Wakati Jeshi la Polisi nchini
limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika
mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Arusha,Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
source:/freebongo (38)
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao
watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama
kwenye msiba huo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto
kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi
wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.
Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk
Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari,
alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa
mkono (grumeti) na hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna
wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na
uchunguzi wa tukio hilo.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi
(IGP), Said Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi
kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na
kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili
na 68 ni majeruhi.
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema,
Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja
la Justin.
“Mpaka hivi sasa watu waliokufa ni wawili na wengine 68
wamejeruhiwa na mlipuko huo, lakini naahidi kuwa tutapambana na
kuhakikisha tunawapata wahusika,” alisema Mwema.
Sanjari na kupatikana taarifa juu ya mtu aliyetupa bomu, Mwema
alisema timu ya jeshi hilo imetumwa kutoka makao makuu kwenda Arusha
kuongeza nguvu katika upelelezi.
Hata hivyo, hakufafanua zaidi juu ya mtuhumiwa huyo kutokana na
kile alichosema taarifa husika zinafanyiwa uchunguzi kabla ya
kuwakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo.
Kwa mujibu wa IGP Mwema, timu ya polisi kutoka Makao Makuu
inayoongozwa na makamishna wawili, imeondoka kwenda mkoani Arusha
kuongeza nguvu katika operesheni na upelelezi.
Timu hiyo inaongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul
Chagonja na Isaya Mngulu kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai,
wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi.
Alisema polisi inafanya operesheni kali nchini kote kuhakikisha
inawatia mbaroni watu wote waliowezesha, waliofadhili na waliotenda
uhalifu huo.
“Kikubwa wananchi waendelee kuwa watulivu na waendelee kutoa ushirikiano kwa wakati wote uchunguzi ukiendelea,” alisema.
IGP ametaka mtu yeyote atakayekuwa na taarifa za wahalifu hao, atoe taarifa kupitia namba yake ya simu ambayo ni 0754 785557 au kwenye kituo chochote cha polisi ili wakamatwe.
‘Kwa nini iwe Arusha’ hii ni kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Mulongo aliyoitoa baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali za Mount
Meru, St Elizabeth pamoja na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical
Centre jijini.
“Nawapa pole sana ndugu zangu wa Chadema, na wana Arusha kwa ujumla
pamoja na watanzania. Lakini najiuliza kwa nini Arusha …tukio hili
limenihuzunisha sana na nawaomba tusiingize masuala ya kisiasa, tuache
polisi wachunguze tukio hili kwani timu ya wataalamu kutoka Jeshi la
Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) pamoja na wataalamu wengine
wanachunguza tukio hili na wahusika watachukuliwa hatua.’’
Mulongo ambaye tukio hilo la juzi limekuja ikiwa ni mwezi mmoja
tangu kutokea kwa mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la
Olasiti, alisema jana anayefanya ulipuaji wa mabomu na kumwaga damu za
watu mbalimbali na wengine kufa, ipo siku Mungu atamhukumu.
Kati ya majeruhi 59 waliolazwa kwenye hospitali hizo, wawili
wamehamishiwa Hospitali ya KCMC kutoka Hospitali ya AICC kwa matibabu.
Wagonjwa wengi wamelazwa hospitali ya Selian ambao ni 40. Hata hivyo,
wanane waliruhusiwa baada ya matibabu.
Mkuu wa Mkoa alisema anajisikia mnyonge kutokana na matukio hayo
mawili tofauti; mlipuko wa kanisani na la juzi wakati Chadema ilipokuwa
ikihitimisha kampeni zake za udiwani kwenye kata nne za Themi, Kaloleni,
Elerai na Kimandolu ambao hata hivyo uliahirishwa kutokana na tukio
hilo.
Mulongo alitaka wananchi wasihusishe na masuala ya kisiasa badala
yake wawaachie polisi kuchunguza tukio hilo. Kwa mujibu wa Mulongo, watu
kadhaa wamekamatwa.
Katika kipindi kisichozidi miezi miwili, mji wa Arusha umeshuhudia
majeruhi wasiopungua 130, na vifo vya watu watano vilivyotokana na
kurushwa mabomu na watu wasiojulikana katika mikusanyiko kanisani na
kwenye mkutano huo wa siasa wa Chadema.
Katika tukio la mwezi uliopita katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu
Joseph Mfanyakazi, watu watatu walifariki na wengine wapatao 59
kujeruhiwa.
Mmoja wa watuhumiwa ambaye ni dereva wa pikipiki maarufu kama
bodaboda, Victor Ambrose alifikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika
katika shambulio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, daktari wa hospitali ya Selian,
Paul Kisanga alisema walipokea wagonjwa 48 kabla ya wanane kuruhusiwa.
Alisema miongoni mwa wagonjwa hao, wamo watoto watano wanne wakiwa
wa kiume na mmoja wa kike. Mtoto Fahad Jamal (7) amelazwa kwenye wadi
ya wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa madaktari.
Hospitali ya St Elizabeth wapo wagonjwa wanane na Mount Meru
imepokea wagonjwa tisa. Mganga Mkuu wa Mkoa wa hospitali ya Mount Meru,
Frida Mokiti alisema wamepokea miili ya marehemu wawili ambao ni Judith
Moshi (25) ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) kata ya
Sokoni 1, Jijini Arusha pamoja na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la
Justin (13).
Kwa mujibu wa majeruhi wa tukio hilo, Abraham Samuel waliona kitu
kikiwa kwenye mfuko wa rambo kikirushwa juu na baada ya muda mfupi
walisikia vilio na wengine kuzimia.
Kitu hicho kilirushwa kabla ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho
Taifa, Freeman Mbowe kuhitimisha kampeni za uchaguzi za udiwani wa kata
nne za Jimbo la Arusha Mjini.
Mlipuko huo unadaiwa kuwa ulitokea jirani na gari la matangazo la
Chadema, aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa karibu na jukwaa alilokuwa
akitumia Mbowe.
Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe amedai tukio hilo si la bahati mbaya bali lilipangwa na kundi la watu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema wabunge wa chama
hicho leo hawataingia bungeni bali watawasili jijini Arusha kwa ajili ya
kuungana na wananchi pamoja na wanachama wa kwenye msiba huo.
Kwa mujibu wa Mbowe, marehemu Judith atapelekwa mkoani Kilimanjaro
na Justin atapelekwa mkoani Tabora kwa ajili ya maziko mara baada ya
polisi kukamilisha uchunguzi juu ya tukio hilo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto
kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi
wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo marehemu hao watasafirishwa.
‘’Nimetembelea majeruhi jana hospitalini lakini kwa Hospitali ya
Selian, Arusha Lutheran Medical Centre majeruhi ni wengi lakini
walioumia sana ni watoto kuna mtoto mmoja amekatika mkono na mguu ambaye
ni Sharifa Jumanne na Amiri Ally ana vyuma vitatu mwilini mwake,’’alisema Mbowe.
Ingawa polisi imesema inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kabla
ya kutoa taarifa kamili, Mbowe aliwaambia waandishi wa habari kwamba
zipo taarifa kwamba shambulio hilo liliambatana na risasi za moto.
Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Profesa
Ibrahim Lipumba, kimelaani tukio hilo na kutaka Serikali ichukue hatua
za haraka na kukamata waliohusika na matukio hayo iwe fundisho.
“Hatuna sababu na tusijenge utamaduni wa nchi yetu kugeuka eneo
ambalo palipo na mkusanyiko mabomu yanalipuka, Tanzania ni nchi ya
amani, kwa matukio haya CUF tunalaani kwa nguvu zote na kutoa pole kwa
familia zilizoathirika,” alisema Lipumba.
Lipumba alisema kitendo kilichofanyika katika mkutano huo wa
Chadema ni unyama wa kutisha wenye makusudi ya kundi fulani kutekeleza
azma yao dhidi ya chama, watu, kundi na viongozi.
Alisisitiza kuwa utamaduni huo wa kufanya unyama katika mkusanyiko
wa watu unapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha madhara mengine ndani
ya jamii kwa kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu na familia tegemezi.
“Tumefikia hatua mbaya sana ya kufanya siasa za mabomu huu ni
utamaduni unaopaswa kukemewa na kupingwa, matukio haya yanajirudia
kutokana na Serikali yenyewe kuyakaribisha kwa kushindwa kuwachukulia
hatua kali wahusika, tunaomba dola ifanye ifanyalo katika uchunguzi wake
na kuwakamata na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment