Moja ya ajali zilizowahi kuhusisha mabasi ya Princess Muro mkoani Tabora. |
Abiria zaidi ya 50 wilayani Nzega
mkoani Tabora wamenusurika kupoteza maisha baada ya basi walilokuwa
wakisafiria kuungua moto kutokana na hitilafu ya kiufundi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Peter Ouma alisema moto huo ulioteketeza mizigo yote ya abiria, ulitokea juzi saa 4 usiku katika kijiji cha Nata kwenye basi la Princess Muro.
Alisema gari hilo aina ya Scania lenye namba za usajili T 6766 CEH, lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza likiwa linaendeshwa na dereva Boniface Francis.
Alisema likiwa na mwendo wa kawaida, lilianza kuwaka moto ndipo kondakta
pamoja na dereva waligundua na kulisimamisha.
Abiria walifanikiwa kushuka wakiwa salama isipokuwa mizigo yao iliteketea kwa moto. Jitihada za kuuzima zilishindikana kutokana na eneo ilikotokea ajali hiyo kukosa kikosi cha zima moto na uokozi.
Kwa mujibu wa kamanda, kulitokea hitilafu kwenye injini ya gari hilo hali iliyosababisha moto. Hakuna mtu alijeruhiwa.
Kamanda amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri hususani vya kusafirisha abiria, kufanya ukaguzi na kuvikarabati kwa nyakati tofauti kuepusha ajali.
No comments:
Post a Comment