Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, October 10, 2012

RPC Kamuhanda alisimamia mauaji ya Mwangosi

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga (katikati), pamoja na mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri, Jesse Kwayu, wakati wa utoaji wa Ripoti Maalum ya Uchunguzi wa mazingira ya kifo aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi iliyotolewa hadharani jijini Dar es Salaam jana. Tume hiyo ya uchunguzi iliundwa na MCT kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri. Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari, Abubakar Karsan 

Alipigwa bomu baada ya operesheni

Uchunguzi wa timu maalum ya wanahabari iliyoundwa kuchunguza mazingira ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, umethibitisha kwamba, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alisimamia moja kwa moja mauaji ya mwanahabari huyo.

Kadhalika, timu hiyo imebainisha kuwa polisi kwa makusudi waliwashughulikia waandishi wa habari wa mkoa huo wakati wakikusanya habari za shughuli za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo, Septemba 2, mwaka huu.

Timu hiyo iliyoundwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), pia imebaini katika uchunguzi wake kuwa marehemu Mwangosi aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Kamanda Kamuhanda.

Ripoti ya timu hiyo iliwekwa hadharani na Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, katika mkutano kati ya MCT, TEF, baadhi ya wajumbe wa timu hiyo na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Timu hiyo iliongozwa na Meneja wa Utafiti na Machapisho wa MCT, John Mirenyi, huku wajumbe wengine wakiwa ni, Hawra Shamte, Mhariri wa masuala ya Siasa wa gazeti la Mwananchi na Simon Berege, Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Kitivo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.

Mukajanga alisema matokeo ya uchunguzi huo yanathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video, za mgando na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa za vyombo vya habari.

“Suala la kukosewa na kutotambulika, halipo kabisa, kwa sababu polisi waliwafukuza na kuwapiga na kuwajeruhi waandishi, ambao walikuwa wanawajua vizuri kabisa,” alisema Mukajanga.

Alisema hadi sasa taarifa kuhusu mauaji ya Mwangosi zimekuwa zikikinzana na kwamba, kuanzia hatua za awali, jitihada za kuficha ukweli zilijidhihirisha.

Mukajanga alisema timu hiyo imebaini kuwa kabla ya mauaji hayo, kulikuwapo na chuki na uhasama kati ya Kamanda Kamuhanda na marehemu Mwangosi katika kipindi chote cha saa kadhaa tangu mkutano wa waandishi wa habari na dakika chache kabla ya mauaji yake mbele ya Kamanda huyo huyo katika Kijiji hicho, Septemba 2, mwaka huu.

Alisema ripoti hiyo inaeleza kuwa chuki na uhasama uliokuwapo kati ya Kamanda Kamuhanda na marehemu Mwangosi, unaibua maswali mengi kuliko majibu.

Mukajanga alisema kwa jumla timu hiyo imebaini kuwa uhusiano kati ya viongozi wa mkoa, wakiwamo polisi na waandishi wa habari mkoani humo, haukuwa mzuri na uligubikwa na kutoaminiana kati ya pande mbili hizo tangu katika robo ya mwisho wa mwaka 2011.

Alisema kwa mfano, Novemba, mwaka jana, mwandishi wa ITV, Laurean Mkumbata, alipigwa na kamera yake ilivunjwa kwa makusudi na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) wa Iringa, Mohamed Semunyu, akiwa kazini.

Pia alisema waandishi wa habari wa mkoani humo walitendewa vibaya na viongozi wa mkoa wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mwishoni mwa Februari, mwaka jana.

Alisema katika ziara hiyo, waandishi walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala.

“Matokeo yake, Machi 6, 2012, viongozi wa polisi wa mkoa waliipatia Klabu ya Waandishi wa Habari ya Iringa (IPC) kibali cha kufanya maandamano ya amani kulalamikia kukua kwa mahusiano yasiyo mazuri kati ya waandishi wa habari na viongozi wa mkoa,” alisema Mukajanga.

Alisema mfululizo wa mahojiano na ushahidi mbalimbali kama vile video, picha za mgando na maelezo kutoka katika mikutano ya waandishi wa habari iliyofanyika Iringa, taarifa za vyombo vya habari na hati mbalimbali zilisaidia katika kufanikisha uchunguzi wa mauaji ya Mwangosi.

Mukajanga alisema kulikuwa na matukio yenye sura mbili tofauti katika siku ya mauaji ya Mwangosi, kwani ofisi mbili za Chadema zilifunguliwa siku hiyo katika muda wa dakika 30.

Alisema katika tukio la ufunguzi la kwanza, busara ilitawala baada ya kutokuwapo mkutano wa hadhara.

