumbani kwake
maeneo ya Mhandu, Nyakato jijini hapa.
Alisema akiwa njiani kurejea nyumbani akiendesha gari aina ya Land Rover
Discovery yenye namba za usajili T318 BJE, alipofika eneo la
Machinjioni, aliona gari kwa mbele yake ambayo ilimmulika kwa taa zenye
mwanga mkali kama ishara ya kumtaka asimame.
Aliongeza kuwa kama vile haitoshi, gari hilo lilimsogelea kwa kasi na
kumzuia mbele, kitendo kilichomshtua na kulazimika kushusha kioo kujua
kulikoni.
Kwa mujibu wa Buchafwe, baada ya kushusha kioo cha gari alimuona askari
mmoja akishuka kutoka kwenye gari aina ya Suzuki rangi nyekundu
iliyompita kwa kasi na akamtambua mtu huyo kuwa ni Abuu ambaye ni askari
polisi.
“Baada ya lile gari kunizuia mbele, aliteremka mtu mmoja kunifuata huku
akinitaka niteremke kutoka kwenye gari, mimi nikashusha kioo cha gari na
kumuita kwa jina nikisema, Abuu ni mimi bwana kwani vipi?", alisema.
Aliongeza kwamba licha ya kumuita kwa jina, askari huyo (Abuu), alimjibu
kwa sauti ya ukali akimtaka ateremke haraka kutoka kwenye gari
vinginevyo atampiga risasi.
Alifafanua kuwa akiwa amepigwa butwaa, alitokea askari mwingine
aliyekuwa na bunduki aina ya SMG huku Abuu naye akitoa bastola zake
mbili.
Ofisa Uhamiaji huyo alidai kuwa baada ya kuona hali hiyo, aliamua
kugeuza gari haraka na kuondoka kwa kasi huku nyuma askari hao
wakimfyatulia risasi zipatazo tano ambazo hata hivyo, ziliishia kupiga
bodi ya gari lake.
“Nilipoondoa gari kwa kasi, wao waliendelea kunirushia risasi,
namshukuru Mungu hakuna iliyonipata, nikaamua kwenda kulala Igoma badala
ya nyumbani kwangu,” alisema.
Alisema ilipofika asubuhi, alielekea ofisini kwake ambako aliamua
kumsimulia bosi wake (Ofisa Uhamiaji wa Mkoa) kuhusu mkasa huo ambaye
naye alimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow,
kumweleza kilichotokea.
Kwa mujibu wa Buchafwe, Kamanda Barlow alimweleza Ofisa Uhamiaji wa mkoa
kwamba (Buchafwe) alikuwa ameingia kwenye mtego wa polisi na kwamba
ilikuwa auawe kwa kupigwa risasi.
Alipoulizwa jana kuhusiana na tukio hilo, Kamanda Barlow alithibitisha
na kusema kwamba Ofisa Uhamiaji huyo alifananishwa kwa kila kitu na
jambazi aliyekuwa anakusudia kwenda kuvamia na kupora katika ghala moja
maeneo ya Nyakato ambalo hata hivyo hakulitaja.
“Ni kweli kuna tukio kama hilo, lakini yalikuwa ni mashambulizi ya
gizani kwa sababu askari walimfananisha Ofisa Uhamiaji na jambazi
waliyekuwa wamemwekea mtego, nadhani ana bahati kwani ndiyo kawaida yetu
huwa hatubembelezani na majambazi,” alisema.
No comments:
Post a Comment