Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, December 12, 2012

Watu 25 mbaroni mkoani Singida kufuatia tukio la kupora fedha katika gari iliyokuwa imebeba maiti...!

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Linus Sinzumwa akionyesha silaha za jadi zilizokuwa zinatumiwa na majambazi yaliyoteka gari la SUA no.SU 37012 na kuporwa zaidi ya shilingi 19.8 miloni na mali mbali mbali nje kidogo ya mji wa Singida.(Picha na Nathaniel Limu).

Na Nathaniel Limu
       Jeshi la polisi mkoani Sngida limefanikiwa kuwakamata watu 25 wanaotuhumiwa kuteka gari la Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro na kisha kupora watu waliokuwa wanasindikiza maiti kupeleka mkoani Mara kwa ajili ya mazishi.
      Gari lililotekwa ni Land Cruiser SU 37012 lililokuwa likiendeshwa na Kalistus Mapulila.
     Katika utekaji huo, inadawa kuwa jeneza lililokuwa limebeba mwili wa marehemu Munchari Lyoba mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha SUA, lilifumuliwa na mwili wa marehemu ukasachiwa.
       Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa, amesema kwa sasa majina ya watuhumiwa hao hayawezi kutangazwa hadharani kwa madai kuwa kitendo hicho kinaweza kuathiri shughuli za upelelezi ambao bado unaendelea.
      Amesema watuhumiwa wengi ni wakazi wa kijiji cha Kisaki kilichopo katika manispaa ya Singida.
      Kamanda huyo amesema katika msako huo mkali ambao bado unaendelea, mbali na kukamatwa kwa watuhumiwa hao, pia baadhi ya mali iliyoporwa ikiwemo nguo za waathirika, kamera, laptop na simu, zimekamatwa.
      Ametaja vitu vingine vilivyokamatwa ni pamoja na vitambulisho vya kazi, charger mbili za simu, kadi aina ya tembo kadi na shilingi 20,500 zizookotwa eneo la tukio.
      Amesema mafanikio hayo makubwa yamechangiwa na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ambao ulipelekea kazi ya kukamata watuhumiwa,kuwa rahisi na nyepesi.
     Kamanda Sinzumwa ameongeza kuwa baadhi ya watuhumiwa baada ya kugawana shilingi milioni 19.8 walizopora, walianza kunywa pombe ovyo huku wakijitapa kuwa wana uwezo mzuri wa kiuchumi.
       Kamanda ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ambao utasaidia mkoa wa Singida kuendelea kuwa eneo lenye utulivu na amani wakati wote.
       Aidha, ameitaka TANROADS mkoa wa Singida kufanya juhudi za makusudi kuondoa mawe mengi makubwa yalioko kandokando ya barabara ambayo majambazi wanayatumia katika azma yao ya kuteka magari.
       Wakati huo huo, Kamanda huyo amewahakikishia wakazi wa mkoa wa Singida, kuwa kipindi chote cha kuelekea siku kuu za Xmas na mwaka mpya, kutakuwa na amani na utulivu wa hali ya juu.

No comments:

Post a Comment