WATOTO wanaoishi katika mazingira magumu na kulelewa
katika vituo maalumu, wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwaondoa
watoto wenzao wanaoishi magerezani na mama zao bila hatia ,kwani licha ya kuteseka na hali
mbaya ya mazingira iliyopo gerezani, wanakosa mahitaji ya msingi yanayostahili kwa
mtoto.
Aidha wamedai kuwa kitendo cha watoto hao kuendelea
kuishi gerezani ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu kwa kuwa hawana
hatia yoyote badala yake wameililia serikali iwatoe na kuwakabidhi kwenye vituo
vya kulelea watoto.
Watoto hao walitoa kilio chao mbele ya mkuu wa mkoa
wa Arusha ,Magesa Mulongo aliyekuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia
ujenzi wa madarasa mawili katika kituo
cha St.Gemma kilichopo kisongo jijini hapa, ambacho ni kituo pekee Tanzania
kinacholea watoto waliopo gerezani ambao mama zao walifungwa.
Wakisoma risara yao iliowasisimua wageni
mbalimbali waliohudhulia hafla hiyo huku baadhi yao kujikuta wakibubujikwa na machozi
akiwemo mkuu huyo wa mkoa,watoto hao wenye umri mdogo walisema kuwa kitendo cha
wenzao kukaa gerezani kama wafungwa ni kuwanyima uhuru wa kuishi kwani hawana
hatia wenye hatia ni wazazi ama walezi wao.
Walisema ni vizuri serikali ikatafakari upya na
kuona umuhimu wa kuwaondoa watoto hao waliopo magerezani ili waungane na wenzao waliopo uraiani na kuondoka na mateso
wanayoyapata bila hatia ikiwemo kuathirika kisaikolojia na kukosa elimu.
‘’kwanini serikali inatufunga gerezani kwani
tumekosa nini kama ni kosa la wazazi wetu sisi tunafanya nini gerezani ,watoto
wanashindwa kusoma ,kula vizuri na kucheza na wenzao tunaomba wenzetu watolewe
gerezani’’walisema.
Naye meneja wa kituo hicho,Flora Ndwata alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa
na watoto watatu , hadi sasa kina jumla ya watoto 14 wenye umri wa miaka mitatu
hadi 10 na kwamba kimeshindwa kuchukuwa watoto wengi kwa sababu ya kukosa fedha za
kujiendeshea.
Alisema
kituo hicho kilibuniwa na masister wa kanisa
katoliki,shirika la St Gemme baada ya masister hao kuguswa na hali za
mbaya za watoto hao waliopo magerezani na kuamua kuanzisha mkakati wa
kuwasaidia kwa kuwaondoa kwa wazazi wao waliopo gerezani.
Alisema hatua hiyo iliwafanya wachangishane na
kuamua kujenga vyumba viwili ambapo walifanikiwa kuwa na watoto wawili ambao
walimudu kuwalea na baadae watu mbalimbali waliwaunga mkono kwa kuwasaidai
michango iliyosaidia kuongezeka kwa watoto hao.
''tumekuwa
tukiwauliza wamewapataje watoto hao wanasema wengine waliingia gerezani
wakiwa na ujauzito na wengine walisema walipata ujauzito wakiwa huko na
kujifungua''alisema Sister Flora
Aliongeza kuwa hadi sasa wana watoto kutoka gereza
kuu la Isanga Dodoma,gereza la Babati na gereza kuu la Kisongo jijini hapa na
kwamba wanatarajia kuomba watoto wengine kadri wanapo kuwa na uwezo wa
kuwahudumia.
Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo
ambaye alikuwa mgeni rasimi kwanye harambee hiyo ya kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya
madarasa,alifanikiwa kuchangisha shilingi milioni 63.3 na kuvuka malengo ya
shilingi milioni 46 zilizokuwa zikihitajika,huku ofisi yake ikichangia shilingi
milioni 10.
Wengine
waliochangia ni pamoja na mkuu wa wilaya ya Arusha,John Mongela ambaye
alichangia shilingi milioni 1pamoja na malori 9 ya mchanga na kokoto,kaimu
mkurugenzi jiji la Arusha,Omari Mkombole shilingi milioni 10.3,Mkurugenzi Rich
Hotel Joseph Masawe shilingi milioni 2.5.
No comments:
Post a Comment