Lakini alisema katika kufungua tawi la pili la Chadema katika kijiji hicho, polisi walitumia nguvu ya ziada wakilenga waandishi wa Iringa na kuwaacha wenzao kutoka jijini Dar es Salaam.

Alisema marehemu Mwangosi alizingirwa na kupigwa na polisi wasiopungua saba na kuuawa wakati polisi mmoja mwandamizi alijeruhiwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye kurasa 29, mchakato wa uchunguzi huo ulihusisha mbinu za uchunguzi za kiuandishi wa habari, ambazo si za uchunguzi wa kipolisi na wa kimahakama.

Inaeleza kuwa metholoji za uchunguzi zilijumuisha mahojiano, kutembelea maeneo husika na uchambuzi mahsusi wa nyaraka kwa kuzingatia adidu za rejea zilizopo na kwamba, waandishi wa habari waliokuwapo Nyololo na, ambao hawakuwapo katika eneo la mauaji walitoa mchango muhimu.

Inataja vyanzo vya uchunguzi huo kuwa ni pamoja na mashahidi walioshuhudia katika kijiji hicho, wakiwamo watoto, pia habari zilizochapishwa katika vyombo vya habari kutokana na taarifa rasmi kuhusu janga hilo zilichambuliwa kwa umakini.

Pia inaeleza kuwa uchambuzi mpana kuhusu hali ya uhusiano wa uongozi wa Mkoa wa Iringa, ikiwamo polisi na wanahabari wa mkoa huo kabla ya mauaji ya Mwangosi, ulifanywa. 

Ripoti hiyo ilihitimisha kwa kusema kuwa mauaji ya Mwangosi mikononi mwa polisi wakati akiwa kazini ni tishio kwa uhuru wa habari na kwa hiyo timu ya uchunguzi haikubali kabisa suala la kukosea utambulisho wa mtu.

Inaeleza kuwa waandishi wanane waliokuwapo katika kijiji hicho walitambulika kwa urahisi, hasa kutokana na mambo kwenda salama, kwani walikuwa na kamera, vidaftari na kalamu na wengine kama siyo wote walikuwa wanafahamika sana na polisi wa Iringa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa imebainika wazi kwamba polisi walikuwa wanawawinda waandishi wa Iringa, ambao walikuwa wakiwajua na kwamba, mapambano ya Chadema na polisi katika kijiji hicho habari zake zilikusanywa na waandishi kutoka Dar es Salaam na kuhoji kwanini waliolengwa walikuwa waandishi wa Iringa katika ghasia hizo?

Mukajanga alisema ripoti hiyo itapelekwa kwenye Bodi ya MCT na baadaye Baraza hilo litashirikiana na Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Jukwaa la Wahariri kuweka utaratibu bora utakaowawezesha waandishi kufanya kazi zao katika mazingira hatari na yenye utata.

“Tutapata wataalamu duniani watakaokuja kuonyesha mbinu gani zitumike kufanya kazi katika mazingira hayo,” alisema Mukajanga.

Naye Mwenyekiti wa UTPC, Abubakar Karsan, alisema wako katika majadiliano na polisi juu ya jinsi waandishi watakavyokuwa wakifanya kazi na polisi.

Alisema kufikia jana walikuwa wameshakaa mara mbili jijini Dar es Salaam na mkoani Mwanza.

Pia alisema wameanzisha tuzo maalum ya Daudi Mwangosi na kwamba, kuna kamati inayoendelea kuratibu namna ya kuienzi familia ya marehemu Mwangosi.

Naye mwakilishi wa TEF, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la NIPASHE, Jesse Kwayu, akijibu swali katika mkutano huo alisema TEF haikukataa kuundwa kwa kamati ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, na wala haikumzuia Theophil Makunga, ila ndilo lilimteua kuwa mjumbe wa kamati hiyo.

“Sisi hatukuipinga Kamati ya Waziri, tulimteua Theophil Makunga, Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited ambaye ni mwanachama wa Jukwaa kutuwakilisha,” alisema.

Hata hivyo, Kwayu alisema walichopinga ni Waziri Nchimbi kuwa sehemu ya waandamanaji katika maandamano yaliyofanywa na waandishi wa habari kulaani mauaji yaliyofanywa dhidi ya Mwangosi.

PITOTI YA KAMATI YA NCHIMBI

Nayo ripoti ya kamati ya kuchunguza mauaji ya Mwangosi iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi, jana iliwekwa hadharani huku ikishindwa kubainisha mtu aliyehusika na mauaji hayo.

Katika ripoti hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo jana jijini Dar es Salaam, mbele ya waandishi wa habari, Jaji Stephen Ihema, ilishindwa kuweka bayana mtu aliyehusika moja kwa moja katika mauaji ya mwanahabari huyo.

Kamati hiyo katika uchunguzi wake iliwahoji watu mbalimbali, wakiwamo watendaji wa serikali hususan wa Kamati za Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa na ya Wilaya Mufindi, viongozi wa Jeshi la Polisi, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa madhehebu ya dini, waandishi wa habari na wananchi wa kawaida.

Katika uchunguzi huo, Kamati hiyo ilibaini kwamba mauaji ya Mwangosi yalitokea baada ya operesheni za Jeshi za Polisi kumalizika katika mkutano wa kisiasa uliotishwa na Chadema.

Jaji Ihema alisema ripoti ya Kamati hiyo ilibaini pia kuwapo haja ya kufanya mabadiliko ya kimfumo katika Jeshi la Polisi badala ya uliopo sasa ambao kwa maoni ya baadhi ya watu waliozungumza na Kamati ni wa kitaifa zaidi na kuacha serikali za mitaa bila ya wajibu wa kulinda usalama wa wananchi.

Alisema Kamati hiyo ilibaini kuwa vyombo vya dola vinatumia nguvu kubwa sana dhidi ya raia, jambo ambalo linapunguza imani ya jamii kwa vyombo hivyo hususan Jeshi la Polisi.

Mambo mengine yaliyobainika katika Kamati hiyo ni pamoja na kupungua kwa maadili na uzalendo miongoni mwa Watanzania kuanzia viongozi wa kisiasa hadi kwa wananchi hususan kwenye shughuli za kisiasa.

Mweyekiti huyo alibainisha kuwa maelezo yaliyotolewa na  Kamanda Kamuhanda, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Iringa na mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga ni kwamba mauaji hayo yalitokea baada ya operesheni ya polisi kumalizika.

Kamati imeeleza kuwa kitendo cha kutotii amri halali ya RPC Iringa aliyowaagiza wafuasi wa Chadema watawanyike kutoka kwenye eneo la ofisi ya kata ya chama hicho ilikuwa chanzo cha kutokea kwa vurugu hizo.

Alisema uchunguzi ulibanisha kwamba kulikuwa na mazingira yaliyosababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu iliyosababisha kifo cha Mwangosi na wengine kuumizwa.

“Baada ya zoezi hilo kukamilika askari Polisi walioshiriki kwenye operesheni waliamriwa kuingia katika magari tayari kwa kuondoka.

Wakati Askari wakipanda kwenye magari kishindo kikubwa kilitokea umbali wa zaidi ya mita 100 kutoka sehemu ambayo operesheni ilikuwa inafanyika na iligundulika kwamba kishindo kile kimesababisha kifo cha Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Maswali ya kujiuliza katika tukio la mauaji ni Je, kulikuwepo na uwiano unaolingana na tukio hili?, Je, Palikuwa na uhalali wa kutumia bomu la kishindo?, na Je, utumiaji wa bomu hilo ulikuwa na umuhimu?

Ripoti hiyo inasema kuwa kulingana na tukio lenyewe majibu ya maswali hayo ni kwamba hapakuwa na uwiano wa bomu na tukio la mauaji, kwa vile utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa nyuzi 45 na umbali mita 80 mpaka mita 100.

Kamati hiyo pia ilibainisha kuwa hapakuwa na uhalali wa kutumia bomu la kishindo kwani lengo la ulipuaji wake ni ili watu waogope na kukimbia na hata ingekuwa ukamataji, tayari askari Polisi wapatao sita walikuwepo eneo la tukio.
 
Kamati ilisema kuwa madai ya kuwapo uhasama kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa Mkoa wa Iringa na kuwapo kwa orodha ya waandishi watatu ambao Jeshi la Polisi limepanga kuwashughulikia ndicho chanzo cha kukua kwa uhasama.

Kamati iliongeza kuwa katika mkutano wake na waandishi wa habari, ilionekana kuwa katika thathmini yao uhusiano kati yao na Polisi hapo mkoani ni mbaya sana.

Kamati hiyo imebainisha kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ana mawasiliano duni na waandishi wa habari na juhudi za wengi wao kumfuata ili athibitishe tukio zimekuwa zikishindwa kwani ameweka maagizo getini kuwa mtu yeyote ambaye anataka kumuona ni lazima aeleze anataka kumuona kwa sababu gani ndipo aruhusiwe kuingia.

Kamati hiyo katika mahojiana na wanahabari imebaini kuwa uhusiano wao na Polisi ulikuwa mzuri kipindi cha uongozi wa RPC Advocate Nyombi, lakini ulianza kuharibika alipohama na nafasi yake kuchukuliwa na RPC  Evarist Mangalla na kuwa mbaya zaidi alipokuja Kamuhanda.

Ripoti ya Kamati hiyo kadhalika inasema kuwa waandishi wa habari mkoani Iringa walionyesha masikitiko yao kuwa tangu kutokee kwa mauji ya Mwangosi, hawajapokea pole kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na watendaji wake wa juu hata kama ni ya “kinafiki”.

Ripoti inaeleza: “Baada ya kuongea na pande hizo mbili, Kamati imebaini kwamba kuna walakini wa mahusiano kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari polisi mkoani Iringa.

Kuhusu madai ya kuwepo kwa orodha ya waandishi watatu (3) ambao jeshi la polisi limepanga kuwashughulikia.”

Kwa mujibu wa Kamati ya Dk. Nchimbi, kwenye tukio la Nyololo ambalo Mwangosi aliuawa, mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE, Godfrey Mushi, alipigwa na Polisi na kujeruhiwa vibaya na baadaye kukamatwa na Polisi.

Ripoti inaongeza kuwa katika mahojiano na kamati, mwandishi wa habari wa Tanzania Daima, Joseph Senga, alisema alimwona mtu amezungukwa na askari akipigwa, lakini hakujua ni nani na yeye aliendelea kupiga picha tukio hilo mpaka naye alipokamatwa na Polisi watatu ambao walimuuliza kama naye anataka aende kuungana na mtu aliyekuwa akipigwa.

Taarifa inasema kuwa Senga alisema wakati kipigo kinaendelea, kuna askari mmoja mwenye nyota tatu (OCS Mwampamba) aliteremka kutoka kwenye gari na kwenda pale ambako mtu aliyekuwa anapigwa huku akiwaambia “mwachieni, mwachieni, namfahamu mimi huyo ni mwandishi wa habari!”

Senga alisema kuwa mara alisikia kishindo kikubwa na wale askari ambao walikuwa wanamshikilia walikimbia ndipo yeye akaendelea kupiga picha za marehemu Daud Mwangosi ambaye alikuwa amekwisha sambaratishwa na bomu.

 SENGA, RPC WATOFAUTIANA

 Kamati hiyo imebainisha kuwa maelezo ya Senga yanatofautiana sana na yale yaliyotolewa na RPC na OC FFU kuwa marehemu alimvamia OCS Mwampamba na kuwa wale askari huenda walidhania kuwa mkubwa wao alikuwa amevamiwa ndipo walipoamua kwenda kumsaidia.

“Kwa minajili hii basi Kamati imeshindwa kubaini baada ya kumalizika operesheni na askari Polisi kuanza kuondoka, kwa nini Mwangosi alishambuliwa kwa kipigo kabla ya kulipuliwa na bomu la kishindo?. Kwa nini kuna maelezo yanayokinzana kati ya Senga ambaye alikuwa karibu sana na tukio na yale ya RPC na OC-FFU ambao katika maelezo yao kwa Kamati walisema kuwa wao walikuwa mbali kidogo na tukio kwa hiyo hawakuweza kuona kwa dhahiri kilichotokea.

Jaji Ihema alisema uchunguzi wa Kamati haukuweza kupata ushahidi wa kubainisha kama kupigwa kwa waandishi hao kulitokana na njama yeyote ya Polisi kuwashughulikia au ilitokea kwenye purukushani ya vurugu zilizotokea baada ya FFU kuamriwa kutawanya wanachama wa Chadema.

Pia kamati haikupata ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa mauaji ya Mwangosi yalikuwa ni ya kupangwa.

MAPENDEKEZO YA KAMATI

Kamati hiyo imependekeza kuwa taasisi za habari zinazosimamia maadili na weledi wa vyombo vya habari, hususan Baraza la Habari Tanzania na Jukwaa la Wahariri wafanye utaratibu unaostahiki za upatanishi kati ya waandishi wa habari, Jeshi la Polisi na uongozi wa mkoa wa Iringa.

Waandishi wa habari wavae mavazi maalum ya kuwatambulisha wakiwa katika matukio hasa kwenye maeneo hatarishi.

Waandishi wa habari wafanye kazi kwa weledi, uadilifu, uwazi na wasijibainishe na vyama vya siasa; Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Mwangosi kabla hajauawa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria na Kamati ya Ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari liyoanzishwa mwaka 2008 ifufuliwe.

Kuwe na jukwaa la mazungumzo ya mara kwa mara kati ya Jeshi la Polisi na vyama vya siasa ili kila upande ujue wajibu wake na wa taasisi nyingine katika kudumisha amani ya nchi na utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopo na kupunguza migongano.


No comments:

Post a Comment