Siku tatu
baada ya Rais Jakaya Kikwete kuponda mpango wa Chadema kuanzisha kambi
kwa ajili ya mafunzo ya ulinzi kuwalinda viongozi na wanachama wake,
chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimeibuka na kusema kuwa
kinaendelea na mpango huo na kambi hizo zitaanza rasmi wiki ijayo.
Kimesema
hakitishwi na kauli ya Jeshi la Polisi kukionya juu ya uanzishwaji wa
mafunzo hayo, kwamba jeshi hilo linatakiwa kuanza kukizuia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kwanza, kwa maelezo kuwa chama hicho tawala pia kina
kikundi cha ulinzi ‘Green Guards’ ambacho kinafanya mafunzo ya kijeshi,
huku kikitumia silaha za moto.
“CCM ndiyo
wataipeleka nchi hii pabaya, wanawafundisha vijana huku wakiwabebesha
bunduki, wanajenga taifa la aina gani, bunduki ni silaha ya kivita sasa
wanaandaa watu kupigana na nani” alisema Mkurugenzi wa Organaizesheni
na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira jana wakati akizungumza na
wanahabari huku akionyesha picha za mafunzo ya CCM, zinazoonyesha vijana
wakiwa wamebeba silaha (hata hivyo ni mbao zilizotengenezwa kwa mfano
wa bunduki).
Wakati Chadema wakieleza hayo, CCM kimeshtushwa na taarifa hizo na kueleza kuwa hali hiyo sasa inahatarisha usalama wa nchi.
Katibu Mkuu
wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Martin Shigela alisema ni
vyema Chadema kikawaambia wananchi wawalinde, kuliko kuanzisha mafunzo
huku akimtaka Msajili wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa kulitizama
kwa kina suala hilo.
Akifunga
Kongamano la Amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD), Dar es Salaam Julai 10, mwaka huu, Rais Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM Taifa pia alikosoa kitendo cha Chadema kususia
kongamano hilo alisema, “Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati
hawapendi tuzungumze wanataka watu wauane, wapigane.”
Mbali na
Rais Kikwete, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SSP Advera Senso juzi
alikionya chama hicho kuhusu mpango huo akisema kuwa kitendo cha chama
chochote cha siasa kikiwemo Chadema, kuanzisha kikundi cha kujihami ni
kinyume na sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli ya
jana ya Chadema ni mwendelezo wa ile iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama
hicho Freeman Mbowe Julai 9, mwaka huu, ambapo alisema kimechukua hatua
hiyo baada ya Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kushindwa
kufanyia kazi malalamiko yao kuhusu mauaji, vitisho na matukio ya
kutisha wanayofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wao.
Katika
ufafanuzi wake Kigaila alisema Chadema hakianzishi vikundi vya kijeshi,
bali mafunzo ya kuwafundisha walinzi wa chama hicho ‘Red Brigade’,
jinsi ya kujilinda.
“Kwa mujibu
wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki kwa raia yeyote
kujilinda, Chadema ni taasisi ni haki yetu kuilinda taasisi yetu ndiyo
maana tumesajili kikundi chetu cha ulinzi, sasa nani anatutisha,
tunataka polisi waanze na CCM kwanza ambao katika mafunzo yao
wanafundisha hadi kupiga saluti na kutumia silaha,” alisema.
Alisema
mafunzo hayo yataanza rasmi wiki ijayo, huku akisita kutaja siku
yatakayoanza, wala mikoa yatakayofanyika na kusisitiza kuwa hayo
yatatangazwa wiki ijayo wakati vijana wakienda katika mafunzo.
Tuhuma
Alisema
kabla ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka 2011, CCM kilianzisha
kambi ya vijana eneo la Ulemo wilayani Iramba katika Jimbo la Iramba
Magharibi na kwamba kambi hiyo ilikuwa na vijana 200.
Alifafanua
kwamba katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga CCM ilianzisha kambi
katika wilayani Nzega, Tabora, Shinyanga na Singida Mjini za kambi hizo
zilikuwa na vijana 800.
“Vijana hao
walipelekwa katika uchaguzi wa Igunga na kusababisha kifo cha kada wa
Chadema, Msafiri Mbwambo ambaye alikuwa wakala wa chama katika uchaguzi
huo, awali tuliwaeleza polisi jinsi kambi hizo zilivyowekwa, lakini
hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka leo,” alisema.
Alisema
mwaka jana CCM ilifanya mafunzo ya kitaifa ya vijana wao wa ‘Green
Guards’ mkoani Mwanza na baada ya mafunzo hayo walifanya gwaride la
kijeshi.
Alisema
wakati vijana hao wakihitimisha mafunzo hayo walikaguliwa na Mwenyiki wa
Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho
Bara, Phillip Mangula pamoja na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, huku
wakipigiwa saluti na vijana hao waliokuwa wamebeba ‘matoi’
yaliyotengenezwa kwa mfano wa bunduki.
“CCM
wanasema kuwa Green Guards wanafundishwa ujasiriamali, hivi watu
wanaofundishwa ujasiriamali huwa wanapigiana saluti, huwa wanabeba
‘matoi’ yenye mfano wa bunduki,” alihoji.
Alisema
kambi za CCM zilianza tangu mwaka 2007 wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Kiteto, na kufafanua kuwa katika uchaguzi huo baadhi ya viongozi wa
Chadema akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Hamad Musa
Yusuf walipigwa na Green Guards huku polisi wakishuhudia.
Kauli ya CCM
Uanzishwaji
wa mafunzo hayo umeonekana wazi kukitesa CCM ambapo jana Shigela
alisema “Chadema kabla ya kuanza kutoa mafunzo hayo kwa vijana hao (Red
Brigade) wanatakiwa kuwaeleza wananchi dhamira halisi ya kuanzishwa
kwake, kama siyo kuchochea uvunjifu wa amani.”
“Chadema ni
chama cha siasa, kinaomba kuwatumikia wananchi wanaowapigia kura wenyewe
hivyo kama wanaona hawatendewi haki na polisi wawaambie wananchi
wenyewe wawalinde lakini si kuanzisha, kutoa mafunzo hayo kwa vijana.”
Habari na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Irene Mossi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment