Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, October 15, 2012

RAIS KIKWETE SAFARINI OMAN KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU NNE.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (pichani) anaanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku nne katika Taifa la Kifalme la Oman, ikiwa ni ziara ya kwanza ya Kiserikali kufanywa na Rais wa Tanzania katika nchi hiyo.
Rais Kikwete na ujumbe wake ameondoka mjini Dar es Salaam asubuhi ya leo, Jumatatu, Oktoba 15, 2012, kwenda Oman kuanza ziara hiyo inayofanyika kwa mwaliko wa Kiongozi wa Ufalme wa Oman, Mfalme Qaboos bin Said, ambaye atakuwa mwenyeji wake kwa siku zote nne.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat, Rais Kikwete anatarajiwa kulakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Mheshimiwa Yousef  bin Abdullah bin Alawi ambaye ataandamana naye hadi Jumba la Muscat Gate ambako Rais atapokelewa na Mfalme Qaboos. Kutoka hapo wataandamana hadi Kasri ya Kifalme ya Al Alam ambako atapokelewa rasmi kwa heshima zote za Kiserikali.
Shughuli kubwa ya jioni ya leo ya Mheshimiwa Rais itakuwa ni kufanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Serikali za Tanzania na Ufalme wa Oman na pia kuhudhuria dhifa rasmi ambayo Mfalme Qaboos atamwandalia mgeni wake kwenye Kasri ya Al Alam.
Kesho, Jumanne, Oktoba 16, 2012, Rais Kikwete atatembelea Jumba la Makumbusho la Majeshi ya Ulinzi ya Oman, atafungua Mkutano wa Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman, atashuhudia utiaji saini makubaliano ya mikataba miwili kati ya nchi hizo mbili, ukiwamo ule wa kuundwa kwa Baraza la Biashara la Tanzania na Oman na ule wa Kuendeleza na Kulinda Uwekezaji katika nchi hizo mbili.
Jioni, Rais Kikwete atatunukiwa nishani ya juu kabisa ambayo Ufalme wa Oman hutoa kwa viongozi wa nchi za nje ya First Order Medal kwenye Chakula Maalum cha Usiku kitakachoandaliwa na Mfalme Qaboos kwa heshima ya Rais Kikwete.
Rais Kikwete na ujumbe wake pia utakutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi Oman katika mkutano utakaofanyika kwenye Hoteli ya Kifalme ya Al Bustan.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Mheshimiwa Kikwete kutembelea Oman. Aliitembelea nchi hiyo mara ya kwanza mwaka 1998, wakati huo akiwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Oktoba, 2012

No comments:

Post a Comment