Kaimu Maofisa Elimu wanne wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Juhudi na Ukonga, jijini Dar es Salaam, wamefikishwa mahakamani kwa
tuhuma za kushindwa kufanya uhakiki wa mishahara ya walimu 23, kutumia
madaraka vibaya na kuiba Sh. milioni 11.8 zikiwa ni mali ya serikali.
Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
jijini Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Agnes
Mchome, Jana.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(Takukuru), Allen Kasamala, aliwataja Makaimu Maofisa Elimu hao kuwa ni
Elizabeth Thomas, Mercy Nyalusi na Joseph Kaika.
alimtaja Mwalimu Mkuu wa Shule hizo kuwa ni Simon Jerome na Clara
Nyongeja aliyeajiriwa na Wizara ya Fedha kama mtaalamu wa kompyuta.
Inadaiwa kuwa mshitakiwa Elizabeth na Mercy hawakuweza kupanda kizimbani
baada ya kuuguwa ghafla kazini kabla ya kufikishwa mahakamani.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mchome jana, Kasamala alidai kuwa
Februari 2010, washitakiwa walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa
kufanya uhakiki wa masalia ya mishahara ya walimu 23 yenye thamani ya
Sh. 11,825,000.
Kasamala alidai mashtaka sita yaliyobaki yote yanamkabili Mwalimu Jarome.
Alidai kwa kutumia madaraka yake vibaya, Machi Mosi, mwaka juzi
alimlazimisha Mwalimu George Masinde wa Shule ya Msingi Ukonga ampe Sh.
3,900,000 katika masalia ya mishahara yake.
Kasamala alidai pia kuwa Machi 2, mwaka juzi, Jarome alimlazimisha
Bahati Saidi, ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Ukonga ampe Sh.
3,895,000 kutoka katika masalia ya mishahara yake.
Alidai katika tarehe hiyo hiyo, Mwalimu Jerome alimlazimisha Mwalimu
mwingine wa Shule hiyo, Ester Mdachi, ampe Sh. 4,030,000 kutoka katika
masalia ya mishahara yake ili kujinufaisha.
Mwendesha mashtaka huyo alidai Machi 3, mwaka juzi, mshtakiwa huyo kwa
kutumia madaraka yake vibaya alimlazimisha Mwalimu Mwaija Chowo wa Shule
ya Msingi Ukonga atoe katika masalia ya mishahara yake Sh. milioni 3
ampe.
Alidai pia kuwa Jarome aliiiba Sh. 11,825,000 Machi 3, mwaka juzi,
zikiwa ni mali ya serikali na kwa njia ya rushwa mshtakiwa huyo
alijipatia Sh 3,000,000 kutoka kwa Mwaija Chowo ikiwa ni kishawishi cha
kutomchukulia hatua kwa kukataa kumkabidhi masalia ya mishahara yake.
Washitakiwa wote walikana kutenda makosa hayo, upelelezi haujakamilika
na Hakimu Mchome alikubali wadhaminiwe kwa masharti ya kuwa na wadhamini
wawili, mmoja awe mfanyakazi katika ofisi inayotambulika na wasaini
dhamana ya Sh. milioni 5.
Kasamala aliomba mahakama itoe hati ya kuwaita washitakiwa wasiofika mahakamani wafike ili wasomewe mashitaka yanayowakabili.
Hakimu alikubali kutoa hati hiyo, washitakiwa waliofikishwa mahakamani
walidhaminiwa na kesi iliahirishwa hadi Oktoba 24 mwaka huu kwa ajili ya
kutajwa.
No comments:
Post a Comment