Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Monday, April 22, 2013

AMUUA BABA YAKE KWA KUMTUHUMU KUWA NI MSHIRIKINA...!

 
JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamsaka Richard Jecap (30) mkazi wa kitongoji cha Matai A kwa tuhuma za kumuua baba yake kwa kumpiga mpini kichwani  akimtuhumu kuwa ni mshirikina.
Tukio hilo lilitokea Aprili 18 saa 4.50 asubuhi wakati baba huyo akiwa amekaa nyumbani kwake akiota jua.

Akizungumza na gazeti hili, mwenyekiti wa kijiji hicho, Emmanuel Mwakibinga alisema kuwa mtuhumiwa alifanya mauaji hayo baada ya watoto wake kufariki ambapo mtoto wa kwanza mwenye umri wa miaka minne alifariki Januari mwaka huu na alikuwa akidai baba yake huyo ndiye aliyemloga.

Alisema kuwa Aprili 16 mtoto wake wa pili mwenye umri wa miaka miwili alifariki na alidai kuwa baba yake ndiye aliyemloga kwani amekuwa akiloga watoto wake hao na siku ya mazishi aliahidi kumfanyia kitu kibaya baba yake huyo licha ya kuwa hakueleza ni kitu gani.

Mwenyekiti huyo alisema siku ya tukio hilo alikuwa akipita karibu na nyumba hiyo akasikia kishindo kikubwa kutoka eneo la nyumba hiyo na kisha kufuatia vilio vya watu na aliposogea alikuta mtuhumiwa huyo amekwishampiga mpini kichwani baba yake huyo na kisha kuanguka na kupoteza fahamu.

Baada ya kuona hivyo, walisaidiana pamoja na wanafamilia wengine kumwahisha hospitali na alitundikiwa maji sambamba na kushonwa katika jeraha kubwa alilolipata kichwani na usoni na kisha kulazwa ili  kuendelea kupata matibabu.

Mwakibinga alisema kuwa wakati akiendelea kupatiwa matibabu alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi na maumivu makali aliyokuwa nayo katika jeraha alilolipata baada ya kupigwa na mpini wa shoka kichwani.

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment