Mambo mengine yakaonekana kufumuka. Watu wakaanza kulitolea macho gazeti la Pamoja ambalo lilikwa na kichwa cha habari kikubwa kilichoonekana kumvutia kila mtu ambaye alikuwa akiliangalia. Habari ile ikaonekana kumshtua kila mtu, hakukuwa na mtu aliyeamini kwamba mambo kama yale yangeweza kutokea kwa mara nyingine.
Gazeti hilo likanunuliwa mtaani kupita kiasi, kila mtu alikuwa
akiligombania. Kila mtu alitaka kujua hasa chanzo cha habari ile ambayo ilikuwa
ikimvutia kila mtu. Mpaka inafika saa sita mchana, gazeti lile halikuwa
likionekana mitaani.
‘VIONGOZI HAWA WATAFUNA MABILIONI YA WATANZANIA’ Kichwa cha
habari kilikuwa kinasomeka vizuri mbele kabisa ya gazeti hilo tena huku kikiwa kimeandikwa kwa
mwandiko mkubwa ambao hata kwa aliyekuwa na matatizo ya macho angeweza kuusoma.
Shauku ya kutaka kufahamu kwa kina juu ya habari ile ndio ambayo
iliwafanya watu kulinunua zaidi gazeti lile. Idadi kubwa ya wananchi ndani ya
jiji la Dar es Salaam walikuwa na nakala ya gazeti lile ambalo mara kwa mara
lilikuwa likizungumzia mambo yanayofanywa na viongozi wa Serikali
Ununuzi mkubwa wa gazeti hilo haikuwa Dar es Salaam tu, bali hadi katika
mikoa ya jirani, gazeti hilo
lilikuwa likigombaniwa kupita kiasi. Habari ile ilimsisimua kila aliyekuwa
akiiangalia. Hawakuamini kama viongozi ambao walikuwa wakiwaamini ndio ambao
walikuwa wamefanya wizi mkubwa wa mabilioni.
Watu hawakutaka kuishia kuisoma habari ile tu, kuna kitu ambacho
walitamani kukifahamu zaidi, jina la mwandishi ambaye alijitolea kuandika
habari ile. Jina la Dominick Hyera lilikuwa likionekana vizuri, mwandishi huyu
ambaye mara kwa mara alikuwa akiyaandika maovu mengi yaliyokuwa yakifanywa na
viongozi wengi alionekana kuyatoa sadaka maisha yake.
Kila Mtanzania alimuona mwandishi Dominick kuwa shujaa, shujaa ambaye
hakutaka kuona Watanzania wakiibiwa fedha zao ambazo walikuwa wakiziangaikia
katika kuzilipia kodi. Dominick alionekana kuwa radhi kupata tatizo lolote lile
ili mladi tu Watanzania wafahamu ni watu gani ambao walikuwa wakichukua fedha
ambazo walikuwa wakiziangaikia.
“Nitaendelea kuandika mambo haya hadi mwisho. Nitataka watu wote wabaya
wajulikane” Hayo yalikuwa maneno ambayo mara kwa mara Dominick alikuwa
akimwambia bosi wake.
Dominick hakuonekana kuogopa kitu chochote kile. Maisha ya dhiki ambayo
alipita katika kipindi cha nyuma ndio ambayo yalikuwa yakimfanya kuandika mambo
hayo. Dominick aliwachukia viongozi wezi kuliko kitu chochote katika maisha
yake.
Aliandika mambo mengi kipindi cha nyuma, wizi ambao ulitendeka katika
kila sekta nchini. Aliandika mambo mengi kuhusu EPA, Dominick hakufumbia macho,
aliandika mambo mengi kuhusu BoT. Dominick hakuishia hapo, kila wizi ambao
ulifanyika, aliuandika gazetini pasipo kujali kitu chochote kile.
Jina lake liliendelea kuwa maarufu, kila mtu alitamani kumuona Dominick.
Siku ambayo Dominick alionekana akihojiwa katika runinga, hakukuwa na mtu ambaye
aliamini kuwa ni yeye. Alikuwa kijana mdogo sana ambaye kwa mtazamo wa haraka haraka alikuwa
na miaka ishirini na tano.
Kila siku maisha yake yalikuwa ni kuwaweka wazi watu wote ambao walikuwa
wakitumia nyadhifa zao katika kuiba mamilioni ya Watanzania, ambao asilimia
zaidi ya tisini na tano walikuwa wakiishi maisha ya kimasikini.
Mtu pekee ambaye alikuwa akimtia moyo katika kazi yake alikuwa mke wake
mpendwa, Christina pamoja na mtoto wake, Ibrahim aliyekuwa na miaka mitatu.
Kila alipokuwa akiwaangalia watu hao, alijiona kupata nguvu ya kuandika mambo
mengi zaidi.
Hakutaka mtoto wake, Ibrahim apate matatizo kama yeye alivyopata
matatizo kipindi cha nyuma kwa viongozi kula fedha ambazo zilitolewa kwa ajili
ya kuendeleza elimu nchini Tanzania.
Alijiona kuwa na jukumu kubwa kuhakikisha wezi anawaweka wazi ili hata nafasi
ya kuiba mamilioni ya Elimu isiwepo tena.
Kila kiongozi alikuwa akimuogopa Dominick, alionekana kuwa adui namba
moja kwa viongozi ambao kazi yao
kubwa ilikuwa ni kuiba mabilioni ya fedha ambazo zilikuwa zikilipiwa kodi kutoka
kwa Watanzania.
Siku za Jumanne na Ijumaa hazikuwa zikikalika ofisini, watu walikuwa
mitaani kununua gazeti la Pamoja kujua ni mambo gani ambayo yalikuwa yametokea
kwa viongozi kwa wakati huo. Kila siku Watanzania walikuwa wakiumia,
hawakuamini kama fedha ambazo walikuwa wakizitoa kama
kodi zilikuwa zikiliwa kirahisi namna ile.
“Unajua kama leo ni sikukuu ya kuzaliwa ya Ibrahim?” Sauti ya Chrstina
ilisikika ikiuliza swali kupitia simu.
“Mungu wangu! Kumbe ni leo! Nilikuwa nimesahau kabisa mpenzi, mambo
mengi” Dominick alisema huku mkono wake mmoja akiutumia kushikilia usukani.
“Basi fanya haraka mpenzi. Fanya haraka kwa sababu wote hapa nyumbani
tumekumisi, njoo tusherehekee pamoja” Christina alimwambia mumewe, Dominick.
“Usijali. Ngoja nipitie madukani nikanunue zawadi” Dominick alimwambia
mkewe.
“Usichelewe....”
“Usijali, nitawahi mpenzi”
“Nakupenda”
“Nakupenda pia” Dominick alijibu na kukata simu.
Ingawa alikuwa safarini kurudi nyumbani, akakata kona na kuanza kuelekea
katika maduka ambayo yalikuwa yakiuza vitu mbalimbali ambavyo vilikuwa
vikitumika kama zawadi katika sherehe
mbalimbali. Mara baada ya kufika katika eneo la maduka hayo, akasimamisha gari
na kuteremka.
“Nahitaji midoli kwa ajili ya mtoto wangu, na ni vizuri kama itakuwa na ujumbe wa siku ya kuzaliwa” Dominick
alimwambia muuza duka.
“Midoli ipo. Ipo ya aina mbalimbali na yenye jumbe tofauti tofauti”
Muuza duka alimwambia Dominick huku akichukua baadhi ya midoli na kumkabidhi.
Dominick akaanza kuiangalia baadhi ya midoli ile, aliyoiona inafaa,
akaichukua na kuondoka dukani hapo huku ikiwa imetimia saa kumi na mbili na
nusu jioni.
Foleni ya magari kuanzia Ubungo ilikuwa kubwa mpaka Manzese Tip Top.
Dominick alionekana kuchoka, tayari alijiona akichelewa kufika nyumbani. Kila
wakati alikuwa akilalamika peke yake, foleni ilionekana kumchosha kupita kiasi.
Muda ulizidi kwenda mbele lakini hakukuwa na dalili ya foleni kusogea
mbele kutokana na magari ambayo mara kwa mara yalikuwa yakijiingiza. Foleni
ilidumu kwa dakika arobaini, magari yakaanza kusogea kwa mwendo wa taratibu.
Magari yalitembea kwa mwendo wa taratibu kwa dakika moja lakini yalikuwa
yakisimama kwa dakika ishirini. Mpaka wanafika Ubungo na kupavuka tayari
ilikuwa imetimia saa mbili kasoro. Dominick akaonekana kukasirika kupita kiasi.
Kutoka Ubungo mpaka Kimara mwisho wala hakuchukua muda mrefu, ni ndani
ya dakika nne tu akawa amekwishafika. Akakata kona na kuanza kuingia barabara
ya vumbi na kuendelea na safari ya kuelekea nyumbani.
Huku akiwa njiani, ghafla akasikia king’ora kikilia. Kwa haraka sana akaliegesha gari lake pembeni
na gari lile la kitengo cha zima moto kupita.
“Wanajifanya wana haraka sana
na wakati utakuta nyumba yenyewe imekwishateketea” Dominick alisema huku akiachia
tabasamu la chini.
Akaendelea na safari yake ya kwenda nyumbani. Kila wakati alikuwa
akiiangalia midoli aliyoiweka katika kiti cha pembeni. Furaha kubwa ilikuwa
moyoni mwake, alimini mkewe, Christina angezifurahia zawadi zile kwa ajili ya
mtoto wake, Ibrahim ambaye alikuwa akifikisha umri wa miaka mitatu.
Dominick aliendelea na safari, moshi mkubwa ukaanza kuonekana mbele yake
huku mwanga wa moto uliokuwa ukiendelea kuwaka ukizidi kuongezeka. Dominick
akaonekana kuwa na wasiwasi, akaongeza kasi ya gari lake.
Akakata kona ya njia ya kuelekea nyumbani kwake. Watu walikuwa wengi
wakikimbilia katika njia ambayo alikuwa akiitumia kufika nyumbani kwake.
Dominick akapigwa na mshtuko mara baada ya macho yake kutua katika nyumba ambayo
ilikuwa ikiteketezwa kwa moto, ilikuwa nyumba yake.
“Christina.....” Dominick akajikuta akiita.
Hakuamini macho yake kama nyumba yake
ndio ambayo ilikuwa ikiendelea kuteketea kwa moto. Kwa kasi ya ajabu akateremka
kutoka garini na kuanza kupiga hatua kuelekea kule ilipokuwa nyumba yake huku
akionekana kuchanganyikiwa.
Majirani zake ambao walikuwa wakiiangalia nyumba ile, walipomuona,
wakamzuia. Dominick akaanza kupiga kelele huku akionekana kuchanganyikiwa
zaidi. Majirani ambao walikuwa wamemshika upande wa kulia na kushoto wakamshika
zaidi.
“Christinaaaaaaa..... Christinaaaaa... Ibrahimmmmm...” Dominick aliita
huku akiwa amechanganyikiwa.
Watu kutoka katika kitengo cha Zima moto bado walikuwa wakiendelea na
kazi ya kuuzima moto ambao ulikuwa umeiteketeza nyumba ile. Kila mtu akaonekana
kuchanganyikiwa, hawakuelewa sababu iliyosababisha moto ule.
“Au shoti ya umeme ilipiga?” Kijana mmoja alimuuliza mwenzake.
“Mmmh! Sidhani. Nafikiri kuna mtu atakuwa ameichoma moto” Kijana
mwingine alijibu.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Hauisikii harufu ya petroli?”
“Mhhhh! Inawezekana”
Zoezi la kuzima moto liliendelea zaidi na zaidi. Dominick alikuwa akilia
kama mtoto, alitamani achoropoke kutoka katika mikono ya watu waliokuwa
wamemshika lakini watu wale walikuwa wamemshika vilivyo.
Moto ulizimwa, hakukuwa na kitu chochote ambacho kilikuwa kimesalia,
kila kitu kilikuwa kimeteketezwa kwa moto. Watu wakasubiri joto lipungue na
ndipo waingie ndani. Walikaa kwa takribani dakika ishirini baada ya moto
kuzimwa na ndipo wakaingia ndani ya nyumba ile ambayo tayari ilikuwa gofu.
Dominick akatamani aingie pamoja nao lakini watu wale waliomshika
hawakutaka kumuachia. Baada ya dakika fulani maiti ya Christina na Ibrahim
zikatolewa huku zikiwa zimefunikwa kwa kanga. Dominick akajikuta akipata nguvu
za ziada, akajitoa mikononi mwa watu wale na kuanza kuwafuata watu wale
waliobeba maiti ya mkewe, Christina na mtoto wake, Ibrahim.
“Christina.... Christina mke wangu...” Dominick aliita mara baada ya
kuwafikia watu wale waliobeba maiti.
“Christina...Christina...” Dominick aliita huku akiwa haamini kile
ambacho kilikuwa kimetokea.
“Ebu angalieni yale maneno pale” Jirani mmoja alisikika akiwaambia
wenzake waangalie maneno ambayo yalikuwa yameandikwa getini.
‘BoT’ Maneno yale
yalisikika.
Dominick akageuka na kuangalia kule getini, maneno yale yalikuwa
yakisomeka vizuri machoni mwake. Akaonekana kugundua ni kitu gani ambacho
kilikuwa kinaendelea kwa wakati huo.
*********
Mara baada ya kukata simu, Christina akaanza kufanya maandalizi kwa
ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mtoto wake, Ibrahim. Kwanza akampeleka kumuogesha na kisha kumvalisha nguo
nzuri ambazo zilionekana kumvutia hata yeye mwenyewe.
Christina akaingia jikoni ambako akaandaa chakula kizuri ambacho
aliamini kingemfurahisha mumewe. Mara baada ya kumaliza kupika, akakipeleka
chakula mezani.
Muda ulizidi kwenda mbele lakini bado Dominick hakuweza kuwasili.
Christina aliendelea kusubiri zaidi na zaidi, wakati mwingine alitamani
kumpigia simu kujua ni mahali gani alipokuwa na kama zawadi alikwishanunua,
lakini kila alipotaka kufanya hivyo, alisita.
Muda ulizidi kusogea, mara kwa mara alikuwa akiangalia mishale ya saa
kubwa ya ukutani, hasa mshale wa dakika, aliona muda ukizidi kusogea lakini
wala mumewe hakuwa amefika nyumbani.
“Fanya haraka mpenzi...” Christina alijikuta akiongea peke yake.
Wala hazikupita dakika nyingi, akashtukia mlango ukigongwa. Christina
akashtuka, hakuelewa ni nani ambaye alikuwa akigonga mlango wakati huo. Wazo la
mumewe likamjia kichwani, lakini likapotea ghafla mara baada ya kugundua kuwa
hakuwa amesikia muungurumo wa gari wala geti kufunguliwa.
Swali juu ya mtu ambaye alikuwa akigonga mlango lilikuwa
likijirudiarudia kichwani mwake kila nukta ambayo ilisogea. Akainuka kutoka
katika kiti alichokuwa amekaa na kuufuata mlango.
Christina akapigwa na mshtuko mara baada ya kuufungua mlango na macho
yake kutua katika uso ambao ulikuwa umefunikwa kwa kutumia kinyago. Hata kabla
Christina hakuchukua uamuzi wa kupiga kelele, akajikuta akizibwa mdomo.
Vijana wengine ambao nao nyuso zao zilikuwa zimefunikwa na vinywago
wakaingia ndani. Christina akawekwa kochini na kuamriwa kutokupiga kelele
zozote zile. Akabaki akitetemeka kama mtu
ambaye alikuwa akisikia baridi kali.
Muda wote Christina alikuwa akilia, hakuelewa ni kitu gani ambacho
kilikuwa kinaendelea mahali hapo. Kijana mmoja akamfuata Ibrahim ambaye alikuwa
amewekwa katika kochi la pembeni, alipomfikia, akambeba na kumpelekea
Christina.
***************************************************
USIKOSE KUANGALIA MUENDELEZO WA HADITHI HII..
No comments:
Post a Comment