Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Friday, October 5, 2012

WALIOFUTIWA MATOKEO KIDATO CHA NNE WARUDIA MITIHANI

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo

Zaidi ya watahiniwa 3, 303 waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, wataruhusiwa kufanya mtihani mwingine wa ngazi hiyo mwakani kama watahiniwa wa kujitegemea.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema watahiniwa hao wameruhusiwa kufanya mtihani huo baada ya kuomba msamaha pamoja na kutumikia adhabu ya miaka miwili tangu kufutiwa kwa matokeo yao mwaka jana hadi mwaka ujao 2013.

Hata hivyo, aliwaonya watakaobainika kufanya udanganyifu kwa mwaka huu kwamba, adhabu haitapunguzwa.

“Kuhusu watahiniwa waliofutiwa matokeo, baada ya kuomba msamaha, wamepunguziwa adhabu na wataruhusiwa kufanya mtihani mwaka 2013 kama watahiniwa wa kujitegemea baada ya kutumikia adhabu kwa muda wa miaka miwili,” alisema Mulugo na kuongeza:

“Ninatoa wito kwa walimu, viongozi na wazazi kuwaasa watahiniwa kuhusu suala la udanganyifu kwani mwaka huu adhabu haitapunguzwa.”

Watahiniwa hao walifutiwa matokeo yao ya kidato cha nne mwaka jana kutokana na kuhusishwa na udanganyifu katika mtihani huo.

Sanjari na hilo, idadi ya watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani wa kidato cha nne Oktoba, mwaka huu, imeongezeka hadi kufikia 481, 414 kutoka 450, 324 waliofanya mtihani huo mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 6.90.

Watahiniwa wanaotarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka huu wamegawanyika katika makundi matatu, ikiwa ni pamoja na watahiniwa wa shule (school candidates) 412, 594, wakiwamo wavulana 228, 991 na wasichana 183, 603, ambapo idadi hiyo imeongezeka kutoka 349, 390 mwaka 2011.

Kundi la pili ni la watahiniwa wa kujitegemea (private candidates), ambapo idadi imepungua kutoka 100, 934 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana hadi 68, 820 mwaka huu, wakiwamo wavulana 34, 211 na wasichana 34, 609 sawa na upungufu wa asilimia 31.82.

Watahiniwa waliobaki ni wale wa mtihani wa maarifa (gualifying test), ambao pia idadi ya waliojiandikisha kufanya mtihani huo mwaka huu imepungua kutoka 29, 447 mwaka jana hadi 21, 314, wakiwamo wanaume 8, 174 na wasichana 13, 140.

Kwa mujibu wa Mulugo, idadi ya shule zilizoandikisha watahiniwa wa shule ni 4, 155 na  vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 902, huku vituo 616 vikiwa ni kwa ajili ya watahiniwa wa maarifa.

Mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, unatarajia kuanza Jumatatu Oktoba 8 hadi 25 kwa watahiniwa wa shule na wa kujitegemea, huku wa mtihani wa maarifa ukitarajiwa kufanywa Oktoba 16.

Aidha, wanafunzi waliochaguliwa awamu ya pili kujiunga na vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na stashahada, wametakiwa kuripoti vyuoni mwao ifikapo Jumapili, Oktoba 14, mwaka huu.

Mulugo aliwahakikishia Watanzania kuwa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu haujavuja, kuanzia Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), mikoani na halmashauri na kuwasisitiza kuwachukulia hatua za kinidhamu wale wote watakaobainika kufanya udanganyifu.

No comments:

Post a Comment