
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Waziri
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameahidi kuwachukulia hatua kali
za kisheria ikiwamo kuwapeleka jela wanaoendeleza vitendo vya hujuma
katika Bandari ya Dar es Salaam na hivyo kudhoofisha ufanisi wa
kiutendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Waziri Mwakyembe alisema ni dhahiri kuwa
baadhi ya watendaji wamekuwa na mazoea ya kusimamishwa kazi mara
wanapofanya makosa, hatua ambayo alisema haijawa fundisho la kukomesha
vitendoi hivyo.
Alisema mara atakapothibitisha ukweli wa
watu hao kuhusika na hujuma hizo, sheria itafuata mkondo wake ili iwe
fundisho kwa wengine.
Aliyasema hayo jana jijini Tanga alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Uchukuzi.
Alisema uko mtandao wa wizi na ubabaishaji uliojengeka miongoni mwa watendaji wa taasisi zote za Wizara hiyo.
“Nimesikia kupitia Gazeti la NIPASHE kuwa
kuna hujuma katika Bandari ya Dar es Salaam, bado sijasoma habari hizo
kiundani zaidi, lakini nitakapozisoma na kubaini kuwepo kwa hujuma kweli
nitawapeleka jela kwa sababu ni bora kufanya maamuzi magumu, lakini
kazi ziende kuliko kulea wahalifu wachache,” alisema.
Alisema siyo rahisi kuimarisha na
kuboresha huduma za usafiri iwapo kuna mwendelezo wa vitendo vya
ukiritimba, wizi na ufisadi miongoni mwa wafanyakazi wa Wizara hiyo
ambao muda wote wanawaza kudhoofisha utendaji wa serikali.
Alisema inasikitisha kuona TPA
inaposhindwa kusimamia kikamilifu bandari zake na hivyo kudhoofisha
uchumi wa nchi kwa kushindwa kuchangia katika Pato la Taifa.
Alisema: “Sitaogopa mtu hata kama ana
fedha nyingi, lakini kwa sababu fedha hizo ni za wizi nitamnyofoa tu
kikubwa ni kwamba nitasimamia haki.”
Alisema kutokana na hujuma na wizi
unaofanywa katika bandari mapato yanayopatikana hayaongezeki na kwamba
kiasi kinachokusanywa kwa mwezi ni Sh. bilioni 32 tu ukilinganisha na
Bandari ya Mombasa ambayo mapato yake ni zaidi ya bilioni 200 kwa mwezi.
Alilitaka Baraza hilo kuimarisha nidhamu,
uadilifu, uaminifu na uzalendo nahali pa kazi kwa lengo la kuhakikisha
kuwa sekta ya uchukuzi inapiga hatua katika kukuza uchumi wa nchi.
Dk. Mwakyembe alisema wakati umefika kwa
kila mmoja kuhakikisha kuwa anatimiza wajibu wake na akishindwa
ajiachishe kazi yeye mwenyewe.
Jana katika hili toleo la jana kulikuwa na habari kuhusu hujuma ambazo zinazodhoofisha ufanisi wa utendaji katika TPA.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment