Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Thursday, February 14, 2013

LOWASSA AWATAKA VIONGOZI WA DINI KUREJESHA AMANI KATI YA WAISLAMU NA WAKRISTO


WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, amewataka viongozi wa dini nchini kusaidia kurejesha hali ya amani kati ya Waislamu na Wakristo ambayo inaonekana inaanza kupotea.

Akizungumza nyumbani kwake Monduli, wakati akipokea ujumbe kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria, Lowassa alisema vurugu na mauaji yaliyotokea huko Buseresere mkoni Geita yanasikitisha sana na kuongeza kuwa ni dalili mbaya ya kutoweka kwa amani ya Tanzania.

``Rais ameelezea masikitiko yake, kwa kweli inasikitisha sana, mimi nawaomba viongozi wa dini na madhehebu yote wasimamie kuzuia mambo haya, nawaomba Watanzania wenzangu tusali kwa imani zetu kuomba amani yetu isipotee,” alisema.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, aliongeza kuwa Watanzania wameoleana, wamekuwa wakiishi pamoja kwa miaka yote bila kubaguana kwa misingi ya dini, rangi wala kabila, na kuhoji haya mambo yanatoka wapi.

Alisema kuwa Tanzania imekuwa ni mfano wa kuigwa kote dunia kutokana na amani iliyopo, ambayo ni matunda ya uongozi wa waasisi wa taifa hili hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Katika fujo hizo za Buseresere, mchungaji mmoja wa kanisa aliuawa baada ya kuzuka kwa mapigano kati ya Waislamu na Wakristo, chanzo kikiwa ni Wakristo kuamua kuchinja ng’ombe na kuuza kwenye bucha yao, hatua iliyopingwa na Waislamu.

Ujumbe huo uliofika nyumbani kwa Lowassa uliongozwa na msaidizi wa askofu mteule wa KKKT dayosisi hiyo, ulimshukuru kutokana na kusimamia na kuendesha harambee ya ujenzi wa kanisa kuu la Shinyanga Januari mwaka jana ambapo zaidi ya sh milioni 200 zikiwa ni fedha taslimu pamoja na ahadi zilipatikana.


Chanzo: kalulunga.blogspot.com

No comments:

Post a Comment