Sakata la
mfungwa aliyekutwa uraiani akiwa na bunduki na risasi, limeingia katika
hatua mpya baada ya Jeshi la Polisi na Magereza kutoa kauli
zinazokinzana.Jeshi
la Polisi mkoani Simiyu limeendelea kuthibitisha kuwa mtuhumiwa
aliyekamatwa nyumbani kwake Novemba 16, mwaka huu akiwa na bunduki aina
ya Sub Machine Gun (SMG), risasi 31 na magazini tatu, Masanja Maguzu
(42), ni mfungwa ambaye hajamaliza kutumikia kifungo cha miaka 15 jela
na kuwa alitoka gerezani katika mazingira ya kutatanisha.
Wakati Jeshi la polisi likisisitiza hivyo, Jeshi la Magereza limetoa taarifa inayoeleza kuwa mtu huyo alishamaliza kifungo.
Kamanda wa
Polisi mkoani Simiyu, Salum Msangi, amekanusha madai ya Jeshi la
Magereza kwamba mfungwa huyo alishamaliza kutumikia adhabu yake ya
kifungo cha miaka mitano jela na kwamba hata kama alikuwa akitumikia
adhabu ya miaka mitano muda huo bado haujatimia.
Kamanda huyo
alifafanua jana kuwa hata kama kuna tetesi za mfungwa huyo kuachiwa kwa
msamaha wa Rais, makosa yaliyompeleka gerezani kwa mujibu wa Sheria ya
Msamaha hayana msamaha.
Alisema
mfungwa huyo alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela mwaka 2010 baada ya
yeye na mwenzake, Japhet Sylivester, kupatikana na hatia ya kukamatwa na
SMG, risasi 622 na nyara za serikali (nyama ya nyati) akiwa ndani ya
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).
Kamanda
Msangi aliiambia NIPASHE kwa njia ya simu kuwa leo atatoa taarifa kamili
ya jinsi mfungwa huyo alivyotoka gerezani baada ya Jeshi la Polisi
kufanya uchunguzi wa kina na kubaini ukweli wa mazingira yaliyosababisha
kuwa uraiani.
Alifafanua
kuwa wafungwa hao walikuwa wakiitumia bunduki hiyo kufanyia vitendo vya
uhalifu ukiwamo ujambazi na ujangili na siku hiyo walikamatwa nayo ndani
ya hifadhi hiyo na risasi 74 na baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi na
wa wanyamapori aliwapeleka nyumbani kwake kuwaonyesha alipokuwa
ameficha nyingine 548.
Alidai kuwa
wafungwa hao walikamatwa katika msako wa pamoja wa kukabiliana na
vitendo vya uhalifu na kukabiliana na ujangili uliokuwa ukiendeshwa kwa
pamoja kati ya askari wa Jeshi la Polisi na Wanyamapori mkoani Shinyanga
kwa wakati huo.
Alisema
baada ya kufunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani
Shinyanga, watuhumiwa hao walipatikana na hatia na hivyo kuhukumiwa
kutumikia kifungo cha miaka 15 jela kila mmoja.
“Kesho
(leo), nitatoa picha kamili ya jinsi mfungwa huyo alivyotoroka gerezani
na kumuacha mwenzake waliyehukumiwa naye kifungo, hii ni baada ya
kufanya uchunguzi wetu wa kina na kumhoji mfungwa mwenyewe na kubaini
mambo kadha wa kadha yaliyosababisha yeye kuwa uraiani na kuendelea
kufanya vitendo vya uhalifu na ujangili kwa kutumia silaha za kivita,”
alisema.
Kwa mujibu
wa Kamanda Msangi, wafungwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya
uhujumu uchumi ambayo ni kupatikana na bunduki, risasi, nyara za
serikali na kuingia na kuwinda ndani ya hifadhi bila kibali na baada ya
kupatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda gerezani, hayawezi kutolewa
msamaha.
“Watuhumiwa
hawa walipatikana na makosa ya kupatikana na bunduki ya kivita,
kupatikana na risasi, kupatikana na nyara za serikali na kuingia kuwinda
ndani ya hifadhi na kuwinda bila kibali nyume cha sheria makosa yote
haya yanaangukia kwenye makosa ya uhujumu uchumi ambayo hayana msamaha
kisheria,” aliongeza.
Alisema siku
10 kabla ya kumkamata mfungwa huyo akiwa uraiani na SMG hiyo, risasi 31
na magazini tatu, moja hutumika katika bunduki aina ya Uzi gun ya
Kiisraeli, jeshi hilo lilikuwa limemkamata mke wake, Holo Mabuga (30),
akiwa na bunduki ya kivita aina ya G3, risasi zake 36 pamoja na risasi
nyingine zinazotumika kwenye bunduki aina ya SMG inayodaiwa pia kutumika
katika matukio mbalimbali ya kihalifu na ujangili katika Senapa na Pori
la Akiba la Maswa.
TAARIFA YA MAGEREZA
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Kaimu Kamishna wa
Magereza, Deonice Chamulesile, ilisema Maguzu alikuwa anatumikia kifungo
cha miaka mitano, lakini Aprili 26, mwaka huu alikuwa ameachiliwa.
“Mfungwa
aliyekuwa na Namba 250/2010, Masanja Maguzu, alipokelewa Gereza la
Wilaya ya Shinyanga tarehe 3 Novemba, 2010 baada ya kuhukumiwa na
Mahakama ya wilaya hiyo kwa makosa mbalimbali ya uhujumu uchumi,”
alisema.
Aliongeza:
“Alianza kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kuanzia Novemba 3,
2010 na kufikia Aprili 26, 2012 aliachiliwa baada ya kutimiza masharti
ya kifungo na kutoka gerezani kwa mujibu wa sheria, hivyo ifahamike
kwamba hakutoka katika mazingira ya utata kama ilivyoripotiwa kwenye
vyombo vya habari.”
Taarifa hiyo
iliyataja makosa aliyohukumiwa kuwa ni kuingia kinyume cha sheria
katika hifadhi, kuwinda kunyume cha sheria na kumiliki kinyume cha
sheria nyara za serikali.
Taarifa hiyo
ya Chamulesile ilieleza kuwa katika kosa la kwanza, Maguzu alihukumiwa
miaka miwili jela, kosa la pili miaka mitano jela na la tatu miaka
mitano jela.
Alisema hukumu iliyotolewa iliamuru adhabu hizo zitumikiwe kwa pamoja kwa kufungwa miaka mitano jela.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment