Dodoma: Wabunge wa CCM wamekuja juu na kumtaka Rais Jakaya Kikwete
kuwafukuza kazi vigogo wa Serikali mkoani Mtwara, wakiwamo Mkuu wa Mkoa
na Mkuu wa Wilaya kutokana na kile walichoeleza ni uzembe uliochangia
vurugu zinazoendelea za wananchi kugomea gesi kutoka nje ya mkoa huo.
Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakifanya doria katika mitaa ya Mji wa Mtwara
Wengine waliopendekezwa kuchukuliwa hatua ni kamati nzima ya ulinzi na
usalama ya ngazi ya mkoa na wilaya ya Mtwara mjini, wakiwamo makamanda
wa polisi.
Kutokana na hali hiyo, vigogo kadhaa mkoani humo wako hatarini kukumbwa
na ghadhabu hiyo akiwamo Mkuu wa vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mkuu wa mgambo na Mkuu wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wabunge hao walikuwa wakitoa mapendekezo hayo kwenye kikao cha Kamati ya
Wabunge wa CCM iliyofanya kikao cha dharura juzi usiku, mjini hapa.
Kikao hicho kiliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Spika wa
Bunge, Anne Makinda ambaye wakati huo alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya
Uongozi wa Bunge, aliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Jenista
Mhagama.
Katika kikao hicho maalumu kilichokusudia kutoa ushauri kwa Rais Kikwete
juu ya njia mwafaka ya kutatua hali ya machafuko, wabunge wengi wali
kukasirishwa na jinsi hali ilivyo mkoani Mtwara.
Chanzo chetu kwenye kikao hicho kilieleza kuwa wabunge hao walichukizwa na jinsi Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walivyokuwa wakipingana kimsimamo. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Joseph Simbakalila, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile na Kamanda wa Polisi Mkoa Linus Sinzumwa wamehusishwa.
Chanzo chetu kwenye kikao hicho kilieleza kuwa wabunge hao walichukizwa na jinsi Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walivyokuwa wakipingana kimsimamo. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Joseph Simbakalila, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile na Kamanda wa Polisi Mkoa Linus Sinzumwa wamehusishwa.
Licha ya baadaye kuonekana kuwa kitu kimoja, wabunge hao walidai kuwa
walishindwa kutumia nafasi zao katika kutatua tatizo hilo, ambalo hadi
juzi Serikali ilisema walikuwa wamekufa watu watano, wakiwamo wanajeshi
wa JWTZ waliofariki katika ajali wakati wakienda kutuliza machafuko.
Chanzo hicho kilieleza kuwa iwapo mapendekezo ya wabunge hao yatapelekwa
kwa Rais Kikwete kama michango ya wabunge hao ilivyokuwa, huenda rungu
likawaangukia pia viongozi wa kisiasa wa CCM mkoani humo. Miongoni mwa
wanasiasa hao, chanzo hicho kimesema ni wale waliotoa kauli za waziwazi
kuunga mkono msimamo wa kutoruhusu gesi kusafirishwa nje ya mkoa huo.
“Hapa wapo wabunge, madiwani na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walipendekeza mkakati wa kutatua uzembe
uliofanyika Mtwara, unapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu usije
ukasababisha madhara mengine kwa Chama na Serikali.
Walisema suala hilo halina budi kuchukuliwa kwa uangalifu hasa
ikizingatiwa kuwa Chama cha CUF ndicho chenye nguvu mkoani humo
ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani.
Wabunge hao walikituhumu chama hicho kuwa kimekuwa kikijaribu kutumia
vurugu hizo kama kigezo cha ushawishi wa kukubalika mkoani humo.
No comments:
Post a Comment