Banner

Banner

FOLLOW US FACEBOOK

propertyfinder.co.tz

Saturday, July 13, 2013

HOSPITALI YA MOI YAJIBU MADAI YA BODABODA KUKATWA MGUU...!

Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa  Muhimbili (MOI), inayodaiwa kuchangia kuongeza ‘ walemavu’ kwa kuwakata viungo majeruhi wa ajali za boda boda, imesema ipo tayari kuthibitisha kuwa waliokatwa viungo si madereva wa pikipiki kama inavyodaiwa.  “Anayetaka kufahamu ukweli tuwasiliane.Takwimu za waliokatwa  miguu na viungo zipo hatuna cha kuficha  tena si madereva wa pikipiki  kama inavyodaiwa,” Ofisa Uhusiano wa  MOI, Almasi Jumaa, alisema.

Wanaotoa tuhuma hizo wanadai wodi ya kuchangia huduma, waganga wanawakata  miguu majeruhi wengi  wa ajali  za bodaboda na hulazwa kwenye wodi maalumu zinazojulikanazo kiutani kama  ‘boda boda na Sanlg’ .
Akijibu madai hayo Jumaa aliongeza:“uamuzi wa kumkata majeruhi kiungo haufanywi kinyemela ni makubaliano ya jopo la madaktari,  hukatwa kiungo  baada ya  daktari wa mgonjwa kupendekeza kwa wakuu wake  ambao huwasiliana na mabingwa wanaomchunguza mgonjwa na kuridhika kuwa  ili kuokoa maisha yake wanalazimika kuondoa kiungo.”
Alisema majeruhi wanaopokelewa MOI wanatibiwa  na kuhudumiwa bila kubaguliwa  na kwamba hakuna wodi ya boda boda wala Sanlg na anayetaka uhakika afike MOI kuthibitisha.
Aliongeza kuwa ukataji viungo huzingatia viwango vinavyokubaliwa kimataifa na kwamba unafanyika pale ambapo mgonjwa ameumia na hawezi kutibika.
Katika mahojiano na baadhi ya majeruhi na jamaa zao hospitalini hapo walibainisha kuwa hawaridhishwi na moyo wa madaktari na wauguzi katika kuhudumia wagonjwa.
Majeruhi wa boda boda walisema madaktari wanawapuuza, huchelewa kuwatibu hali inayowasababishia maumivu makali licha ya kwamba wapo hospitalini.
Walisema kutotibiwa kwa haraka husababisha viungo kuharibika,  kukatwa
na wengine kupoteza maisha na kudai kuwa katika wodi  ya wagonjwa wanaochangia huduma za afya, majeruhi hulundikana kupindukia.
Walisema baadhi huambukizwa hata maradhi  ya wodini  pia kuna harufu mbaya inayotokana na ama vidonda vyenye usaha sivyosafishwa au uchafu wa shuka zilizochafuliwa na damu na pia majeruhi  kutooga kutokana na kuumia viungo.
Walidai madaktari huwakimbia wagonjwa wakitoa mfano kuwa ukifika hospitalini hapo unapewa daktari atakayekuelekeza vipimo na dawa.
Hata hivyo  baadaye tabibu huyo hutoweka na mgonjwa  kupigwa dana dana na kulazimika kumtafuta mwingine ambaye anakerwa na kuhoji sababu za kukimbiwa na daktari wake hali inayomfanya mgonjwa kutapatapa kusaka huduma.
Walisema jamaa za wagonjwa huzunguka kila mahali kuwatafuta madaktari ambao nao hawaonekani.
Walidai MOI haina dawa na pia hakuna gozi wala dawa za maji za kusafishia vidonda.
Baadhi walidai hakuna umakini wa kumfuatilia mgonjwa ambaye anaweza kuvalishwa mhogo (pop) mara kadhaa na mguu wake usiunge.
Pia walidai iliwahi kutokea  baadhi ya wataalamu wa dawa ya usingizi (nusu kaputi) walimwekea mgonjwa dawa kidogo na kusababisha kuzinduka kabla ya upasuaji kukamilika.
“Walilazimika kumuongezea mgonjwa  nusu kaputi iliyomzidia na kusababisha kifo ,” alidai mgonjwa  mmojawapo.
UFAFANUZI 
Akijibu malalamiko hayo  Jumaa alisema  wodi ya wagonjwa wa kuchangia huduma ina vitanda 33 lakini idadi ya majeruhi wanaolazwa inafikia zaidi ya 60 hali inayosababisha  mlundikano na harufu wodini.
Alitoa takwimu za wagonjwa zilizoonyesha kuwa kati ya 1996-1997 waliolazwa walikuwa  5,000 wakati wagonjwa wa nje walikuwa 6,700 na kwa  mwaka 2011 na 2012 wagonjwa waliolazwa walikuwa 7,070 wakati wa nje walikuwa  62,000.
Alisema hospitali hupokea  majeruhi angalau 10 kila siku na kwamba kila ajali kubwa majeruhi hufikishwa MOI hali inayosababisha msongamano na foleni  hata kwenye upasuaji.
Alisema hakuna uhaba wa madaktari wa mifupa na kuhudumia wagonjwa wa ajali kama inavyodaiwa na kwamba taasisi hiyo inawasaidia majeruhi  kwa kuwapa tiba,chakula na hata kuwafikisha kwao wakipona.
 
Habari na Gaudensia Mngumi. 
Source: Nipashe

No comments:

Post a Comment