Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, November 5, 2012

Mkurugenzi Halmashauri Mpwapwa asimamishwa kazi..!

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma limemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Fanuel Senge, kwa tuhuma mbalimbali, ikiwamo kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Hatua hiyo imechukuliwa na baraza hilo katika kikao chake baada ya mkurugenzi huyo kukutwa na makosa ya kushidwa kukusanya mapato ya halmashauri, kusimamia watendaji wake wa ngazi ya chini kuhusu utaratibu wa mapato na matumizi ya halmashauri.

Diwani wa Kata ya Chunyu, Nehemia Kongawadodo, alisema kuna baadhi wa watendaji wa halmashauri hiyo  wameigeuza halmashauri kuwa sehemu ya kutajirika mithili ya ‘shamba la bibi’.

Alisema mkurugenzi huyo amekuwa akipelekewa taarifa za ubadhirifu wa watendaji hao, lakini amekuwa akishindwa kuwachukulia hatua za kinidhamu.

Kongawadodo alisema halmashauri hiyo ina utaratibu wa kukusanya fedha kwa ajili ya Mfuko wa Elimu, ambapo kila kaya hutoa Sh. 5,000, lakini watendaji hao hawazirejeshi kwenye akaunti za kata kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa.

Pia ilidaiwa na madiwani hao kuwa kumekuwa na matumizi mabaya ya Sh. mil. 26.2, ambapo taarifa zinadai kuwa fedha hizo zilitumika kwenye mitihani ya moko ya elimu ya msingi kwa usimamizi na kusahihisha mitihani hiyo.

Walisema katika matumizi ya moko, mzazi alichangisha Sh. 1,000 kwa ajili ya matumizi ya mtihani huo na kuhoji: “Iiweje leo waambiwe fedha hizo zilitumika katika mtihani wa moko?”.

Kutokana na tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Alexander Nyaulingo, alitangaza mkurugenzi huyo kusimamishwa kazi, ikiwa ni pamoja na wakuu wa idara wa halmashauri hiyo kuamriwa waandikiwe barua za onyo.

Awali, madiwani hao walivikataa vikao viwili vya nyuma kutokana na mkurugenzi huyo kushindwa kuandaa vikao hivyo kwa taratibu zinavyosema, ikiwamo madiwani kutopata makabrasha kwa wakati na kushindwa kuandika taarifa za kamati.

Akizungumza na NIPASHE, mkurugenzi huyo, alisema baraza hilo halina mamlaka ya kumsimamisha kazi.

Alisema hawezi kuzungumzia chochote kuhusu tuhuma hizo kwani yeye alikuwa safarini jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa amepeleka matokeo ya uchaguzi mdogo wa Diwani wa Kata ya Mpwapwa Mjini.

“Hawana mamlaka ya kunisimamisha kazi...kwanza katika kikao hicho mi sikuwapo. Nilikuwa Dar es Salaam kupeleka matokeo Tume ya Uchaguzi ya uchaguzi mdogo. Hivyo, sijui chochote na siwezi kuzungumza,” alisema na kuongeza:

“Wewe si ulikuwapo? Mimi sijui chochote hadi nirudi nielezwe, ndiyo nitaweza kukujibu.”

Mkurugenzi huyo amekuwapo katika halmashauri hiyo kwa miezi mitatu akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Halmashauri ya Tabora.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment