Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, November 5, 2012

Watakaofeli kidato cha pili mara mbili kutimuliwa..!

Wakati Mitihani ya Taifa kidato cha pili ikianza leo nchini kote, serikali imetoa tamko ikisisitiza kuwa mwanafunzi atakayeshindwa mara kwanza atapewa fursa nyingine mwaka unafuata na baada ya hapo akishindwa kupata alama zinazotakiwa, atatimuliwa shule na kwenda kusoma elimu isiyokuwa rasmi.

Tamko hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuongeza kuwa mitihani hiyo itaanza leo hadi Novemba 16, mwaka huu.

Dk. Kawambwa alisema ili mwanafunzi aweze kuingia kidato cha tatu, anatakiwa kufaulu mitihani ya kidato cha pili, na akishindwa ataruhusiwa kurudia mara moja na baada ya hapo atatimuliwa moja kwa moja katika mfumo rasmi.

“Mwanafunzi ataruhusiwa kukariri  (kurudia), mitihani yake ya kidato cha pili mara moja tu na endapo atashindwa kwa mara ya pili, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi,” alisema Dk. Kawambwa.

Dk. Kawambwa alisema mwaka huu vituo/shule 4,242 (sawa na ongezeko la asilimia 1.3) vitatumika ikilinganishwa na 4,187 vilivyotumika mwaka jana kuwatahini wanafunzi 442,925.

Alifafanua kuwa kati ya wanafunzi hao,  214,325  ni wasichana (sawa na asilimia 48.39), na 228,600 (sawa na asilimia 51.61) wakiwa ni wavulana wataingia katika vyumba vya mitihani kuanzia leo ili kufanya mitihani hiyo ya kidato cha pili.

Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mitihani ya kidato cha pili ni muhimu kwa kuwa matokeo yake hutumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) wakati wa kupanga matokeo ya mitihani ya kidato cha nne.

Aliwataka wadau wa elimu na wazazi kuhakikisha wanafunzi wotewa kidato cha pili walioandikishwa kufanya mitihani kwa nchi nzima wanaifanya bila kukosa.

Ili mwanafunzi ahesabike kama amefaulu mitihani ya kidato cha pili, atatakiwa kuwa amepata alama kuanzia wastani wa kuanzia 30 na atakayepata chini ya hapo, atalazimika kurudia mitihani na fursa hiyo itatolewa mara moja.

“Mwanafunzi atakayekariri (kurudia) kidato cha pili na kushindwa kufikia wastani wa asilimia 30 ataondolewa katika mfumo rasmi wa elimu,” alisema Dk. Kawambwa.

Pamoja na msimamo huo wa serikali, wadau wa elimu siku za nyuma wamekuwa na maoni tofauti juu ya uamuzi huo wa serikali, huku baadhi wakisema umejaa kasoro mbalimbali.

Walisema kuwa ingekuwa vema mtoto kurudia darasa pale anaposhindwa mtihani, lakini siyo kufukuzwa shule kwa sababu amerudia mara mbili na kufeli.

Walisema watoto hao bado ni wadogo na kwamba siyo vizuri kufukuzwa shule, lakini wakiwa wanarudia darasa, itawasaidia kujitahidi na kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Kwa kawaida watoto wadogo hawasomi kwa malengo kama watu ambao wapo vyuoni, kwa hiyo ili kuhakikisha hawa watoto wanasoma, lazima kuwe na sababu ya kuwafanya wapende ama walazimike kusoma,” alisema mmoja wa wadau hao.

Wanasema kufanya hivyo ni sawa na kuwatupa wanafunzi hao nje ya mfumo wa elimu na kwamba  serikali inawakaanga kabisa na badala yake ingeangalia uwezekano wa kuwasaidia katika vyuo vya ufundi.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment