Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Wednesday, January 9, 2013

ALIYEKAMATWA KUMTEKA DR.ULIMBOKA AGOMA KULA, ULIMBOKA AFUNGUKA YA MOYONI ...!

RAIA wa Kenya, Joshua Mulundi, anayekabiliwa na kesi ya kumteka na kutaka kumsababishia kifo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini, Dkt. Ulimboka Stephen, ameanza mgomo wa kula na ameamua kuishi juu ya paa la Gereza la Keko akitishia kutaka kujiua.

Mtuhumiwa huyo ambaye Jumapili iliyopita kupitia chanzo chetu makini alitoboa siri ya jinsi alivyokamatwa na kutoa kauli nzito kulalamikia mwenendo wa kesi yake, amefikia hatua hiyo kwa lengo la kuishinikiza serikali imlete mbele yake Dkt. Ulimboka ili afanyiwe gwaride la utambulisho kubaini kama alihusika katika tukio la kumteka.

Akizungumza na chanzo chetu akiwa ndani ya Gereza la Keko, Joshua alisema kuanzia jana alitarajia kuanza mgomo wa kutokula na atakuwa akiishi juu ya paa la gereza hilo kwa lengo la kuishinikiza serikali ikamilishe uchunguzi wa kesi yake.

Habari kutoka ndani ya Gereza la Keko ambako mtuhumiwa huyo amehifadhiwa, zilisema kuwa raia huyo wa Kenya ameanza mgomo jana. Imeelezwa kuwa amechukua uamuzi huo mgumu baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa kesi ambayo tangu Julai 3, mwaka jana bado iko kwenye hatua ya upelelezi na hajui utakamilika lini.

Askari mmoja wa Jeshi la Magereza kutoka ndani ya gereza hilo alikiri kuwa mtuhumiwa huyo amegoma na usiku wa kuamkia jana alishinda juu ya paa la gereza huku mvua ikimnyeshea, “Ni kweli huyo bwana amegoma, uongozi wa gereza umefanya juhudi za kuzungumza naye na kilio chake anasema anataka upelelezi wa kesi yake ukamilike haraka ili atendewe haki, lakini kubwa kuliko yote, ameitaka serikali imlete Dkt. Ulimboka mahakamani ili aweze kumtambua,” alisema askari huyo.

Habari zaidi zinasema kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambaye hana wakili mahakamani, wamewasili kutoka nchini Kenya kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria.

Kwa mujibu wa ndugu hao, hadi sasa hawaoni maendeleo ya kesi hiyo kwani kila ikifika mahakamani upande wa mashitaka hutoa hoja ya kutaka iahirishwe kwa madai kuwa upelelezi haujakamilika.

Juzi mtuhumiwa wa kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini aliliambia gazeti hili kuwa amepata kutoa malalamiko kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), akiiomba serikali imlete mbele yake, Dkt. Ulimboka ili amtambue na kuhakikisha upelelezi wa kesi hiyo unafikia tamati.

Mbali ya maombi hayo, mtuhumiwa huyo pia alisema aliwaomba viongozi hao wamsaidie kupata dhamana kwani kesi inayomkabili inaruhusu dhamana na hana wakili wa kumtetea.

Dkt. Ulimboka ajipa muda

Wakati Joshua akitaka afanyiwe gwaride la utambulisho, kwa upande wake Dkt. Ulimboka alisema kwa sasa hana cha kusema, lakini muda ukifika atasema ukweli wote.

Alisema hajawahi kuitwa na kukutanishwa na mtuhumiwa wa kesi hiyo wala hajaombwa kuwa mmoja wa mashahidi, ingawa anajua atatakiwa kwenye ushahidi, “Mimi sina la kusema kwa sasa, naviachia vyombo husika kufanya kazi yao, lakini muda ukifika naweza kusema lolote, ila kwa sasa tuviachie vyombo vya dola,” alisema Dkt. Ulimboka.

Magereza wang’aka
Kwa upande wake, Jeshi la Magereza nchini limegoma kuzungumzia mgomo wa mahabusu huyo na hatua anazochukua gerezani kushinikiza kesi yake iendeshwe haraka.

Msemaji wa jeshi hilo, Danstan Lissu, alipoulizwa na gazeti hili alikuwa mbogo na kuhoji gazeti hili limepataje taarifa za mgomo wa mahabusu huyo, “Taarifa hizi umepata wapi? Nani amekuambia? Siwezi kulizungumzia suala hilo kwa vile sijaruhusiwa, mtafute Kamishna Mkuu wa Magereza akupe taarifa hiyo,” alisema Lissu.

Hata hivyo chanzo chetu Jumatano ilipomtafuta Kamishna Mkuu wa Magereza, John Minja, kupata taarifa juu ya mahabusu huyo hakuweza kupatikana na simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila majibu.

Dkt. Ulimboka ambaye alikuwa kinara wa mgomo wa madaktari uliotikisa nchini kwa wakati tofauti mwaka jana; alitekwa, kuteswa, kupigwa hadi kung’olewa meno na kucha na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.


Chanzo: Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment